Na Mwandishi Wetu, Jeshi la Polisi -Arusha.
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha limekutana na viongozi wa madereva wa Daladala Mkoani humo kwa ajili ya kusikiliza changamoto zinazowakabili Kwa ajili ya kuzitatua.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani humo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema lengo la kikao hicho ni kusikiliza kero zinazowakabili madereva wa daradara mkoani humo ambapo amewapa elimu juu ya masuala ya usalama barabarani.
Aidha, SSP Zauda amebainisha kuwa kikosi cha Usalama Barabarani kinaendelea na operesheni ya kuwakamata na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamekaidi zoezi la kuondoa namba za 3D.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Madereva daladala Jijini Arusha , Albano Matemwe amesema sekta hiyo ya usafiri ilikua ikikabiliwa na changamoto nyangi, hivyo wakaona ni vyema kuomba kukutana na uongozi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuziwasilisha ili zipatiwe ufumbuzi.
Naye Godfrey Mlacha ambaye ni dereva daladala pamoja na mambo mengine, amesema kero kubwa wanayokutana nayo ni abiria kulazimisha kushushwa maeneo ambayo hayana vituo ambapo Hali hiyo hupelekea kuibuka kwa migogoro baina yao na abiria.
Sajenti Athilio Choga wa dawati la elimu kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Arusha amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabani na kutoa taarifa kwa wale watakao kikuka sheria hizo.