Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
SERIKALI mkoani Pwani, imekemea tabia ya uchomaji moto misitu ,unaofanywa kwenye baadhi ya maeneo ,kwani kwa kufanya hivyo ni kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayoshamiri kwa changamoto ya uharibifu mkubwa wa mazingira suala ambalo linahitaji msukumo wa kudhibiti uchomaji moto misitu.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge alitoa kalipio hilo ,katika kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) kilichofanyika ukumbi wa mikutano , kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa.
Kunenge alieleza,Rais Samia Suluhu Hassan ,Makamu wa Rais ambae pia ni mlezi wa mkoa huo hawapendezwi na tabia ya uchomaji moto misitu ovyo pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira katika mkoa huo.
Aliwaasa watendaji na viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya chini mkoani hapo , kufanya kazi ya kutosha kudhibiti hali hiyo.
“Rais wetu mpendwa ameipa Nchi heshima kubwa Kwa utunzaji wa mazingira na masuala ya nishati safi ,hivyo jamii ibadilike ,ukipita njiani unakuta misitu inachomwa Jambo ambalo sio zuri Kwa mkoa wetu”
Kunenge pia alitaka iongezwe nguvu ya ziada katika utalii na uvuvi maana Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa yenye fukwe ndefu na nzuri.
Pamoja na hilo , alieleza katika sekta ya elimu mkoa upo kwa asilimia 83 ya ufaulu, kitaifa ni asilimia 80,mkoa upo juu kwa asilimia 3 ya kiwango cha kitaifa lakini bado ipo changamoto ya kutofikia ufaulu kwa asilimia 17.
“Tufanye kazi ,bado tuna kazi ya kufikia asilimia 17 kwenye ufaulu”alifafanua Kunenge.
Hata hivyo Kunenge alisisitiza, kuboresha vyanzo vya mapato ili kuinua mapato.
Awali Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu mkoa wa Pwani, Edina Katalaiya akisema, wameomba kiasi cha sh.bilioni 364.9 katika utekelezaji wa mpango wa bajeti 2024/2025.
“Rasimu ya mpango wa bajeti 2024/2025 vipaombele 19 ikiwemo nane sekretariet na 11 kutoka halmashauri vitakavyotatua kero za wananchi”
Alieleza, ruzuku matumizi ya kawaida bilioni 207.5 kati yake bilioni 101 Kwa ajili ya mishahara,fedha za maendeleo bilioni 88.8 kati ya kiasi hicho sh. 54.8 Bilion ni fedha za ndani na sh.34 Billion ni fedha za nje zinazotoka kwa Wahisani na wadau wa nje.
Edina alisema, sekretarieti ya Mkoa huo unatarajia kukusanya sh 60.4 Billion kutoka kwenye upangishaji wa ofisi na ukodishaji wa ukumbi.
Alieleza kuwa ,Halmashauri za mkoa huo zimekisia kukusanya sh 68.5 Billion kutoka katika vyanzo vya ndani vya mapato kati ya kiasi hicho sh. 49.7 Billion ni kutoka vyanzo visivyolindwa na sh 18.7 Billion ni kutoka vyanzo vilivyofungiwa.
Mbunge viti maalum Mkoani humo ,Subira Mgalu alisisitiza kuboresha makusanyo kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato .