Idara ya Uhamiaji imeanza uchunguzi kuwapata watumishi wake walioshiriki kumpa hati ya kusafiria, Mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali (NGO) la Pastoral Women Council (PWC), Maanda Ngoitiko, anayedaiwa kuwa ni raia wa Kenya.
Shirika hilo linaloendesha shughuli zake Ngorongoro mkoani Arusha, linahusishwa na migogoro ya muda mrefu kati ya wawekezaji, wananchi na Serikali wilayani humo.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa awali, Maanda alikuwa na hati ya kusafiria yenye jina la Maanda Sinyati Ngoitiko, yenye Na. AB 113266 iliyotolewa Dar es Salaam, Januari 21, 2006. Hati hiyo iliisha muda wake Januari 20, mwaka jana.
Imeelezwa kuwa alipokwenda Uhamiaji wilayani Ngorongoro ili kupata hati nyingine, Uhamiaji waligoma, wakimtaka atoe vielelezo vya kuthibitisha uraia wake wa Tanzania.
“Tangu wakati huo hakuweza kuthibitisha uraia wake, kwa hiyo suala lake likawa bado linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi,” kimesema chanzo chetu.
Wakati hayo yakiendelea, JAMHURI likabaini kuwa tayari Maanda ameshapata hati nyingine ya kusafiria jijini Dar es Salaam, ilhali fomu zake za maombi zikiwa bado zipo Ngorongoro.
Msemaji wa Uhamiaji, Ali Mtanda, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo, na akaahidi kuwa ofisi yake itatoa ufafanuzi wa suala hilo baada ya kupokea taarifa kutoka Uhamiaji Mkoa wa Arusha ambako Maanda amehojiwa.
“Uhamiaji imetoa maelekezo ya kutomruhusu kusafiri hadi hapo suala lake litakapokuwa limemalizwa. Vituo vyote vya Uhamiaji nchini vimejulishwa kuhusu hatua hiyo,” amesema Mtanda.
Wakati Uhamiaji wakiendelea kuwapata waliomwezesha Maanda kupata hati ya kusafiria, taarifa nyingine zinawahusisha Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mfaume Taka, na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kuwa ndiyo waliofanikisha suala hilo.
Taka na Gambo wanatajwa kuwa na ushirika wa karibu na Maanda na NGOs nyingine ambazo kwa muda mrefu zimekuwa wapinzani wakuu wa Serikali katika migogoro inayoendelea Loliondo.
Hata hivyo, Taka amezungumza na JAMHURI na kusema hahusiki na suala hilo, licha ya kukiri kuwa anatambua Uhamiaji waligoma kumpa hati nyingine hadi hapo atakapothibitisha kama kweli ni raia halali wa Tanzania.
Mashirika ya PWC na Pingos Forum ambalo kiongozi wake ni Edward Porokwa, yanadaiwa kushirikiana na raia wa kigeni wanaochochea migogoro Loliondo.
Wiki kadhaa zilizopita, NGOs hizo ziliwaingiza nchini kinyemela raia wawili wa kigeni – Mfaransa, Profesa Jeremie Gilbert, na Mwingereza, Luke Tchalenko, ambao walifika Loliondo na kuchukua maelezo na picha ambavyo vinadaiwa kutumiwa kuichafua Tanzania kwa kuonesha kuwa inakiuka haki za binadamu kwa wakazi wa Ngorongoro.
Gilbert anatoka shirika la kimataifa la Minority Rights Groups (MRG), ilhali Tchalenko ni mpiga picha za filamu na majarida maarufu Uingereza, Kanada na Marekani ya The Times, The Globe and Mail na World of Interiors.
Raia mwingine wa Sweden, Suzan Nordlund, ameshafukuzwa nchini kwa PI mara kadhaa, lakini akawa anasaidiwa na NGOs kupenya na kuingia Loliondo kufanya uchochezi.
NGOs zaidi ya 30 zimekuwa zikijihusisha na masuala ya ‘utetezi’ Loliondo, idadi ambayo ilimshitua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipozuru Ngorongoro, Desemba mwaka jana.
Waziri Mkuu alimtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi ili kubaini ukwasi wa mashirika hayo na kazi zake ili yatakayobainika kutenda kinyume cha maombi ya kusajiliwa kwake, yafutwe.
Mgogoro wa Loliondo umedumu kutokana na viongozi wakuu wa Serikali wilaya na mkoa kuwa upande wa NGOs, hasa kwenye suala la kutengwa kwa eneo la kilometa 1,500 kwa ajili ya uhifadhi endelevu. Eneo hilo la Loliondo ndilo lenye asilimia 50 ya vyanzo vyote vya maji yanayoingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).
Taarifa za kiuhifadhi zimeainisha mara zote kuwa kufa kwa Loliondo maana yake ni kufa kwa SENAPA. Uongozi wa juu wa Serikali unasubiriwa kutoa uamuzi juu ya mapendekezo ya kuanzishwa kwa, ama Hifadhi ya Jamii (WMA), Pori Tengefu, au Pori la Akiba.
Mara zote NGOs zimejipatia mabilioni ya shilingi kutoka kwa wafadhili, na hatua hiyo inatajwa kuwa ndiyo kiini cha kutomalizwa kwa mgogoro katika eneo la Loliondo.