Klabu ya soka ya Simba leo Februari 2, imetangaza rasmi kumsamehe kiungo wao Clatous Chama Baada ya kumsimamisha kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Kupitia ukurasa wao wa Instagram Simba wametoa taarifa ya maamuzi hayo ambayo yamefanywa na kamati ya ufundi ya bodi ya klabu baada ya kupitia barua ya utetezi iliyoandikwa na Chama.
Aidha Taarifa hiyo imeeleza kuwa Chama ameungana na kikosi kilichopo mkoani Kigoma kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mashujaa FC.
Clatous Chama na mchezaji mwenzie Nassor Kapama walisimamishwa na Simba Desemba 21, 2023 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Hata hivyo Simba haijatoa taarifa juu ya Kapama.
Simba wanatarajia kushuka dimbani kesho Februari 03, katika dimba la Lake Tanganyika majira ya saa 10 jioni kuumana na Mashujaa FC.