Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi (98), amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena jini Dar ea Salaam.
Akitangaza msiba huo jioni ya leo Februari 29, 2024 Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Mzee Mwinyi amefikwa na umauti wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya mapafu.
Rais Samia amesema Mzee Mwinyi alikuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba 2023 London Uingereza na baadaye kurejea nchini na kuendelea na matibabu katioa.Hospitali ya Mzena .
Rais Samia ametangaza siku saba za maombolezo kuanzia kesho Machin1, 2024 kufuatia kifo hicho na pia bendera itapepea nusu mlingoti kwa siku saba.
“Kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia leo 29 Februari saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.
“Mzee Ali Hassan Mwinyi, amekuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba mwaka jana huko London, Uingereza na baadaye kurejea nchini na kuendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena,” amesema Rais Samia.
Mzee Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili aliingia madarakani rasmi tarehe 5 Novemba 1985.
Mei 8, 1925, ndiyo tarehe ambayo Mwinyi alizaliwa. Kijiji cha Kivure, Wilaya ya Mkuranga, Pwani.