· Global Medicare yasema ni matunda uwekezaji wa Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, JamhuriaMedia, Dar ea Salaam

WATU 12 wamefanyiwa upasuaji rekebishi wa macho kwenye kambi ya macho iliyoendeshwa na Hospitali Muhimbili Mloganzila kwa kushirikiana na taasisi ya utalii tiba ya Global Medicare.

Kambi hiyo ilifanywa na madaktari bingwa wa macho, Nabila Elias, Safwat El Badri kutoka Sudan kwa kushiriiana na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Kanda ya Mbeya, Tumbi Kibaha, Benjamin Mkapa ya Dodoma , Ligula Mtwara na St. Benedict ya Lindi.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili tawi la Mloganzila, Dk Eric Muhumba, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuhitimishwa kwa kambi hiyo.

Amesema waliamua kuwashirikisha madaktari bingwa wa ndani ili kupata ujuzi huo ambao haupatikani hapa nchini kwani wagonjwa wamekuwa wakisafiri kwenda kupata huduma hiyo nje ya nchi.

Madaktari bingwa wa macho, Nabila Elias, Safwat El Badri kutoka Sudan kwa kushiriiana na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Kanda ya Mbeya, Tumbi Kibaha, Benjamin Mkapa ya Dodoma , Ligula Mtwara na St. Benedict ya Lindi wakifanya upasuaji rekebishi wa macho kwenye hospitali ya Mloganzila wakati wa kambi maalum ya siku tano.

Amesema kambi hiyo maalumu ya upasuaji rekebishi wa macho ilihusisha watu wenye uvimbe nje ya jicho, makengeza kwa watu wazima, majeraha yatokanayo na ajali au makovu ya muda mrefu ya macho na wagonjwa wengine wanaotoka machozi kwa muda mrefu kutokana na kuziba kwa njia za machozi.

Amesema upasuaji huo umefanyika kwa kiwango kikubwa bila changamoto zozote na wagonjwa wanaendelea na maisha yao kama kawaida.

Amesema watu 50 walifika kwenye kambi hiyo kwaajili ya kupata huduma hiyo lakini waliofanikiwa kufanyiwa upasuaji rekebishi ni wagonjwa 12 pekee.

Daktari bingwa wa macho kutoka hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya, Stephane Nyamsanya, ameishukuru Hospitali ya Mloganzila kwa kuwaalika kuja kushiriki upasuaji huo wa aina yake.

“Kuna mambo tumeshuhudia tulikuwa tunayafahamu lakini mengine mengi hatukuwa tunayafahamu kwa hiyo tumepata ujuzi na tumejengewa ujuzi ili tuweze kuwatibu wagonjwa wa aina hii hapa nchini na wasilazimike tenda kwenda nje ya nchi,” amesema.

Naye Catherine Makunja, ambaye ni daktari bingwa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, amesema hospitali hiyo imekuwa ikitoa matibabu ya ubingwa bobezi kwa matibabu ambayo hayapatikani hapa nchini.

Amesema hali hiyo imesaidia kuwapunguzia wananchi adha ya kwenda nje ya nchi kutafuta huduma hizo na kwamba miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na huduma ya kupunguza uzito kwa puto maalum, upasuaji wa kupunguza uzito na upandikizaji wa figo kwa kuvuna figo kwa kutumia matundu madogo.

Ameaema hospitali hiyo pia imekuwa ikitoa uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia tundu dogo.

Msemaji wa Global Medicare, Albert Kilalah, amesema kambi hiyo inakuja kufuatia uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vilivyonunuliwa na serikali ya awamu ya sita samabamba na madaktari kusomeshwa kwa wingi na kupewa utaalamu wa hali ya juu kufanya matibabu ya kibingwa.

Amesema zamani matibabu kama hayo yalikuwa yakifanyika nje ya nchi lakini kutokana na uwekezaji huo matibabu hayo yanafanyika hapahapa nchini.

“Zamani wagonjwa kama hawa tuliwapeleka nje ya nchi, lakini sasa madaktati bingwa kutoka nje wanakuja kuwatibu wagonjwa wetu hapahapa kwasababu nchi ina kila aina ya vifaa tiba ambavyo tulikuwa tunalazimika kuvifuata nje ya nchi na kwa sasa nchi ina madaktati bingwa wenye uwezo mkubwa wa kutumia vifaa hivyo,” amesema.

Mwisho