Si mara yangu ya kwanza kufika Arusha, lakini hii ni safari yangu ya kwanza kuzuru Arusha ikiwa “imepachikwa” hadhi ya kuitwa jiji. Kwangu mimi, Arusha ni “zizi.” Kama wingi wa watu ndiyo kigezo pekee cha mji kupandishwa hadhi na kuitwa jiji, basi watawala wetu watakuwa wanakosea.
Arusha ile niliyoijua miaka hiyo ndiyo hii ninayoiona leo. Barabara zinajengwa, lakini si kwa kiwango cha kunivuta hadi niamini kuwa kweli zina hadhi ya kuitwa barabara za jiji.
Maskini katika jiji hili ni wengi. Wanaishi katika nyumba ambazo si rahisi kuamini kama kweli zinapatikana katika ardhi ya tanzanite, ardhi ya utalii na kilimo cha mazao ya kila aina.
Mwenyeji wangu anasema ninayoyaona hapa katikati ya jiji ni “cha mtoto.” Anaamua kunipeleka hadi eneo la mbele kidogo ya Unga Limited. Huko nakumbana na mazingira ya kusikitisha. Watoto kwa watu wazima wanashiriki kusaka masalia ya vyakula kwenye dampo lililopo kando ya reli iliyotelekezwa miaka mingi. Pamoja nao, kuna makundi ya mbuzi na nguruwe -wote wanapishana na kunyang’anyana riziki inayoshushwa kutoka kwenye malori ya kubeba taka.
Muda ni jioni, mimi na mwenyeji wangu tunajiandaa kuzuru mji huu tuweze kujionea hali ya mambo. Tunakutana na watoto wengi mno wasiokuwa na makazi maalumu. Wanaitwa watoto wa mitaani. Katika eneo la mzunguko karibu na Arusha Hotel, tunawakuta kina dada wengi wakijiuza. Wanavuta sigara, bangi na wanatumia aina zote za vilevi, bila kusahau mirungi ambayo wanaiita “gomba.” Hii inaingizwa kutoka Kenya ambako imehalalishwa.
Kutoka hapa tunaelekea katika ukumbi wa Pin Point. Hapa kunachezwa disko. Mashabiki wengi wa hapa ni vijana. Kiingilio ni bure. Kwa sababu hiyo, wasichana ni wengi mno. Wanapatikana kuanzia chini hadi ghorofa ya kwanza ambako ndiko kwenye burudani. Ndani ya ukumbi wanaume ni wachache, hali hii inawafanya wanaume wawe na soko lisilo la kawaida.
Gharama ya hapa Pin Point ni bei ya vinywaji. Soda inauzwa Sh 1,000; ilhali bia za Tanzania ambazo kwa bei ya kawaida zinauzwa Sh 1,800; ndani ya ukumbi huu zinauzwa Sh 2,500.
“Kaka naomba kiroba.” Ndiyo salaam ninayokutana nayo kabla ya kuulizwa swali jingine. Wakati nikijiandaa kujibu, naulizwa, “Vipi una mtu? Usiwe na wasiwasi, tuelewane tu.” Daa, hali hii si ya kawaida. Sikuzoea kutongozwa. Najitahidi kujifaragua, lakini binti anaendelea kunikazia macho huku akinisogelea mithili ya chatu asogeleavyo mawindo!
Ghafla najifanya ninapokea simu, hivyo naelekea barazani kukwepa adha hizi za kutongozwa. Ninachofanya ni sawa na kuruka majivu na kukanyaga moto. Hapa kwenye baraza kuna wasichana wasio na idadi. Wote wanajitahidi kunisogelea pengine kwa kuamini kuwa nahitaji wa kuondoka naye.
“Tutaondoka kwa shilingi ngapi?” Namuuliza msichana ambaye kwa haraka haraka nakisia kuwa ana umri wa miaka 22 hivi. Anajibu, “Wewe sema tu, kama una arobaini sawa, twende hadi asubuhi”. Mimi naanza “kubageini.” Namweleza, “Mimi nitakupa Sh 15,000.”
Msichana anakomaa, anataka Sh 20,000. Muda ni saa nane usiku, namweleza anisubiri nikakague gari tuondoke. Anakubali, na hilo linakuwa kosa kwake. Namchukua mwenyeji wangu kinamnanamna hivi tunaondoka Pin Point na kurejea hotelini. Nalala.
Muda ni asubuhi. Tunapata kifungua kinywa na mwenyeji wangu. Tunaanza kukumbushana yaliyojiri usiku. Ananishangaa namna ninavyoshangaa. “Ulichokiona ni cha kawaida kabisa, sasa kama utakubali, nikupeleke mahali ukajionee mambo.” Nakubali nikiamini kuwa ziara hiyo itakuwa usiku.
Ananishitua baada ya kunieleza kwamba anakonipeleka, shughuli ya ukahaba inafanywa kwa saa 24. Hakuna saa wala siku ya kumzika!
“Uliwahi kuona mlango wa mapokezi kituo cha polisi ukiwa umefungwa?” Ananiuliza, nami namjibu, “Sijawahi, pengine kituo kiwe kimehamishwa.” Anasema, “Basi hapo tunapoenda ‘ofisi’ haifungwi.”
Saa 2:45 tunawasili eneo linaloonekana kuwa na nyumba nyingi za wageni pamoja na baa. Mbele yetu kuna maandishi yanayosomeka, “Karibu Mrina Annex”.
“Haya wewe ingia ndani, mimi nakuacha hapa nitarudi baada ya dakika 40 hivi. Utapata huduma zote, kuanzia supu, vinywaji na hayo mengine,” ananieleza mwenyeji wangu, huku akitambua kuwa “hayo mengine” kwa kweli sina mpango nayo.
Naingia Mrina Annex. Napokewa na wanywaji wengi walio kushoto na kulia kwangu. Naingia moja kwa moja. Kushoto naona kaunta ya vinywaji. Kulia kuna wanaume na wanawake walioketi – wengine wakionekana kurembua (kulegea macho) pengine kutokana na ulevi.
Napita mlangoni kama vile naelekea msalani. Hapo nawaona wanaume na wasichana takriban 18 wakiwa wameketi na wengine wakiwa wamesimama. Wengine wanatazama televisheni (iliyonipa mgongo); na kushoto wapo wengine wanaochangamkia supu.
Upande wa kushoto na kulia kuna kijiukuta kifupi kilichojengwa, lakini kikiwa hakikufika juu kwa sababu milango ya vyumba vya kulala inaonekana. Najiona mgeni kweli kweli, lakini katika kuuficha ugeni wangu, naamua kununua bia moja nifananefanane na hawa niliowakuta hapa.
Ninapojiandaa kwenda kununua bia, sauti zinapazwa, “Kaka karibu, karibu, usiondoke.” Nawajibu, “Nachukua kinywaji, nakuja.”
Kusikia hivyo, wanatulia. Nachukua bia. Narejea nilipokuwa. Sikuzoea kutazamwa na wanawake zaidi ya 10 kwa wakati mmoja, kibaya zaidi, wote wakiwa wanahitaji kufanya ngono na mimi. Muda wote niliopo hapa, vijana kwa watu wazima wanapishana mithili ya wanunuzi wanaokagua bidhaa.
Wasichana hawa wapo wa maumbo ya kila aina. Kuna wanene, wembambe, weusi na weupe. Wanavuta sigara na kutafuna mirungi muda wote. Mavazi yao ni suruali zinazoacha nguo za ndani zikionekana.
“Kaka karibu, twende chumbani,” naambiwa. Nami najifaragua, na kuuliza, “Bei gani?” Anajibu, “Short time ni Sh 7,000 kama unachukua chumba, lakini kama mimi nachukua unapaswa ulipe Sh 8,000. Kati ya hizo, elfu tatu ni kwa ajili ya chumba na zinazobaki ni zangu.” Da, jibu hili linanitoa jasho. Namuuliza kama ana vifaa vya kujikinga na maradhi kama ukimwi.
“Hilo lisikupe shida, vifaa vipo, mteja anayekataa kuvitumia na sisi hatumtaki. Mimi nimeacha mtoto wangu Moshi, sitaki nife nimwache. Hapa ninachuma, lazima nizingatie usalama wangu,” ananijibu.
Jambo la kustaajabisha ni kwamba wasichana hawa hawana muda wa kutazama pembeni, isipokuwa kule mbele wanakoingilia wateja. Wengine wamesimama karibu na njia ya msalani kwa ajili ya kuwapokea wateja na kuingia nao vyumbani.
Lakini wakati haya yakiendelea, muziki wa Injili nao unapigwa. Baadhi ya maneno kwenye wimbo huu ni: “Zunguka, umenizunguka. Shetani na watu wake wamekalia misumari, wema wa Mungu umenizunguka, walitaka nife kwa magonjwa, lakini wema umenizunguka.”
Kana kwamba haitoshi, mzee mwenye umri wa miaka zaidi ya 70 anaingia hapa akiwa anauza rozari. Sina hakika kama zimebarikiwa. Babu huyu anamsogelea karibu kila msichana aliyepo hapa akiwashawishi wanunue, lakini mwisho anaondoka bila kuuza japo moja. Anaondoka huku akiwa anapigana vikumbo na makumi ya wanaume wanaoingia hapa Mrina Annex kupata huduma ya ngono.
Wasichana watatu wametoka vyumbani kuwahudumia wateja. Wamebaki wakiwa wamesimama njiapanda kuelekea vyumbani. Mwenzao mmoja anawaambia kwa sauti kali, “Jamani zamu yenu imeisha, njooni huku.” Mwingine anaongeza, “Wanajifanya hawasikii.” Mmoja kati ya wale watatu anajibu, “Hatujasikia, mtasema sana.”
Baada ya kuona sichangamki, mmoja ananisogelea na kuniuliza, “Kaka wewe vipi? Unatuogopa? Nichukue mimi basi.” Kauli hiyo inanifanya nitazame chini. Muda wa mwenyeji wangu kurejea naona unapita. Nasingizia kwenda kumpokea mgeni wangu. Mbinu hiyo inanifanya niachwe niende nje.
Wakati nikiwa bado natafakari, namwona mwenyeji wangu akiwa mbele yangu. Anacheka na kuniuliza, “Vipi mzee, umejionea mambo? Basi, hapa Jumamosi hupati nafasi, kuna wanajeshi wanaokuwa kwenye mafunzo kule Monduli, huwa wakipata posho wanashuka hapa. Siku hiyo huduma ni kwao tu hadi jioni.”
Naam, naondoka nikiwa natafakari mengi. Najiuliza kama kweli aina hii ya maisha inaweza kuwa na tija kwa wasichana hawa! Nashindwa kujiridhisha kama kizazi hiki kitapita salama.
Mwisho, narejea kwenye maandiko ya kimapokea yanayosema, “Pombe na ngono ndiyo biashara kongwe kuliko zote duniani.” Pengine ni kwa sababu hiyo, hata Halmashauri ya Jiji la Arusha pamoja na Jeshi la Polisi, wameibariki biashara hii ndani ya Mrina Annex na hata kupafanya pawe kivuli cha wanaume wakware wanaozuru jiji hilo.
Swali moja nitaulizwa na unayesoma hapa, “Je, ulishinda vishawishi au na wewe uliamua kufanya practical? Jibu liko wazi, nilikosa ujasiri. Sikuthubutu kuvunja amri ya sita!!