Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Songea
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana ya Rushwa (TAKUKURU), mkoani Ruvuma imebaini mapungufu na kuchukua hatua katika miradi minne ya maendeleo yenye thamani ya bilioni 1.55.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha miezi mitatu kwa wanahabari kwenye ukumbi wa Taasisi hiyo uliopo Mahenge mjini Songea.
Mwenda ameitaja miradi iliyobainika kuwa na mapungufu kuwa ni ujenzi wa madarasa katika shule za msingi Kipapa,Kipika na Mpepai katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambapo kila shule mradi uligharimu Zaidi ya shilingi milioni 331.
Amesema katika miradi ya shule hizo tatu kulikuwa na changamoto ya mabati kutokuwa na ubora ambapo TAKUKURU iliishauri Kamati za Ujenzi kuyaondoa mabati hayo na kubadilishwa na tayari Kamati zilitekeleza kwa kuweka mabati yenye ubora.
Mwenda ameutaja mradi mwingine uliobainika kuwa na mapungufu ni ujenzi wa sekondari mpya Kijiji cha Lugagara Kata ya Kilagano Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambapo serikali ilitoa Zaidi ya shilingi milioni 560 kutekeleza mradi huo.
“Hata hivyo kwenye mradi huu kulikuwa na changamoto ya baadhi ya mafundi walioingia mkataba na mwajiri kutokuwepo eneo la mradi hivyo kusababisha mradi kuwa nyuma ya muda’’,alisema Mwenda.
Amesisitiza kuwa TAKUKURU ilimshauri Mhandisi kuwafuatilia mafundi hao na kuhakikisha wanakuwepo eneo la mradi ili uweze kukamilika kwa wakati.
Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma amesema katika kipindi hicho waliweza kufuatilia miradi 23 ya maendeleo yenye thamani ya Zaidi ya shilingi bilioni 4.66 ambapo ufuatiliaji huo umefanyika katika miradi ya ujenzi wa madarasa katika shule mpya saba za sekondari na ujenzi wa nyumba mbili za walimu.
Ameongeza kuwa TAKUKURU katika kipindi hicho imefanya kazi moja ya uchambuzi wa mfumo uliohusu mfumo wa utoaji huduma za sekta ya ardhi katika Wilaya ya Songea,Tunduru na Namtumbo lengo likiwa ni kuangalia uzingatiaji wa sheria,kanuni na miongozo.
Amesema katika uchambuzi huo mambo mbalimbali yalibainika na kuchukuliwa hatua ambapo ameyataja mapungufu hayo kuwa ni ukosefu wa upatikanaji wa usafiri wa uhakika,uhaba wa wafanyakazi na maafisa Ardhi na watoa huduma kutotambua vema mkataba wa kisheria wa utoaji huduma.
Mwenda amesema katika kipindi hicho cha miezi mitatu TAKUKURU wameweza kupokea jumla ya malalamiko 55 ambayo yameshughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa kuanzisha uchunguzi ambao upo katika hatua mbalimbali.
Ameyataja matarajio ya kipindi cha miezi mitatu ijayo kuwa ni kuendelea kuelimisha wananchi juu ya rushwa na madhara yake,lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata uelewa kuhusu rushwa .
Ametoa wito kwa wananchi mkoani Ruvuma kuendelea kuunga mkono jitihada za kufichua vitendo vya rushwa na walarushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika