Serikali isipuuze, udini upo, iudhibiti (7)

Mihadhara hiyo ya Kiislamu inasema kwamba Yesu alikuwa akivaa kanzu. Pili, Wakristo wenyewe katika michoro yao, filamu zao mavazi ya viongozi wao ni uthibitisho wa kutosha wa mavazi hayo.

Tatu, maandiko ndani ya Biblia yanazungumzia utakatifu na uvaaji wa kanzu. Soma Walawi 16:4, 8:13 na Luka 3: 11. Je, hiyo ni kashfa?


Mihadhara inazungumza wazi Yesu si Mungu. Mwenyezi Mungu (Allah) hana mtoto. Mwislamu haamini kwamba Yesu ni Mungu na mwana wa Mungu, ila anakubali kuwa ni mtume wa Mungu. Kashfa iko wapi? Kwani lazima aamini watakavyo wao?


Ni dhahir shahir mihadhara ya Kikristo inazungumza kuwa Yesu ni Mungu na Mwana wa Mungu,  Muhamad si mtume. Ndiyo imani yao inavyosema sasa kashfa iko wapi? Je, hiyo si kashfa?


Wale wanaojiita manabii na mitume wachungaji, n.k, katika mihadhara wanapokejeli Uislamu, tena kwa runinga au kumwambia mteja wao dini gani wewe waambie unangoja nini katika Uislamu hawatapata kitu. Hiyo si kashfa wala kejeli, si chuki, si uchochezi?

 

Leo nakamilisha maada yangu kuhusu udini na kutoa maswali kwa pande zote tatu, Uislamu Ukristo na Serikali kutokana na mifano michache yenye vinasibishi vya chuki na uchochezi wa kutaka amani na utulivu vitoweke nchini.

 

Inapobainika serikalini kuna idara moja muhimu ina watendaji wote kutoka dini moja hawana uadilifu na wanapendelea dini yao. Hiyo maana yake nini, huo siyo udini?

 

Kwa mujbu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,  Serikali haina dini ila raia wake wanaabudu katika dini mbalimbali.

 

Unaposhabikia uwiano wa wanawake na wanaume kupeana nyadhifa mbalimbali nchini lakini hutaki kuisikia uwiano wa kupeana nyadhifa mbalimbali kati ya Waislamu na Wakristo, huo siyo udini?

 

Unapowakataza watu kuishi kwa mujibu wa maagizo ya dini yao na kesi zao ziendeshwe kwa mujibu wa Quran na Sunna kama inavyotakiwa na dini yao huo siyo udini?


Vipi viongozi na waumini wa Kikristo wapinge wasichana na wanawake katika shule na vyuo kuvaa hijabu kwa mujibu wa dini yao,  huo siyo udini?


Namaliza kwa kusema kuwa ndugu msomaji ambaye umekuwa ukifutilia mada ya udini tangu mwanzo hadi leo, nina kila sababu ya kukushukuru na kukupa kongole kutokana na mawazo na hasa maswali yaliyonipa changamoto.


Nakiri kuwa waliojitokeza miongoni mwenu wamo Wakristu na Waislamu kwa kutetea dini zao, wote wamekiri kuwa udini upo na kutaka Serikali iukomeshe, iache upendeleo wa dini yeyote na ijenge utamaduni wa kujibu malamiko husika kunusuru idhilali isitokee.


Binafsi nina imani na matumanini makubwa kuwa Serikali imesikia, viongozi wa madhehebu ya dini wamesikia na kuelew. Suala la kuzingatia ni kuacha udini kwani udini ni adui wa haki kama ilivyo rushwa na ufisadi. Mungu ibariki Tanzania.