Wanangu, poleni na kazi na hongera sana kwa kuvuka mwaka 2012. Nasikia mnapeana “Happy New Year” kila ninakopita na mnashangilia kwa nguvu, sina hakika mnashangilia kwa sababu zipi, lakini nafikiri kuumaliza mwaka siku hizi ni kazi ya ziada kutokana na maradhi na misukosuko mingi ya maisha.

Kuna maajali yanayotisha kutokana na matakwa ya walimwengu wenyewe. Kwa ufupi mnamtafuta mchawi miongoni mwenu.

 

Wiki kadhaa sasa nimekuwa na ndoto ya kushika madaraka makubwa katika nchi hii, lakini kila nikifikiria umri wangu naona upo ki-TANU TANU zaidi, hivyo siwezi kushika madaraka ya kisasa ambayo labda lazima uende na wakati, uwe wa fasheni, mazungumzo, dili, kujuana na watu wazito wazito, na labda uwe kwenye mfumo wa siasa.

 

Wanangu, mimi siwezi kwa sababu kubwa moja – hakuna anayenijua hata wa kupendekeza jina langu nje ya hapa Kipatimo ambako nilipewa madaraka ya uzee wa baraza, lakini nilienguliwa mapema baada ya kujifanya najua sana kufuata sheria na mambo yanakuwa marefu bila sababu. Kumbe wenzangu walikuwa wanakula nauli na wanatafuta njia za mikato, masikini Mzee Zuzu nikamwaga kibarua.

 

Ndoto zangu zinakuwa kama za maono kwamba ipo siku rais anaweza akaamua bila kunijua na kujali umri wangu, kunijaribisha niwe waziri. Hiyo ndiyo ndoto ninayoitaka ili athibitishe kuwa TANU YAJENGA NCHI, atathibitisha kwa vitendo na jinsi nitakavyovuruga hizo dili, kujuana, fasheni, kwenda na wakati, mazungumzo ya pembeni na kadhalika.

 

Nimehisi madaraka mengi na baada ya kufikiria naona mengine kama yatakuwa na vikwazo. Niliwahi kufikiria kama ningelikuwa waziri wa usalama barabarani, lakini rafiki yangu ambaye sasa ana upofu wa umri, aliniambia hizo sheria zangu zingenifika mwenyewe kwani mvunja sheria ni mwanasheria mwenyewe kama ilivyokuwa zamani, kuwa mvunja nchi ni mwananchi mwenyewe japokuwa zamani ilikuwa na maana ya kuilinda ardhi yetu.

 

Wanangu, leo naomba rasmi kwa rais alivunje baraza la mawaziri alilonalo, ajaribu kutenganisha mambo katika kila wizara ili ikiwezekana huu mzigo mkubwa alionao kila waziri upungue na tuweze kumpata wa kumtoa kafara, maana wakati mwingine unakuta waziri anatakiwa ajiuzulu kwa kosa lisilokuwa lake. Mkurugenzi fulani tu anaamua kwa manufaa yake kufanya uzembe ambao unamlazimu waziri ajiuzulu.

 

Wanangu, mimi ningekuwa naruhusiwa kutoa ushauri ningesema kuwa afadhali tuwe na mawaziri hata mia tano, lakini kila mmoja akashika kitengo chake ambacho tungeweza kumuuliza kwa uhakika kabisa anafanya nini pale ambako linaonekana tatizo kujitokeza. Waziri mhusika awajibike kwa kosa lake na si kosa la mkuu wa kitengo.

 

Leo wanangu ningeomba rais aniteue kuwa waziri wa dawa na matibabu. Ningeomba wizara hiyo kwa sababu ya kero ambazo naziona. Kwanza, kero kubwa ingekuwa kuwaacha akina Mzee Zuzu bila matibabu kwa sababu hawana fedha za matibabu. Hii inatokana na uchungu ambao naukumbuka kwamba zamani enzi za TANU, wazee, vijana na watoto wote tulikuwa tunapata matibabu bure na dawa zilikuwa zikipatikana kwa wakati. Ningeomba wizara hii ili nirudishe heshima hiyo.

 

Wanangu, ningeomba kuwa waziri katika wizara hii kwa sababu najua ninachotaka kufanya. Ninajua kuwa Watanzania wanaumwa nini na wanahitaji dawa gani kwa wakati gani kwa umri gani, kama ilivyokuwa wakati wa TANU. Si vibaya kuwa na marejeo ya zamani na hasa kama yalikuwa na manufaa kwa umma.

 

Wanangu, nikipewa wizara sitaruhusu zabuni kwa sababu, mojawapo ya matatizo makubwa katika uhai wa binadamu ni kucheza na afya yake. Ningetoa oda maalumu kwa wale wanaotengeneza dawa za matibabu na si dawa za biashara. Ningerudisha tiba za zamani ambazo ulikuwa ukitumia unapona badala ya kuendelea kuugua.

 

Wanangu, dawa za kuponya maradhi zilikuwapo na bado zipo japokuwa utaratibu wa sasa wa zabuni naamini unatupeleka katika kupata dawa za kibiashara zaidi. Mimi nikiwa waziri nitajaribu kurudisha dawa zile zinazoitwa zimepitwa na wakati kwa sababu ya kujulikana kwa bei yake. Sitoweza kuziacha cafenol, aspro, minyua, mkojo wa punda na nyinginezo.

 

Sitaziacha hizo dawa kwa sababu wakati wa TANU ndizo zilizotufanya tukawa na afya njema na hatukuugua wala kufa kwa sababu ya dawa. Hatukuwa na malaria kwa sababu ya matumizi ya DDT na tulikuwa tukilala na DDT vyumbani na hatukudhurika hadi leo. Sielewi na wala hainiingii akilini kwa nini mataifa yanayotengeneza dawa za kileo yaseme kuwa DDT ni sumu ilhali tuliitumia bila matatizo na si kuua mazalia ya mbu tu, bali kutunza mazao ya shamba na katika vihenge.

 

Nikiwa waziri nitaagiza klorokwini, niacin, rangimbili, homakwini gauze, boscop, kwinini, salfa, jivii, karimangano, andrews, sodabaikafu na chumvi ya mawe maana matibabu yake naona bado yana nguvu kuliko hizi dawa za “ki-dotcom” ambazo ukinywa leo kesho homa inapanda.

 

Najua nawakera wengi, lakini namuomba rais aniteue niwe waziri wa dawa na matibabu, muone jinsi ninavyoweza kurudisha matibabu ya TANU na uponyaji wake kama wa roho mtakatifu. Mimi bado baadhi ya dawa ninazo pamoja na ku-expire kwake, lakini nakunywa na ninapona.

 

Mheshimiwa rais anzisha hii wizara mpya nisafishe haya masumu yaliyopo. Nataka dawa za kweli za matibabu, sitaki dawa za biashara na mwisho, lakini si kwa kujipendekeza ili unichague kuwa waziri. Nasema Heri ya Mwaka Mpya na Mungu akupe nguvu ya maono ya kutupatia mawaziri, makatibu, wakurugenzi na wakuu wengine wenye moyo na taifa letu, kwani taifa litajengwa na sisi wenyewe.

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu

Kipatimo