Naandika makala hii nikitambua kwamba wapo watakaoniunga mkono, na wapo mahafidhina watakaonishambulia.

Si siri tena kwamba Taifa letu linakabiliwa na tatizo kubwa la udini. Ukabila upo, lakini sidhani kama ni tishio kubwa kwa mustakabali wa Taifa letu kama lilivyo tatizo la udini.

 

Nirejee kusema kwamba nimelelewa katika mazingira ya Kikristo. Pamoja na ukweli huo, tumejikuta katika familia yetu tuna Muislamu. Huyu ni mdogo wangu. Kwetu kuwa na tofauti ya dini si jambo la kutufarakanisha. Tunaishi kwa raha mustarehe tukiheshimiana kama ndugu wa damu moja.


Tena nikiri kwa mara nyingine kuwa ninao marafiki zangu wengi ambao ni Waislamu. Wamenisaidia na wanaendelea kunisaidia mambo mengi. Isitoshe, ni rafiki yangu Muislamu aliyenisaidia ada iliyoniwezesha kupata elimu yangu ya awali ya taaluma hii ninayoitumikia leo.

 

Si hivyo tu, hata aliyeniuzia shamba, hata nami leo nikaweza kuwa na mahali pa kuishi jijini Dar es Salaam, ni Muislamu. Nimejaribu kuyasema haya katika kuonyesha kuwa tofauti zetu za kiimani kimsingi hazina fursa ya kutufarakanisha Watanzania.

 

Tumefanikiwa kuwa na Taifa la aina hii ninayoisema kutokana na uongozi shupavu uliokuwapo. Udini, ukabila na aina zote za ubaguzi havikupewa fursa ya kupenya ndani ya umoja wa Watanzania.


Lakini tunu hii ambayo imekuwa ikitufanya tutembee vifua mbele, inatoweka. Tatizo la udini katika nchi yetu linakua kwa kasi. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kulikemea hili.


Mara kadhaa nimesikiliza mijadala mbalimbali katika vyombo vya habari na hata mitaani. Kinachojionyesha wazi ni kwamba wakorofi ni Waislamu.

 

Wanaosema hivyo wanajiegemeza kwenye uchomaji makanisa, uuzaji kaseti na CD zenye kuukashifu ukristo, na kadhalika. Madai haya yanaweza kuwa na ukweli ndani yake, lakini hatupaswi kuamini kuwa wakorofi ni waislamu pekee.

 

Katika siku za karibuni kumeibuka wahubiri wa kikristo kwenye vituo vya daladala. Wanatundika vipaza sauti vikali kweli kweli. Wanaendesha mahubiri asubuhi na jioni. Kisichokera kwenye mahubiri haya ni ule ujumbe wa kumtangaza Mungu; lakini kwenye uhalisia wa mambo, mahubiri haya ni kero kwa watu wenye imani tofauti.


Kuna jambo jingine nimeliona ambalo kwa hakika linaweza kuwa kichocheo cha udini. Mmiliki wa Kituo cha Mafuta cha Victoria jijini Dar es Salaam, pamoja na kupamba kituo chake kwa maneno halali ya kumsifu Yesu na Mungu, amekwenda mbali zaidi kwa kuhakikisha wafanyakazi katika vituo hivyo wanavaa sare zenye kumsifu Yesu.

 

Kwa imani ya mmiliki wa kituo hicho, jambo hilo si baya. Kasoro ninayoiona hapa ni kwamba mmiliki wa Victoria ambaye ana kituo kingine Barabara ya Nyerere, wateja wake si Wakristo pekee. Wateja wake ni wa imani tofauti-tofauti.


Tatizo linakuja kwenye sare za wafanyakazi katika vituo hivyo. Kwa tafsiri ya wazi ni kwamba kama wewe si Mkristo, huwezi kupata ajira hapo. La, kama wewe ni Muislamu, unaweza kupata ajira, lakini kwa “kuikana” imani yao. Kwa hiyo unaweza kuwakuta Waislamu wengi wamelazimika kuvaa nguo zenye maandishi yasiyo ya imani yao kwa sababu tu ya kusukumwa na umaskini.


Waislamu nao wanaweza kuamua kuajiri wafanyakazi kwenye vituo vya mafuta kwa kigezo cha kumtangaza Mtume S.A.W kama kiongozi pekee anayepaswa kuaminiwa. Kufanya hivyo kutawakwaza wakristo ambao pengine hawamtambui.


Wakati huu tunapoelekea kupata Katiba mpya, ni vema mambo ya aina hii yakadhibitiwa. Ni ya kibaguzi. Ajira zisitolewe kwa misingi ya kiimani, hasa kwenye shughuli au maeneo ya huduma yanayoigusa jamii yenye imani tofauti-tofauti. Masuala ya kidini yaachwe kwenye dini, na masuala ya kijamii yapewe sura isiyoukwaza upande wowote wa kiimani. Tanzania iwe kwa Watanzania wote.