Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Serikali imedhamiria kutumia kiasi cha Tshs.Bilioni 79 kujenga Vituo vya Polisi Kata 698 katika maeneo mbalimbali nchini lengo ikiwa kutataua changamoto za kiusalama kwa jamii ambapo kila kituo kinatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 115.
Hayo yamebainika leo jijini Dar es Salaam wakati wa uwasilishwaji wa utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Vituo vya Polisi Kata ambapo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) na Jeshi la Polisi.
Ripoti hiyo ya utekelezaji imewasilishwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni huku ikihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Adolph Ndunguru,Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Dkt.Maduhu Kazi,Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI,Sospeter Mtwale na wataalamu kutoka pande zote zinazohusika na mradi huo.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amesema adhma ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kumaliza tatizo la uhalifu kwa kulipeleka Jeshi la Polisi chini kwa wananchi na ndio maana amepandisha vyeo kwa ngazi ya nyota moja kwa askari katika maeneo mbalimbali nchini ili wakaongoze Vituo vya Polisi Kata na kushirikiana na wananchi katika dhana nzima ya kudhibiti uhalifu.
‘Rais Samia ametoa ajira na kupandisha vyeo askari akitaka jeshi lishuke chini kwa wananchi ili kuweza kupambana na uhalifu kuanzia ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya Shehia kwa Zanzibar na ndio maana tunataka kuona mradi huu unaanza ili tuweze kufikia lengo husika,jamii ikon a wahalifu na inawajua ndio maana tunataka tusogee chini ili tuweze kusaidiana na jamii yae neo husika kudhibiti uhalifu.’ amesema Waziri Masauni.
Mradi huo utatekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Bajeti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI,wadau na mapato ya ndani ya Halmashauri husika kuanzia mwaka wa fedha 2024/25 mpaka 2026/2027 huku utaratibu wa force akaunti ambapo wataalamu wa Jeshi la Polisi,Halmashauri,taasisi zingine za serikali,wananchi na wadau mbalimbali watatumika kutekeleza mradi.