Na Isri Mohamed
Ikiwa ni mwaka moja umepita tangu Rapa mkubwa nchini Afrika Kusini, Kiernan Forbes ‘A.K.A’ apigwe risasi na kufariki dunia, Polisi nchini humo wamethibitisha kuwakamata Watuhumiwa sita wa mauaji yake akiwemo ‘Mastermind’ aliyeandaa mpango mzima na kulipa Wauaji wote walioshiriki tukio hilo lililotokea Februari 10, 2023 huko katika mji wa Durban Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri anayehusika na Idara ya Polisi Bheki Cele, watu hao sita wakiongozwa na ‘Mastermind’, watumia bunduki wawili, watoa taarifa wawili na mmoja aliyehusika kutafuta silaha na magari watafikishwa Mahakamani Alhamisi Februari 29, 2024.
Waziri Cele amesema miongoni mwa waliokamatwa wamewahi kuhusishwa na mauaji ya kutisha ambapo walikimbilia nchi jirani ya Eswatini ( zamani Swaziland) kujificha lakini tayari wamekamatwa na taratibu za kuwarejesha South Africa zimeshaanza kufanyiwa kazi.
Pamoja na kwamba Polisi wamesema hawatozungumzia nia ya mauaji hayo, imefahamika kwamba wauaji walianza kumfuatilia AKA kuanzia anawasili uwanja wa Ndege wa Durban hadi kwenye Mgahawa alikouawa.