Na Abel Paul,Jeshi la Polisi- Tinde Shinyanga
Jeshi la Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo STPU, kimesema kinawashikilia watuhumiwa kadhaa kwa tuhuma za wizi wa mifugo na utoroshaji mifugo nje ya nchi huku likisema kuwa litaendelea kushirikiana na wananchi kwa karibu ili kudhibiti uhalifu huo hapa nchini.
Akitoa taarifa hiyo leo Machi 12,2024 na Kamanda wa Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua wakati alipotembelea mnada wa Tinde uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga amesema jeshi hilo linawashirikilia watuhumiwa wa wizi wa mifugo katika maeneo tofauti tofauti hapa nchini.
Kamanda Pasua ameongeza kuwa watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za wizi wa mifugo katika maeneo tofauti hapa nchini majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi ambapo amesema kikosi hicho kitaendelea kuwakamata wale wote watakao bainika katika kujihusisha na wizi wa mifugo.
Aidha amewaomba wananchi kote nchini kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi za baadhi ya watu wanaojihusisha na wizi wa mifugo Pamoja na kutorosha mifugo nje ya nchi.
Kwa upande wake afisa biashara Kutoka Shinyanga vijijini Upendo Milisho amebainisha kuwa wananchi na wafanya biashara mifugo katika mnada wa Tinde uliopo halmashauri ya Shinyanga wamekuwa na mwitikio Chanya katika ulipaji Ushuru kwa kielektroniki mnadani hapo.
Afisa Mapato Wilaya ya Shinyanga Bw. Victor Moleli pamoja na kushukuru kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo amebainsha kuwa Jeshi la Polisi pamoja na wananchi wameendelea kudhibiti uhalifu katika eneo hilo la mnada wa Tinde kitendo kilichopelekea mnada huo kuwa miongoni mwa minada yenye kukusanya mapato vizuri na usalama wa kutosha.