Ndugu Mhariri,

Sisi ni wanatunduru, tunaandika barua hii tukiwa na majonzi, mfadhaiko na huzuni kubwa kwani tunaona Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imetutupa kabisa. Tumeamua kuandika barua hii kupeleka kilio chetu kwa Mheshimiwa Rais kupitia gazeti lako, Jamhuri.

Mheshimiwa Rais, tunakumbuka Oktoba, 2005 ulikuja Tunduru na kutueleza lengo la ujio wako kwamba ulihitaji kura zetu ili utuletee maendeleo.

 

Mheshimiwa Rais, tulisikiliza na kuelewa sera za chama chako zilizojikita kusisitiza usawa na utu kama nyenzo katika kuleta amani na maendeleo ya nchi. Tulivutiwa sana na mantiki katika hoja zako na kuamini ulikuwa na nguvu ya hoja, hivyo kutushawishi kukuchagua kuwa Rais ulete uliyoahidi.

 

Mheshimiwa Rais, wanatunduru tulikupa kura tukiamini huenda sasa ni muda mwafaka wa wewe kutekeleza uliyoahidi na tukiamini miaka mitano tuliyokupa haikukutosha kuwaangalia Watanzania wote. Mheshimiwa Rais, lazima tukiri kuwa Serikali yako ni imara na aminifu kwani tumekuwa tukishuhudia ikitekeleza mikakati mbalimbali na wakati mwingine kufanya uamuzi mgumu kwa mustakabali mwema wa Taifa letu.

 

Mheshimiwa Rais, Serikali yako ndiyo ilitoa mabilioni ya fedha kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, kuchangia ujenzi wa shule za kata nchini, kuongeza fedha za malazi na chakula kwa wanfunzi wa Elimu ya Juu kutoka Sh 5,000 hadi Sh 7,500 kwa siku na kukubali kulipa ongezeko la ada kwa vyuo vikuu binafsi nchini. Mheshimiwa Rais, tumekuwa tukishuhudia ukifungua miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya miundombinu ya barabara, elimu, afya na kilimo (kwa ujumla tunakiri kuwa Serikali yako imefanya mambo mengi na makubwa ambayo hatuwezi kuyaeleza katika barua hii).

 

Mheshimiwa Rais, pamoja na Serikali yako kutekeleza yale uliyoahidi huku ukiongozwa na Ilani ya chama chako, Chama Cha Mapinduzi(CCM), sisi wanatunduru tunaona utekelezaji huo si chochote kwetu kwani hautunufaishi chochote bali tunabaki kuwa mashahidi tu wa mendeleo unayowapatia watu wengine wa taifa hili. Inaumiza sana Mheshimiwa Rais!


Mheshimiwa Rais, tunathubutu kuyanena haya kwa sababu tunashuhudia maendeleo yanayofikiwa katika maeneo mbalimbali ya taifa hili, lakini sisi tunaendelea kubaki nyuma na hatusongi mbele japo kwa hatua moja. Inahuzunisha sana Mkuu!


Mheshimiwa Rais, tumeshuhudia ukifungua barabara kwa muda mfupi toka ujenzi wake uanze, lakini sisi tunashuhudia wakandarasi wakidai kufanya upembuzi yakinifu miaka nenda rudi. Inafadhaisha sana Mheshimiwa!

 

Mheshimiwa Rais, kwa ujumla tunathubutu kusema kuwa tunakabiliwa na matatizo mengi ambayo hayawezi kuelezwa katika barua hii. Kwa ufupi ni kwamba suala la umeme huku ni msiba kwani mpaka sasa ni Mega Watt moja inayosambaza umeme, tena ni mjini tu. Huko kwenye sekta ya elimu ndiyo hakusemeki maana mpaka sasa zipo maabara tatu kati ya shule 20 zilizopo wilayani hapa. Sekta ya afya nayo ni msiba mwingine kwani wagonjwa wawili hulala katika kitanda kimoja na dawa ni mtihani kwa zahanati zilizopo vijijini kwani wakati mwingine hufika hadi mwezi mmoja bila dawa zahanatini.


Mheshimiwa Rais, tunaamini kuwa huenda kwa sababu ya baadhi ya matatizo haya kuwa na ‘long term impact’ ndiyo maana Serikali ina ‘delay’ katika utekelezaji wake, lakini cha kusikitisha ni pale Serikali yako inapoonekana kutochukuwa ‘serious measures’ katika zao la korosho ambalo ni uti wa mgongo wa uchumi wa wanatunduru.


Mheshimiwa Rais, zao hili ni uti wa mgongo wa uchuimi wetu  kwani linatuwezesha kuwapeleka watoto shule ambapo tunafanya uwekezaji wa ‘human capital’, linalotuwezesha kununua chakula wakati huu wa masika kutokana na uzalishaji wa zao la mahindi usiokidhi haja. Koroso pia zinatuwezesha kununua vyombo vya usafiri, vyombo  vya habari na wakati mwingine kupeleka wagonjwa hospitalini.


Mheshimiwa Rais, kupuuzwa kwa zao hili ni sawa na kutangaza rasmi kuwa Wilaya ya Tunduru inakufa, hivyo kuichimbia kaburi izikwe. Tunalia sana Mheshimiwa, tunahitaji huruma yako Mkuu.


Mheshimiwa Rais, tunashangaa, tunasikitika na kuhuzunika zaidi pale tunaposhuhudia wenzetu wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakiuza korosho zao kwa raha mustarehe “Why not Tunduru?


Mheshimiwa Rais, tulipowauliza wabunge wetu tatizo ni nini? Walitujibu kuwa vyama vya ushirika vinadaiwa na benki ambayo inakataa kuvikopesha na hii ni kwa sababu vyama hivyo vilichelewa kuuza korosho za mwaka 2011 kwa kukosa wanunuzi na hatimaye kusababisha korosho hizo kuuzwa Novemba 2012 kwa bei ya kutupa ya Sh 850 kwa kilo, hivyo kusababisha hasara ya 350 kwa kilo.


Mheshimiwa Rais, tulipoendelea kuwauliza kwanini soko hilo linakosa kwa wanatunduru ilhali vyama vya ushirika vya mikoa ya Mtwara na Lindi viliuza korosho kwa wakati? Walitujibu kuwa ni kutokana na sababu za umbali wa kijiografia kwenda Bandari ya Mtwara.


Mheshimiwa Rais, ‘We are very sad and frustrated’, hatujui tutapelekaje watoto wetu shule ambazo zitaanza kufunguliwa Januari 6, mwaka huu, tutapataje mbolea? Tutakulaje Mheshimiwa? Tutauguzaje? Mheshimiwa tunakereka sana AMIRI JESHI MKUU.


Mheshimiwa Rais, kwa mamlaka uliyopewa na Katiba ya nchi hii tunaamini hakuna utakachoshindwa kukifanya kwa yenye uwezo wa kibinadamu.


Mheshimiwa, ni fedha za kitanzania Sh bilioni tano zitakazowezesha korosho hizo kununuliwa maana uzalishaji wa zao hili wilayani hapa hauzidi tani 5,000 kwa mwaka, ambapo bei yake ni Sh 1,200 kwa kilo.


Tunaomba huruma yako Rais. Janga la njaa litatuua kama korosho hizo hazitanunuliwa. Tunaumia Mheshimiwa, tuonee huruma wananchi wako, uwezo huo unao Mheshimiwa Rais.

Tunawasilisha.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Tunduru.

Wanatunduru,

Mwandishi: Madaya Bakari

Simu: 0789357823