Niliposikia kwamba wananchi wa Mtwara wameandaa maandamano kupinga usafirishaji gesi kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam, sikuamini. Kutoamini kwangu kulitokana na dhana iliyojengeka kwa miaka mingi kwamba wakazi wa mikoa ya kusini si “wakorofi” kama walivyo ndugu zao wa mikoa kama Mara, Kilimanjaro au Arusha.
Kabla ya kuendelea kujadili mada hii, niseme wazi kuwa siungi mkono mbinu au hatua zozote za kuuvunja umoja na mshikamano wetu Watanzania. Kwa miaka yote tumeweza kuishi kama ndugu wamoja. Kuishi kwetu kwa njia hiyo kumechochewa kwa kiasi kikubwa na matumaini tuliyopewa na viongozi.
Viongozi wetu walipowaeleza wananchi kwamba Tanzania ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea, walau nadharia hiyo iliweza kuonekana, ingawa wanafiki walikuwa wengi. Leo hatuna sababu ya kuuliza nani alikuwa muumini, na nani hakuwa muumini wa kweli wa Ujamaa na Kujitegemea.
Wapo Watanzania waliosoma shule moja na watoto wa marais, mawaziri wakuu, mawaziri, wakurugenzi na viongozi wa kada mbalimbali. Watoto wa viongozi walikwenda JKT kwa mujibu wa sheria na kutendewa kama walivyotendewa watoto wa makabwela.
Tanzania ya wakati huo ilikuwa moja. Wengi, kama si wote, tulitibiwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za hapa hapa nchini.
Leo, matumaini hayo hayapo. Kumeibuka matabaka makubwa ya matajiri na makabwela – walionacho na wasiokuwa nacho. Kwenye matokeo ya mitihani ya darasa la saba yaliyotangazwa juzi, sidhani kama kuna mtoto wa diwani aliyekuwa akisoma katika hizi shule za umma! Sijui kama kuna mtoto wa DC anayesoma katika sekondari ya kata, ukiacha familia ya DC wa Kilindi mkoani Tanga.
Tanzania ya leo ni ya matabaka. Wakubwa wanaposumbuliwa na upele unaosababishwa na joto, uchunguzi wa afya zao unafanywa India, huku masikini wakifariki dunia kwa kukosa tiba kwa magonjwa yanayozuilika. Mambo haya yote yameibua hasira za makabwela dhidi ya viongozi na matajiri katika Taifa letu. Maandamano ya ndugu zetu wa Mtwara ni matokeo ya hasira hizi.
Bila kumung’unya maneno, niseme wazi kwamba naunga mkono maandamano hayo. Tena sijui kwanini hawakutoa mwaliko ili wengi tuweze kushiriki. Naunga mkono maandamano hayo kwa sababu yamelenga kudai haki, na wala si ya kuivunja nchi.
Wananchi wa Mtwara wana haki ya kuzaliwa ya kuhoji namna watakavyonufaishwa na utajiri wa gesi na baadaye mafuta. Hiyo ni haki yao ya msingi ambayo haipaswi kuhojiwa wala kuzimwa na yeyote awaye. Lazima wajisemee wenyewe. Hakuna mwekezaji wala kiongozi wa Tanzania – katika lindi hili la uporaji rasilimali za nchi – atakayethubutu kuwatetea. Hakuna.
Maandamano ya Mtwara ni kiashiria cha wapi nchi yetu inakoelekea. Serikali makini haipaswi kupuuza hili jambo. Lazima iketi na wananchi. Iwaelimishe na iwahakikishie manufaa watakayopata kutokana na ukwasi utakaotokana na gesi na hata mafuta.
Mtwara wameng’amka. Hawataki kurejea makosa yaliyowapata ndugu zao wenye madini katika maeneo mbalimbali nchini. Hawataki kuona wakiishi kama ndugu zao wa Buhemba mkoani Mara, ambao sasa wamebaki na mashimo kama kivutio cha wageni wanaofika kushuhudia uporaji dhahabu ulivyofanywa na kampuni ya kitapeli ya Meremeta iliyopata baraka zote za viongozi wakuu wa Serikali hii hii.
Wananchi wa Mtwara si wajinga. Si mbumbumbu. Wapo waliotembea hadi Buhemba. Wameyaona mashimo yale ambayo sasa ni janga kwa mazingira ya eneo hilo na Mkoa wa Mara. Wapo waliosoma au kusikia athari hizo kupitia vyombo vya habari. Ni kutokana na uelewa huo, Mtwara wamesema hawataki kurejea makosa ya wenzao.
Wakati kampuni ya Meremeta ikipora dhahabu Buhemba, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Profesa Philemon Sarungi, aliwatetea eti kwa kile alichodai kwamba kampuni hiyo ilikuwa ikiwanufaisha wakazi wa eneo hilo. Nakumbuka nilindika makala ndefu kupinga hadaa hiyo, hasa pale alipodai kwamba wametengenezewa barabara. Fikiria, wewe una dhahabu. Inachukuliwa na wanaojiita wawekezaji, halafu unabaki ukishangilia barabara ya vumbi!
Profesa Sarungi wakati akisambaza hadaa hizo, Meremeta wakawa wameingia mkataba na vijiji vya Butiama, Rwamkoma na Bisarye, wa kutumia maji kutoka katika Bwawa la Kyarano. Bwawa hilo lilijengwa na Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo. Mkataba ule ni wa kijinga kweli kweli. Walichoambulia Butiama ni kujengewa vyumba viwili vya madarasa na bwawa kukauka.
Buhemba kwenyewe hakuna chochote kilichowekwa na waporaji waliorembwa kwa jina la wawekezaji.
Hawakujengewa darasa, zahanati wala mradi wowote wa maana. Hadi waporaji hao wanaondoka, Buhemba ikawa imefanikiwa kupanda chati ya maambukizi ya Ukimwi. Baadaye ndiyo tukang’amua kuwa kumbe yale mashimo makubwa na ya kutisha yaliachwa ili yatumike kama makaburi kuwazika watakaokufa kwa Ukimwi!
Wezi hao walipoondoka, waliacha kila kitu – mitambo, mashine, majenereta, magari, nyumba, samani, boti, na kila walichokuwa nacho! Kwanini waliviacha vitu hivyo? Waliviacha kwa sababu walikuwa wamepora dhahabu kiasi kwamba hawakuwa na sababu ya kuondoka na “takataka” yoyote. Huo ndiyo uwekezaji wa Tanzania ambao sasa Mtwara wanaandaliwa kuupokea!
Nimefurahishwa na nadharia za kimaendeleo za Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo (Mapesa). Kwa suala la uwekezaji, Cheyo mara zote amesisitiza kuwa ni vizuri wananchi wanaoishi kandokando ya migodi ya madini, wafanane na utajiri unaopatikana katika maeneo hayo. Amekuwa akitoa mfano wa Bulyanhulu, Buhemba, Geita, Nzega, Kahama, Mwadui, Mererani; na kadhalika.
Msimamo huu ni wa maana sana. Haiwezekani mtu anayeishi mahali kunakochimbwa dhahabu akawa na maisha yanayofanana na ya yule asiye na dhahabu. Ni kwa sababu hiyo hiyo, viongozi wetu mahiri waliamua kuikataa mikataba dhalimu iliyowekwa na wakoloni kuhusu matumizi ya maji ya Ziwa Victoria.
Kwa kufuata mkataba kati ya Uingereza na Misri, Watanzania hawana haki ya kutumia maji ya ziwa hilo bila ridhaa ya Misri! Huu ni upuuzi ambao Mwalimu Nyerere aliukataa hata kabla hatujajitawala, na kwa bahati nzuri Serikali zetu zilizofuata zimeendelea na msimamo huo huo.
Kwa uamuzi huo, ndiyo maana leo Kahama na Shinyanga wanakunywa maji kutoka Ziwa Victoria licha ya kelele zinazopigwa na Misri. Ni uzuzu kuheshimu mkataba wa kipuuzi wa aina hiyo na kuwaacha Watanzania wenzetu na mifugo yao wakitaabika kwa kukosa huduma ya maji.
Ni kwa sababu hiyo hiyo, wananchi wa Mtwara wana haki ya kuelezwa na kujiridhisha juu ya utajiri wa gesi iliyopatikana mkoani mwao. Haiwezi kuwa haramu kwa Misri kuizuia Tanzania kutumia maji ya Ziwa Victoria, lakini ikawa halali kwa Serikali ya Tanzania kuwanyima haki wananchi wa Mtwara kuifaidi gesi yao. Wala katika hili Serikali isitake kujifaragua kwa kutaka kupotosha kuwa maandamano na sauti za kuhoji jambo hili ni kuhatarisha umoja wa nchi au kuligawa Taifa letu.
Wananchi wa Mtwara “dhahabu” yao ni gesi. Lazima wanufaishwe nayo kwanza. Wananchi wanaoishi kando ya Ziwa Victoria wana haki ya kuanza kula samaki kabla ya kuwasafirisha kwenda Ulaya. Wananchi wanaozunguka hifadhi za Taifa wana haki ya kufaidika kwanza na hifadhi hizo kabla ya wengine walio mbali. Wanaoishi kwenye ukanda wa madini, wafaidike kwanza wao. Kufanya hivyo si kwamba kunasababisha utengano katika nchi, bali kunazidi kuwafanya wananchi katika maeneo hayo wawe wadau wazuri wa kuhakikisha kunakuwapo uendelevu kwenye rasilimali husika.
Tena basi, nikifika hapa ndipo ninapoona umuhimu wa kuwa na sera ya majimbo. Mikoa hii hii tuliyonayo sasa iendeshwe kimajimbo. Kila jimbo lichume na lijiletee maendeleo yake, ziada iingizwe kwenye Serikali Kuu ili itumike kuziba mapengo ya kule kusiko na rasilimali nyingi zaidi (ingawa Tanzania hakuna mkoa usio na rasilimali -kama upo, nisutwe).
Kuzungumzia majimbo sidhani ni dhambi. Kwa hali ilivyo sasa, ya kila kitu kuratibiwa Dar es Salaam, haki ya Mungu tutabaki hivi hivi! Haiwezekani Waziri wa Elimu akajua shule ya msingi kule Nyamongo au Kasesya au Itungi ina walimu au haina. Hawezi. Majimbo hayamaanishi ukabila, bali yanasaidia kupeleka maendeleo karibu na wananchi.
Narejea kusema kwamba Mtwara wana haki ya kudai maelezo na kuhakikishiwa namna watakavyonufaishwa na utajiri wa gesi. Mtwara wameonesha mfano mzuri. Wananchi katika mikoa mingine nao wajitokeze kuhoji namna wanavyofaidika na utajiri wao. Watakaovunja amani si wanaohoji, bali hawa watawala wanaotaka kufunika mambo na kuendelea kuongoza kwa mazoea. Wananchi wamechoka kuporwa na kuibiwa rasilimali zao.
Mtwara wameona hawafaidiki na hadaa za viongozi wa Serikali. Wameona nchi hii bila kusimama kidete, hakuna cha maana watakachoambulia. Wameona matibabu nje ya nchi ni ya wakubwa. Wameona korosho inaporomoka kila siku ilhali wakubwa wakizidi kununua na kutembelea mashangingi.
Kila siku wanasikia namna wajumbe wa Bodi ya Korosho wanavyolipana posho hadi kuwapa hata wake zao wasio wajumbe! Hawaoni watoto wa viongozi katika shule za kata. Hawaoni mwanga mbele ya safari. Walichoamua kukifanya ni kitu halali. Binadamu mwenye akili timamu lazima ahoji. Mtwara wamehoji. Lazima wapewe majibu.
Tena basi, majibu hayo yawe chanya kwao na kwa Taifa zima. Gesi haijachimbwa, lakini tayari tuna watu waliokwishatajirika. Mtwara endeleeni kuhoji. Kwa salamu hizi nawathibitishia kuwa tupo pamoja na tutaendelea kuwa bega kwa bega hadi mtakaposhinda.