Na Suzy Butondo, JamhuriMedia, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Annamlingi Macha amewataka viongozi na wataalamu kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuacha kucheza kamali na kushinda kwenye kahawa, badala yake wathamini muda kwa kufanya kazi kwa bidii, kwani maisha ni muda.
Rai hiyo ameitoa leo kwenye hafla ya makabidhiano ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika mjini hapa, ambapo amesema vijana wengi wamekuwa wavivu kufanya kazi na wanapopewa fedha za mikopo wanapeleka kucheza kamali na wengine kushinda kwenye kahawa, kufanya hivyo ni kurudisha maendeleo kuanzia kwenye famialia hadi Mkoa.
“Ili uchumi wa mkoa wa Shinyanga uongezeke ni lazima tutoke tukatoe elimu kwa wananchi wafanye kazi kwa bidii waone wajibu wa kuwatunza watoto wao, tuthamini muda tukawasisitize kila mtu akaone kuongeza thamani ya muda wake,tuna haja ya kwenda kuwafundisha watu waache kucheza kamali,waache kuchezea muda,”amesema Macha.
“Pia leo mimi nimeleta salamu za Rais tu yale aliyoongea siku ya uapisho kwamba angependa kuona wananchi wanaendelea kuishi kwa furaha waendelee kufurahia kuishi katika nchi yao, pale ambapo furaha haipo tuwarejeshee, pale patakapokuwa na kero hasa za migogoro ya ardhi zitatuliwe kwa wakati wananchi watendewe haki mkatatue migogoro ya aina yote kila mwananchi asikilizwe na kuthaminiwa”amesema Macha.
Macha amewaomba viongozi washirikiane kwa pamoja katika kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo ili kusisitiza ataanza kwa kukutana na watendaji kuanzia kijiji , madiwani viongozi wa vyama vya upinzani viongozi wa dini, Taasisi mbalimbali ili kuhakikisha anaweka sawa katika kuuendeleza mkoa wa Shinyanga uwe na maendeleo zaidi”amesema Macha.
Kwa upande wake aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme ambaye kwa sasa ni Naibu katibu mkuu ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira amesema amewashukuru wanashinyanga kwa ushirikiano wao pamoja na taasisi zote.
“Namshukuru Mungu ambaye ameruhusu haya yatokee,nimetumikia mkoa wa Shinyanga takriban mwaka mmoja na wiki mbili mmenipa ushirikiano mkubwa,mimi naondoka Shinyanga naomba mmpe ushirikiano mkuu wa mkoa ninayemuachia kijiti hiki, ili aweze kuendeleza pale nilipoishia, pia namshukuru Rais wangu kwa kuniweka hapa nilipo sasa “amesema Mndeme.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo amesema wataendelea kumpa ushirikiano na umoja mkuu wa Mkoa na kuhakikisha amani na upendo unadumu katika mkoa wa Shinyanga.