Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima amewashauri wahariri wa vyombo vya habari nchini kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Mpango wa Malezi, Makuzi, Maendeleo ya Awali ya Mtoto ( MMMAM ) kupitia vyombo vya habari.
Waziri Gwajima amesema hayo leo Februri 26,2024 wakati walipozugumza na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari katika ofisi ndogo za Wizara hiyo jijini Dar es Salaam, kuelekea katika mkutano wa kimataifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto utakohusisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, March 11-14, 2024 jijini Dar es Salaam huku Mgeni Rasmi akitaraijiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri Gwajima amesema Tanzania imepata neema hiyo ya kuandaa mkutano huo kutokana na jitihada na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa programu ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) iliyozinduliwa Desemba 2021.
Aidha Waziri Gwajima amesema kutokana na mkutano huo Tanzania inatarajiwa kunufaika kwa kuingiza fedha za kigeni na wajasiriamali kujiingizia kipato kutokana na huduma watakazozitoa kwa wageni watakaoshiriki.
Hata hivyo Waziri Gwajima amesema mkutano huo utaambatana na mambo mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa Kampeni ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto, na kuangalia maeneo ya kuwekeza.
Akisisitiza juu ya umuhimu wa Mkutano huu Gwajima amesema Kisayansi ni muhimu kwa mtoto kupata huduma zote pasipo kupungua hata moja wakati akiwa na miaka 0-8.
“Kisayansi Ubongo hukua kwa asilimia 90 kwa mtoto akiwa na umri kati ya miaka 0-8 na ndiyo wakati wa kumuweka mtoto kuja kuwa wa aina gani……… ni muhimu saana kuimarisha huduma zote kwa mtoto kwa usawa bila kuacha hata huduma moja”. Gwajima amesema.
Kwa upande Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) amesema mkutano huu ni fursa ya kipekee kwa Watanzania kujifunza na kutangaza utalii wa nchi kutokana na uhudhuliaji wa watu kutoka mataifa mbalimbali.
Mkutano huo umebeba kauli mbiu ya ‘Wekeza katika Makuzi, Malezi ya Watoto Kujenga Raslimali watu kwa Taifa’ na unatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 1000 huku washiriki kutoka nje ya nchi wakiwa 700, na 400 kutoka Tanzania.