Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani
Kaya zaidi ya 900 za Kijiji cha Lupunga, mkoani Pwani wamo hatarini kukumbwa na njaa baada ya kinachodaiwa mwekezaji kuvamia mashamba na kuharibu mazao kinyume cha sheria.
Akizungumza hivi karibuni kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Lupunga, Abdalah Selemani, amesema mgogoro wao na Kampuni ya Continental ni wa muda mrefu, na amedai mwekezaji huyo amekuwa akikingiwa kifua na uongozi wa mkoa.
Amesema mwekezaji huyo kwa mara ya kwanza alikwenda kwenye kijiji chao kudai ni cha kwake na uongozi haukumwelewa na kuhitaji uthibitisho wa eneo hilo amelipataje.
“Ilipofika hatua hiyo hakuwa na uthibitisho, alikwenda katika uongozi wa mkoa kuomba msaada na hadi kufikia hatua ya kupata jeuri ya kuharibu mazao na mali za wananchi.
“Kiukweli wananchi wanaumizwa na kadhia hii, wamechoka, tunamwomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie kupata haki yetu kwa sababu mkoa umeshindwa kutusaidia,’’ amesema.
Amedai kilio chao walikipeleka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na walipewa ahadi kwamba suala lao litashughulikiwa, lakini baadaye mwekezaji huyo amekwenda kuvamia maeneo ya wananchi na kuharibu mazao mbalimbali.
“Nakumbuka siku ya tukio lilikuja bulldoza kwenye maeneo ya wananchi likaanza kukatakata mazao, nilipopata habari nilikwenda kujionea, nikawakuta wakiendelea kuharibu.
“Nilipohoji wamepata wapi kibali wakasema kwa Katibu Tawala. Kwa hiyo tunaomba waandishi mtusaidie kupeleka kilio chetu kwa rais wetu tunayeamini kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi. Sisi hatumtambui mwekezaji mita 500 za mraba kama uwekezaji mkoa unavyotaka na hatuko tayari,” amesema.
Mkazi wa kijiji hicho, Naftari Chacha (70), amesema ameishi hapo kwa miaka mingi na tayari amewekeza fedha zake za mafao katika kilimo na mifugo.
Amesema kitendo cha mwekezaji huyo kuingia na kudai eneo la kijiji hicho ni lake amekuwa anachanganyikiwa kwa sababu fedha yake ameziweka katika kilimo na hana kazi nyingine zaidi ya kutegemea mali hizo.
“Rais atusaidie kupata ardhi yetu, vinginevyo watu watakufa kutokana na mgogoro huu, lakini kwa sababu tuna imani na Rais Samia, suala hili litapatiwa ufumbuzi wa haraka,” amesema.
Mwathirika mwingine wa mgogoro huo, Beatrice Makundi, ameomba viongozi kuingilia kati ili waendelee kuishi kwa amani bila hofu.
Amesema wanawake wengi katika kijiji hicho ni wakulima na wanapoharibiwa mazao yao watoto wao watateseka kwa njaa.
Akizungumza hivi karibuni kuhusu mgogogoro huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema ulishapatiwa ufumbuzi lakini wananchi hawakuridhika.
“Sisi tunamtambua mwekezaji huyo na tulifanya jitihada za vikao mbalimbali ili kupatikana ufumbuzi.
“Hivyo kama wanaona haki yao imedhulumiwa ni vema wakaenda ngazi za juu ili kupata haki, na sisi tunatekeleza sheria tu, kama wameona hawakutendewa haki wanapaswa kwenda mahakamani,” amesema.
Naye mwakilishi wa Continental, Masoud Saed, amesema kampuni inayomiliki eneo hilo ina hati ya uthibitisho kwamba ipo hapo kwa uhalali.
“Hili eneo linamilikiwa kwa uhalali tangu mwaka 1987 na lina hati halali, hivyo wananchi hao ndio wamevamia kwenye eneo ambalo tayari linamilikiwa kwa njia halali.
“Tuna vithibitisho vyote vya umiliki wa eneo hilo, hivyo nipo tayari kwa mgogoro huu kufikishwa ngazi za juu ili niweze kupata haki yangu ya msingi,” amesema.