Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau amesema Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) imekuwa ikiwaibia mapato halmashauri ya Mafia, yatokanayo na ada ya tozo la kiingilio kwenye maeneo iliyoyachukua kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.
Dau amesema taasisi hiyo imekuwa ikikusanya mapato ya ada ya kiingilio yanayofikia zaidi ya Sh Bilioni 2 kwa mwaka lakini uongozi wa taasisi hiyo umekuwa ukitoa taarifa zenye utata kuwa wanakusanya Sh milioni 700 tu.
Amesema kati ya Sh milioni 700 wanazodai kukusanya wanachukua Sh milioni 500 ambazo wanaeleza kuwa ni gharama za uendeshaji, ikiwemo vikao na mikutano yao na kulipana posho tu.
“Baada ya kuchukua kiasi hicho cha fedha kwa madai ya kulipa gharama zao za uendeshaji, Sh milioni 200 zinazobaki ndio wamekuwa wakizigawa tena kwa kuipa Halmashauri maduhuli ya asilimi 10 na vijiji asilimia 20 na wao wanachukua tena asilimia 70.
Huu ni wizi mkubwa sana. Kwani hata mikataba ya hao wanaowaita wawekezaji waliopewa vijiji vya huku Mafia hatuifahamu na madhumuni yao inaonekana ni kuchukua ardhi za wananchi na kuziuza wageni,” amesema.
Amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 1994 kwa kile kinachoitwa kuendeleza utalii wa bahari walianza kwa kuchukua vijiji vitatu, na matokeo yake hawakuishia katika maeneo hayo tengefu, walifika hata nchi kavu na kuchukua maeneo ya wananchi.
Hata hivyo ameongeza kusema kuwa Wilaya ya Mafia ina jumla ya vijiji 23 ambako vijiji 13 vimechukuliwa na MPRU na kati ya vijiji hivyo ni vitatu tu ndio waliwashirikisha wananchi na vingine wamevichukua bila kuwashirikisha.
“Ninyi JAMHURI, mmegusa mambo ya utendaji wa taasisi hiyo lakini kwa hiki kinachofanyika hapa Mafia hatukielewi. Mafia ni kisiwa kikubwa na vingine vidogo vidogo vinavyokaliwa na wananchi na vingine ni makambi ya wavuvi ambavyo vimeuzwa.
Mfano kijiji cha Shongimbili kimeuzwa na kujengwa Hoteli ya Nyota tano (Thanda Hotel) na jina la kijiji hicho limefutwa na eneo hilo kwa sasa linajulikana kwa jina la Thanda Highland, hakuna mkataba wala Halmashauri haina mapato yoyote, hakuna hata kibali cha ujenzi, na sheria lazima zifuatwe.
Waliwahadaa wananchi kwamba lengo lao ni kuhifadhi mazingira ya bahari na viumbe vilivyopo, pia kelele za wavuvi katika kambi zao zinawanyima uhuru kasa kutaga mayai lakini maeneo hayo wenyewe ndio wameyauza na kujengwa makazi ya kudumu.
Suala hili tumelifikisha kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na ameahidi kulishughulikia lakini hakuna kinachoendelea hadi sasa.
Waziri Mkuu alipofanya ziara yake hapa Mafia, Septemba mwaka jana tulilizungumza suala hili la MPRU, na akaitwa Meneja wa taasisi hii ili atoe majibu ya madai yetu mbele ya watu wote kwenye mkutano wa hadhara na kutoa majibu ya uongo na hivyo yakatolewa maelekezo na Waziri Mkuu kwamba tuunde kamati ambayo itakutana naye ofisini kwake.
Tulikuja Dar es Salaam viongozi wa Kamati hiyo lakini hatukuweza kuonana na Waziri Mkuu kutokana na majukumu aliyokuwa nayo ikiwemo kuhamia Mjini Dodoma.
Nasisitiza kuwa mwekezaji halipi chochote kama sehemu ya mapato ya Halmashauri. Taasisi hii iko kwa ajili ya kuuza maeneo yetu kwa watu wanaowaita wawekezaji na taratibu zinakiukwa, na sasa wana mpango wa kuuza maeneo mengine na kuiacha Wilaya ya Mafia katika umaskini wa kutisha,” amesema Dau.
Amesema Sheria ya MPRU hairuhusu kujengwa makazi ya kudumu kwenye maeneo ya utalii, na kujengwa kwa Hotel yenye hadhi ya nyota tano ni ukiukaji wa makusudi wa sheria hizo.
Pamoja na hayo amesema visiwa vya Nyororo na Mbarakuni navyo wanataka kuviuza kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa kisingizio cha uwekezaji wakati wananchi hawanufaiki kabisa na uwekezaji huo.
Amesema ada ya kiingilio kwenye maeneo hayo ya hifadhi ya bahari ni Dola za Marekani 200 kwa mgeni na kinachokusanywa ni kiasi kikubwa kutokana na wingi wa wageni wanaofika katika maeneo hayo lakini taasisi hiyo imeamua kufanya shughuli zake kienyeji na kulenga kuwadhulumu wananchi wa maeneo hayo.
“Kinachoshangaza zaidi maduhuli wanayopelekewa wanavijiji ambayo ni asilimia 20 hawapeleki fedha taslimu, na badala yake uongozi wa taasisi hiyo umekuwa ukihoji mahitaji ya wananchi na ikiwa ni ujenzi wa madarasa au kukarabati zahanati wao wenyewe wamejipa jukumu lisilowahusu la ujenzi wakati hawana wataalamu.
Mfano Shule ya Msingi Kibaoni, Kata ya Kiegeni wamejenga jengo la darasa chini ya viwango na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo na MPRU amekimbia.
Wakimaliza kazi yao ya ujenzi wanaandika: Jengo hili limejengwa kwa msaada wa taasisi ya hifadhi ya bahari. Huu ni uhuni, hawa sio wahisani na wanachopaswa ni kutulipa wanavijiji hiyo asilimia 20 na kufuata utaratibu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ndiye mwenye wataalamu na kitendo cha kutopitisha fedha hiyo hapo na kujihusisha na shughuli ambazo hawahusiki nazo hakikubaliki kabisa,” amesema.
Amesema Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi aliagiza fedha hizo zote ziingizwe moja kwa moja katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya lakini bado imekuwa ni tatizo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Erick Mapunda amelieleza JAMHURI kuwa wanaidai MPRU maduhuli ya mwaka 2011 hadi 2013 na 2015-2016 na hayo ni mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Mapunda amesema maduhuli ya mwaka 2014-2015 ambayo ni Sh milioni 92 waliwaletea mwezi Juni mwaka huu ambazo tayari amezipeleka katika vijiji husika na mwaka 2015-2016 zaidi ya Sh milioni 200 bado hawajawapa hadi sasa.
“Mgao wao una utata, kwani wanakusanya na kutumia na kinachogawanywa ni fedha zilizobaki baada ya kile wanachokiita gharama zao na kuchukua tena asilimia 70 na kutuachia asilimia 30 ambazo ni za vijiji na Halmashauri.
Mwaka wa fedha wa 2015-2016 wamekusanya fedha nyingi sana kuliko uwezo wa halmashauri ikiwa ni zaidi ya Sh milioni 100 lakini haieleweki wanazitumia namna gani fedha hizi na kutugawia mabaki.
Kwa ujumla hii taasisi iko kwa ajili ya kudidimiza sana uongozi wa halmashauri hii. Wanatoza ushuru na faini zilizo kinyume cha sheria.
Pia mkataba wa Hotel ya Thanda haueleweki na tumeomba watupatie, lakini wametukatalia na wamejenga Hotel hiyo ya nyota tano bila kutushirikisha chochote.
Licha kukataa kutupatia mkataba huo, tulichoelezwa ni kwamba waliosani mkataba huo ni MPRU na Mkuu wa Wilaya ya Mafia jambo ambalo ni kinyume kabisa taratibu,” amesema Mapunda.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ni kwamba uongozi wa taasisi hyo hauna bodi ya zabuni na kwamba shughuli zote za manunuzi zinazofanywa ni kinyume cha sheria.
“Shughuli zote za ujenzi na miradi mbalimbali ya wananchi inayofanyika kwa fedha zao ambazo hawajui kiasi gani walichopata hazina kibali cha bodi kwani taasisi hiyo inaendeshwa bila bodi ya zabuni.
Kutokana na utaratibu huu mbovu serikali inapaswa kufanya uchunguzi dhidi ya dhuluma hii wanayofanyiwa wananchi wa vijiji vya Mafia ili wanufaike na mapato yao,” kimeeleza chanzo hicho.