Wakati mfanyabiashara maarufu Harbinder Singh Sethi akiendelea kusota rumande kutokana na kesi inayomkabiri kuhusu sakata la akaunti ya Escrow, yenye mashtaka 12, vyombo vya habari nchini Kenya vimeandika kashfa kadhaa zilizowahi kufanywa na mfanyabiashara huyo.
Mtandao wa Standard Digital wa nchini Kenya, umechapisha katika tovuti yake tuhuma zilizowahi kufanywa na Sethi miaka zaidi ya 20 iliyopita.
Kashfa hizo zimechapichwa katika tovuti ya www.standardmedia.co.ke taarifa hiyo ikiwa na kichwa cha habari kinachoeleza jinsi tajiri mwenye historia tata nchini Kenya alivyoingia kwenye kashfa kubwa Tanzania.
Taarifa hiyo inaanza kwa kusema, ni watu wachache waliopata mamilioni ya Dola za Marekani, kupitia zabuni za mikataba ya ujenzi katika serikali ya Kenya katika miaka ya 1990, mmoja wapo ni mfanyabiashara tajiri Harbinder Singh Sethi.
Akiwa amezaliwa na kukulia Iringa, mji mdogo uliopo nyanda za juu Kusini mwa Tanzania, Sethi aliingia Nairobi (Kenya) miaka 1980.Wakati huo utaratibu wa kutoa zabuni katika miradi ya serikali ukiwa bado mpya nchini humo.
Mtandao huo unaripoti kwamba, mfanyabiashara huyo alianzisha kampuni yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 19, alijua anaweza kutengeneza utajiri mkubwa kupitia mikataba ya ujenzi yenye thamani ya mabilioni ya shilingi kutoka taasisi za nchini Kenya.
Sethi alitumia ipasavyo vuguvugu la ujenzi wa Kenya mpya kupitia kauli mbiu ya serikali ya nchi hiyo ya Harambee, ambapo mara kwa mara alikuwa akijitokeza kwenye shughuli za kijamii na kutoa michango na msaada mbalimbali.
Michango yake ilivutia vyombo vya habari na kujiweka karibu na maafisa wa serikali. Hata hivyo, mambo yalianza kwemwendea kombo baada ya kampuni yake ya ujenzi iitwayo, Ruaha Concrete Co Ltd, aliyoianzisha na ndugu zake kukumbwa na kashfa kubwa nchini Kenya hali iliyosababisha biashara zake kufuatiliwa kwa karibu.
Mwaka 1997 ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Kenya, ilifichua kampuni yake ya Ruaha Concrete Co Ltd, ilipata mkataba wa kujenga barabara yenye urefu wa kilimita tisa, kutoka Shirika la Mafuta la Kenya (KPC) kinyume cha taratibu.
Pamoja na kasoro hiyo, ujenzi wa barabara hiyo ulichelewa kumalizika na kusababisha kuongezeka kwa gharama za ujenzi na huku ikiwa imejengwa chini ya kiwango.
Gharama za ujenzi ziliongezeka mara mbili na nusu kutoka Sh za Kenya Milioni 197, Februari 1995 hadi zaidi ya Sh milioni 510 Juni 1998, wakati ujenzi wa barabara hiyo ulipokamilika. Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alipendekeza kampuni ya Ruaha ichunguzwe.
UKWEPAJI KODI
Kampuni yake nyingine ya Pan Africa Builders and Constructors (PABCO) iliingia mkataba mkubwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii nchini Kenya (NSSF).
Mkataba huo ulikuwa na thamani ya karibu Sh bilioni 2 za Kenya, kwa kujenga nyumba na vituo vya biashara katika maeneo ya Kitsuru jijini Nairobi (Kenya). Hata hivyo, mradi huo nao ulichelewa kukamilika na kupelekea gharama za mradi huo kushushwa ahadi Sh. Milioni 822.
Wakati wa kukabidhi mradi huo kwa NSSF Februari 2007, yalitolewa madai kwamba mfuko huo haukulipa kiasi cha fedha kilichobaki cha Sh bilioni 1.3.
Sethi alikwenda Mahakama Kuu ya nchini humo, kutaka alipwe fedha hizo, ambapo hukumu ya mahakama iliangukia upande wake na mfuko wa NSSF kutakiwa kumlipa Sh. Milioni 668 (Dola milioni 7.4) kujumlisha gharama na riba zilizoongezeka. Lakini kampuni yake ilikubali kupokea Sh.milioni 590 kama malipo ya awali.
Baadaye ilibainika kwamba kampuni hiyo ilikwepa kulipa kodi ya Sh.milioni 260 katika Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA). Hali hiyo ilisababsha Kamati ya Bunge ya Vitega Uchumi (PIC) kupendekeza Sethi asipewe mkataba wowote wa ujenzi mahali popote nchini humo.
Ni mambo machache yaliyokuwa yakijulikana kuhusiana na Sethi hadi hivi karibuni wakati alipokamatwa pamoja na mfanyabiashara mwingine maarufu Tanzania na kufikishwa mahakamani wakihusishwa na kashfa ya akaunti ya Escrow.
Sethi ndiye muhimili mkuu katika kashfa hiyo iliyodumu kwa miaka 20 sasa ijulikanayo Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo imeishi katika awamu tatu za uongozi nchini Tanzania hadi pale hatua zilipochukuliwa na utawala wa sasa wa Rais John Magufuli.
Ni kashfa ambayo ilimtikisa Mwanasheia Mkuu wa Serikali na maofisa kadhaa wa serikali wa ngazi za juu, huku Bunge likipendekeza Waziri Mkuu, wakati huo Mizengo Pinda, awajibike kisiasa kutokana na kashfa hiyo.
Bunge liliazimia kufukuzwa kazi mawaziri wawili akiwemo Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), Prof. Anna Tibaijuka, ambaye hata hivyo amekuwa akijitetea kwamba Sh.milioni 100 (Dola za Marekani milioni 1) alizopokea kutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Tanzania Limited zilikuwa ni mchango tu.
Kwa upande wa Sethi, kampuni yake nyingine ya Pan African Power Solution Tanzania LTD (PAP) ilikuwa sehemu ya ‘dili’ hiyo ambayo ndiyo iliyosababisha akamatwe.
Sethi pamoja na mfanyabiashara mwenzake, James Rugemalira wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Tanzania Limited (VIPEM) wamefunguliwa mashtaka sita katika kesi ya uhujumu uchumi. Moja ya mashtaka hayo ni kuikosesha serikali ya Tanzania zaidi ya Sh bilioni 306.
Kukamatwa kwa Sethi kuna hitimisha mivutano na mijadala ya muda mrefu ambayo ilitawala katika vyombo vya habari nchini.
Sakata hili lilianza mwaka 1994 wakati kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa ubia na kampuni ya Merchmar Corporation ya Malaysia na kampuni ya hapa nchini ya VIP Engineering, kusaini hati ya makubaliano (MoU) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linalomilikiwa na serikali kwa ajili ya kuingiza umeme kwenye gridi ya taifa.
Gharama za mradi
Makubaliano ya kuanzishwa mradi huo, yalisainiwa kutokana na kuwapo kwa uhaba mkubwa wa nishati ya umeme nchini, hali iliyosababishwa na ukame kwa muda mrefu. Ili kutafuta suluhisho la tatitozi hilo kwa njia ya dharura, Tanesco iliamua baada kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme wa dizeli kwa misaada ya nje.
Hapa ndipo ulipojitokeza muungano wa kampuni hizo, Mechmar Corporation ukimiliki hisa asilimia 70 ya hisa na VIP Engineering asilimia 30 na kwa pamoja kuunda kampuni ya IPTL kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
IPTL iliendelea na majadiliano ya Tanesco hadi June 1995, makubaliano ya kampini hiyo kununua umeme kwa miaka 20 yalisainiwa kwa IPTL kutakiwa kuzalisha umeme wa megawati 100 MW kwa kutumia mitambo ya dizeli iliyosimikwa Tegeta, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kwa gharama ya Sh. Bilioni 16.8 (dola za Marekani milioni 163.5).
Makubaliano hayo pia yalihusu gharaza za manunuzi na ujenzi wa mradi kwa thamani ya Sh. Bilioni 13 (dola za Marekani milioni 126.39).
IPTL iliendelea na majadiliano ya Tanesco na June, 1995, makubaliano ya kampuni hiyo kununua umeme kwa miaka 20 yalisainiwa kwa IPTL kutakiwa kuzalisha umeme wa Megawati 100 kwa kutumia mitambo ya dizeli iliyosimikwa Tegeta, kwa gharama ya Sh bilioni 16.8 (Dola za Marekani milioni 163.5, kwa mujibu wa viwango vya kubadili fedha kwa kipindi hicho).
Makubaliano hayo yalihusu gharama za ununuzi na ujenzi wa mradi kwa thamani ya Sh bilioni 13 (Dola za Marekani milioni 126.39).
Bila kuitaarifu Tanesco, IPTL iliingia makubaliano na kampuni nyingine ya Wartsila kwa ajili ya kujenga mtambo wa kati wa kuzalisha umeme kwa kutumia dizeli (MSD). Dili la Wartsila liliongeza gharama kwa asilimia 33 kutoka Dola za Marekani milioni 85.7 hadi dola milioni 114.2.