na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kesho inatarajia kutoa uamuzi wa kukubali ama kuyakataa maombi ya Freeman Mbowe ya kutaka waandishi wa habari wanaomdai mtoto wake Sh milioni 62.7 wamlipe gharama.
Maamuzi hayo yametolewa leo Machi 12, 2024 na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio katika kesi iliyofunguliwa na Mbowe dhidi ya waandishi wa habari 10 wanaomdai mtoto wake, Dudley Mbowe ambaye ni Mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima.
Kupitia wakili wake John Mallya Mbowe aliwasilisha maombi mahakamani akitaka nyumba iliyokamatwa na dalali kwa amri ya mahakama iondolewe na wajibu maombi wamlipe gharama za kesi.
Waandishi wa habari 10 wanamdai Mkurugenzi wa Tanzania Daima, Dudley Mbowe Sh milioni 62.7 wameachia nyumba ya Freeman Mbowe waliyoikamata ili kuipiga mnada lakini wamegoma kulipa gharama za kesi kwa sababu hata wao wanaingia gharama katika kudai haki yao.
Kulwa Mzee kwa niaba ya wajibu maombi alidai walipitia nyaraka zote na viambatanisho wamejiridhisha na wamekubaliana kwa pamoja kwamba hiyo nyumba waliyoikamata ni ya familia lakini inamilikiwa na Freeman Mbowe.
“Mheshimiwa tumepitia nyaraka pamoja na viambatanisho ikiwemo hati ya nyumba, tumejiridhisha kwamba mkurugenzi tunayemdai Dudley Mbowe si mmiliki, hivyo tunaiomba Mahakama tuiondoe hiyo nyumba kwenye maombi yetu.
“Kuhusu gharama mheshimiwa, kwa uelewa wetu kwa mashauri ya migogoro ya kikazi hakuna gharama na hiyo inatokana na uwezo wa vipato vidogo vya wafanyakazi.
“Wakati sisi tunafanya hili jambo tulikuwa tukiamini kabisa kuwa ni nyumba ya mkurugenzi wetu kwa sababu katika hatua ya makubaliano alikuwa anatuambia kuwa tutafanya vikao nyumbani kwake na tumefanya hapo vikao kwenye hiyo nyumba.”alidai Kulwa.
Akijibu dalali wa Mahakama Jesca Massawe alidai alipokea amri ya Mahakama kwa ajili ya kukamata nyumba hiyo.
“Sisi kama madalali wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yetu, tulikaa na Mahakama hii chini ya Jaji Mfawidhi akatuelekeza kuwa katika mashauri haya ya kukamata mali tusijihusishe na utambuzi wa mali bali tukamate na kama kuna changamoto basi italetwa mahakamani,” alidai na kuongeza kwamba alitekeleza amri ya Mahakama kama ilivyoelekezwa.