Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar
CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimeanza kutoa Shahada za Umahiri kwa njia ya mtandao kwa fani sita njia ambayo imeanza kuchangamkiwa na wasomi wengi kutokana na kuwa nafuu kulinganisha na kusoma darasani.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanzishwa kwa kozi hizo.
Amesema CBE imekuwa ikitoa Shahada za Umahiri takribani 10 katika fani za biashara na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA na sasa wameona ni wakati muafaka kuanza kufundisha kwa njia ya mtandao.
“Kwa sasa tumeanzisha Shahada sita za umahiri mtandaoni ‘Online Master’s Degree’ kwa fani sita ambapo tayari tumeanza kupokea maombi kwa muhula wa Machi na kusoma kwa njia ya mtandao (Online) kuna faida kadhaa ambazo zimefanya njia hii ya kujifunza kuwa maarufu na yenye ufanisi kwa watu wengi,” amesema.
Aidha, Profesa Lwoga ametaja faida za kusoma kwa njia ya mtandao kuwa kunamwezesha mtu kusoma kutoka mahali popote na wakati wowote unaofaa bila kujali eneo lake au muda wa siku.
“Kusoma kwa mtandao mara nyingi hupunguza gharama zinazohusiana na elimu, kama vile usafiri, malazi, na vifaa vingine. Hii inafanya elimu kuwa nafuu zaidi na inawapa watu fursa ya kufuata masomo bila kuhitaji kuhamia au kutenga bajeti kubwa,” amesema Profesa Lwoga.
Amesema njia hiyo inawapa wasomi uwanda mpana wa kuchagua programu na inaruhusu wanafunzi kuchagua masomo yanayolingana na malengo yao na maslahi yao, bila kujali wanavyoishi.
Profesa Lwoga amesema kusoma kwa mtandao mara nyingi humuunganisha mwanafunzi na teknolojia za kisasa kama vile majukwaa ya mtandao, mabaraza ya mazungumzo na zana za ushirikiano na inaboresha uzoefu wa kujifunza.
Amesema njia hiyo inamwezesha mwanafunzi kushirikiana na wenzake kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Alisema kupitia njia hiyo wanafunzi wanaweza kusoma kwa kasi yao wenyewe, kurudia sehemu zenye changamoto, au kuchunguza zaidi masomo yanayowavutia na kwamba inaruhusu kila mtu kujenga uelewa imara wa mada wanazojifunza.
“Kusoma kwa njia ya mtandao huleta ubunifu wa rasilimali za kujifunza, na mara nyingi huja na rasilimali nyingi za dijitali kama vile video, vitabu vya elektroniki, na michezo ya kujifunza na hii inaboresha njia za kufundisha na kufanya masomo kuwa ya kuvutia zaidi na yenye kuvutia,” alisema.
Alisema wanafunzi wa kusoma mtandaoni wanapata uzoefu wa matumizi ya teknolojia, ambayo ni ujuzi muhimu katika ulimwengu wa kisasa wa kazi na inawawezesha kuwa tayari kwa changamoto za teknolojia kazini.
“Kwa ujumla, kusoma Online kunaweza kuwa chaguo linalowavutia wengi kwa sababu ya urahisi, ufanisi wa gharama na upatikanaji wa rasilimali za kujifunza,” alisema.
Alisema CBE imewekeza katika miundombinu bora, teknolojia ya kisasa na mazingira mazuri ya kujifunzia, huku ikiweka mkazo kwenye maadili ya kitaaluma na utawala bora mambo ambayo yameifanya CBE kuwa chaguo bora kwa wanaotafuta elimu ya biashara.