na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi, Aisha Amour, kutafuta haraka mkandarasi wa kujenga daraja la Nzali, lililopo wilayani Chamwino, mkoani Dodoma mara tu baada ya hatua za usanifu wa daraja hilo kukamilika.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Chilonwa na Itiso wilayani humo, Bashungwa amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kulijenga daraja hilo ili kuunganisha mawasiliano ya kata hizo mbili ambazo hukumbwa na adha ya kukosekana mawasiliano hususan katika kipindi cha mvua.
“Nikuahidi ndugu yangu Ndejembi, baada ya usanifu kukamilika, na baadae kujua gharama zake, hakikisha Katibu Mkuu unaleta Mkandarasi hapa ili daraja hili kujengwa”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa mita 60 na kina cha mita 8 utaambatana na ujenzi wa barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 1.5.
Kadhalika, Bashungwa amesema kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miradi mbalimbali ya miundombinu nchini ili kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, ambaye pia ni Mbunge wa Chamwino, Mhe. Deo Ndejembi, ameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua ya kuanza usanifu wa daraja hilo kwani watu wengi ikiwemo wajawazito hupoteza maisha hususan kipindi cha mvua kutokana na kujaa maji kwa daraja hilo na kushindwa kupita upande wa pili kufuata huduma za kiafya.
Amemuomba Waziri Bashungwa kuhakikisha mkandarasi anafika eneo la ujenzi ili kuwasaidia wananchi wa Itiso ambao barabara hiyo ndio uti wa mgongo katika maisha yao.
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Eng. Colman Gaston, amemueleza Waziri Bashungwa kuwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na ukamilishaji wa uandaaji wa nyaraka za zabuni unatarajiwa kukamilika Machi, 2024.