Waziri wa Afya ,Ummy Mwalimu amesema serikali ya awamu ya sita imetoa kiasi cha Sh trilioni 6.722 ndani ya miaka mitatu ili kuboresha sekta ya afya hivyo sekta ya afya inakwenda mbele na namba inawabeba.
Mambo makubwa 11 katika kipindi cha miaka mitatu ikiwemo uboreshaji mkubwa wa miundombinu, huduma ya afya ya uzazi na matibabu ya kibingwa.
Maeneo mengine ni vifaatiba, vitanda vya wagonjwa ,dawa, rasilimali watu,magonjwa ya kuambukiza, ugharamiaji wa huduma na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam wakati akileza mafanikio ya sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu Ummy amesema vituo vya kutolea huduma vimeongezeka kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi 9,610 Machi 2024 sawa na ongezeko la vituo 1,061.
Amesema ongezeko hilo linahusisha zahanati 7,999, vituo vya afya 1,170, hospitali za halmashauri 172, hospitali zenye hadhi ya wilaya 181, hospitali za rufaa za mikoa 28, hospitali zenye hadhi ya mkoa 36, hospitali za rufaa za kanda tano, hospitali zenye hadhi ya kanda 12, hospitali maalumu sita na hospitali ya taifa moja.
“Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara na awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, na hospitali mpya za halmashauri 127 zimejengwa.
Ummy amesema serikali imenunua vifaa tiba vya Uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya Sh bilioni 290.9 ambavyo ni MRI sita,CT Scan 32 kwenye hospiali za Mikoa ambapo watu 15386 walipata huduma,Mini Angio suit moja ,Fluoroscopy moja,Ultrasound 192,Digital X-ray 199,Echocardiogram saba,pet scan moja na Cathlab tatu.
Amesema idadi ya vitanda vya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeongezeka kutoka vitanda 86,131 mwaka 2021 hadi vitanda 126,209 Machi 2024.
Vilevile amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa wodi 45 za wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ngazi ya Taifa, Maalum, Kanda na Mkoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba.
“Pia Serikali inaendelea na ujenzi wa ICU 28 katika ngazi ya Halmashauri ambapo 27 kati ya hizo zimekamilika na moja (1) iko hatua ya ukamilishaji sasa vitanda viko 1,362 kutoka 258.
Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitatu, wastani wa Sh bilioni 20 zimekuwa zikitolewa kila mwezi kwaajili ya dawa ambapo sasa zinapatikana kwa asilimia 84 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 58 mwaka 2022.
“Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 727 ambapo hadi sasa jumla ya 327 yamepokelewa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma.
Amesema jumla ya wataalam 35,450 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.
“Jumla ya ajira za mikataba kwa watumishi wa Afya 2,836 kupitia miradi mbalimbali ya Serikali zilitolewa.