Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Moshi
Michuano ya Gofu inayoitwa Lina PG Tour imeanza kurindima katika Viwanja vya TPC Moshi ambapo zaidi ya wachezaji 80 wakiwemo 16 wa kulipwa wamejitokeza kushindana.
Shindano hilo limeandaliwa na familia ya Said Nkya kwa kushirikiana na Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) kwa lengo la kumuenzi mchezaji wa zamani wa timu ya taifa anayeitwa Lina Nkya.
Lina Nkya alikuwa ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Gofu na miongoni mwa wachezaji waliopeperusha vyema bendera ya Tanzania mwaka 2011 walipotwaa taji la Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa usajili wa wachezaji hao Makamu wa Rais wa TLGU, Ayne Magombe alisema ushiriki umekuwa mkubwa kuonesha namna watu walikuwa wakimkubali mchezaji huyo wa zamani hivyo anategemea ushindani utakuwa mkubwa.
“Wachezaji wengi wameshawasili na wako tayari kupambana, tunategemea ushindani utakuwa mkubwa na vipaji vitakuwa vingi, tunawahimiza mashabiki wa mchezo huu kujitokeza kushuhudia mastaa wakichuana,”alisema.
Naye Enock Magire ambaye ni Katibu wa Chama cha Gofu Tanzania alisema chama kiliona umuhimu wa kushirikiana katika shindano hilo hasa kwenye kusaidia kupata washindi wengi zaidi watakaoiwakilisha nchi katika mshindano mbalimbali ya kimataifa.
Kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa wanaoshindana katika mashindano hayo, Brison Nyenza alisema ni jambo jema na zuri kwa Tanzania kuwa na mashindano ya Tour(ziara) kwani yatasaidia kuwaleta pamoja wachezaji na kujipatia kipato kwa wale watakaoibuka washindi.
“Kiasi ambacho kimewekwa kama zawadi ni kikubwa hivyo ni fursa kwangu kama mchezaji wa gofu wa kulipwa kutengeza pesa zaidi na kunipa motisha ya kuendelea kucheza mchezo huu,” amesema
Mashindano hayo yanatarajiwa kumalizika siku ya Jumaapili Machi 3,2024 na baada ya hapo yatafanyika katika mikoa mingine ambayo ni Arusha, Zanzibar na Dar es salaam.