Mwaka 2012 utakumbukwa pamoja na mambo mengine nchini, kwa matishio kadhaa yakiwamo ya uharamia baharini, wahamiaji haramu, biashara haramu ya usafirishaji binadamu, ajali za barabarani, biashara ya dawa za kulevya, uingizwaji wa silaha haramu, bidhaa bandia, uhalifu dhidi ya mazingira na maliasili.

Taarifa za Jeshi la Polisi zinasema hadi sasa Tanzania haijakumbwa na tishio dhahiri la ugaidi, lakini haikuacha kuchukua tahadhari dhidi ya tishio hilo. Tahadhari hizi zinazochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama likiwamo Jeshi la Polisi,  zinazingatia ukweli kwamba baadhi ya nchi  zinazoizunguka Tanzania zinashiriki mapambano na makundi ya kigaidi.

 

Katika taarifa ya matukio ya uhalifu nchini mwaka 2012, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Isaya Mungulu, anatahadharisha umma wa Watanzania kutobweteka kwani ni kweli pia kwamba nchi jirani za Kenya na Uganda, kwa nyakati tofauti hivi karibuni, zimekumbwa na mashambulizi ya kigaidi.

 

“Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi mipakani na maeneo nyeti, sambamba na kuwatahadharisha wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa za nyendo za watu au vikundi wanavyovitilia shaka,” anasema DCP Mungulu.

 

Kuhusu matishio ya uharamia baharini, taarifa zinasema vitendo vya uharamia katika Pwani ya Afrika Mashariki, vimekuwa vikifanywa na raia wa Kisomali wanaoteka meli za biashara za mafuta na bidhaa mbalimbali katika bandari zilizopo eneo la Afrika Mashariki, na zinazopita kwenda na kutoka nchi za kusini mwa Afrika. Awali, utekaji wa meli hizo ulikuwa ukifanyika zaidi katika maji ya Somalia na Ghuba ya Aden.

 

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Tanzania, tayari vitendo vya uharamia vimedhibitiwa kutokana na jitihada zinazofanywa kwa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine ndani na nje ya nchi.

 

DCP Mungulu anasema mwaka 2012 maharamia watano wamekamatwa mkoani Lindi wakiwa na bunduki tano aina ya SMG, mabomu ya RPG matatu na risasi 260 pamoja na meli ya uvuvi waliyokuwa wameiteka kutoka kwa wavuvi wa Sri Lanka. “Watuhumiwa wamefikishwa mahakamani na kesi zinaendelea,” anasema.

 

Kadhalika, kumekuwa na taarifa za watu kupatikana na silaha haramu na zinazomilikiwa kinyume cha sheria. Hali hii imetokana na kutokuwapo kwa amani ya kutosha katika baadhi ya Nchi za Maziwa Makuu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoonesha kuziathiri nchi hizo.

 

Kuhusu wahamiaji haramu na biashara haramu ya usafirishaji binadamu, Jeshi la Polisi limepambana, ingawa kumekuwapo ongezeko la kukamatwa kwa wahamiaji haramu nchini hususan kutoka nchi za Somalia, Ethiopia, Bangladesh na Pakistan.

 

Kwa mujibu wa DCP Mungulu, wahamiaji haramu waliokamatwa mwaka 2012 ni 1,714 na kwamba waliingia nchini kufuatia matatizo mbalimbali katika nchi zao.

 

“Mafanikio haya yamepatikana kutokana na taarifa zilizotolewa na wananchi kwa Jeshi la Polisi kupitia mpango wa Polisi Jamii na Ulinzi shirikishi,” anabainisha.

 

Anataja mikoa inayoongoza na idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa ikiwa kwenye mabano kuwa ni Mbeya (525), Kilimanjaro (488), Kigoma (157), Njombe (103), Kagera (83), Tanga (31) na Iringa (23).

 

Anaongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kukomesha biashara hiyo haramu kwa ushirikiano na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama na wadau mbalimbali kwa kuimarisha ulinzi mipakani na kufuatilia kwa karibu mitandao inayojihusisha na biashara hiyo.

 

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa uingizaji bidhaa bandia ni tatizo linaoonekana kupungua ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

 

Imebainika kuwa  bidhaa bandia zinazoingizwa nchini ni pamoja na vyombo na vifaa vya umeme zikiwamo TV, redio, simu, DVD Players, deck, nyaya, swichi, extension cables, generators, vipuri vya magari na pikipiki, mipira ya magari, dawa za binadamu, mifugo na za kuulia wadudu.

 

“Kupungua kwa tatizo hili,” anasema DCP Mungulu, “kumechangiwa na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wadau wengine zikiwemo Tume ya Ushindani na Mamlaka ya Uhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) na wananchi waliotoa taarifa zilizowezesha kupanga operesheni za kukamata.”

 

Habari zaidi zinasema mwaka 2012 imefanyika misako 19 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Ruvuma, Rukwa, Tarime-Rorya na Kilimanjaro, ambako watuhumiwa 128 walikamatwa na kati yao, 124 walitozwa faini na wanne wamefikishwa mahakamani.

Tatizo jingine lililoisulubisha Tanzania kwa mwaka 2012, ni ongezeko la makosa yanayohusisha uharibifu wa mazingira na maliasili za taifa.

 

Imebainika kuwa, kwa siku za karibuni, kumekuwa na ongezeko la makosa hayo na kupatikana na nyara za Serikali, kuchoma misitu, uvuvi haramu, uchimbaji madini, kokoto na mchanga kwenye maeneo yaliyozuiliwa, na wengine kuendesha kilimo katika maeneo ya hifadhi na uvunaji wa misitu kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.

 

Kwa mujibu wa takwimu za kipolisi kwa mwaka 2012, mikoa iliyoonekana kuwa na tatizo hili na takwimu za makosa ya kupatikana na nyara za Serikali zikiwa kwenye mabano ni Mara (164), Morogoro (80), Simiyu (49), Iringa (45), Manyara (43) na Arusha (41).

 

“Mafanikio ya kukamata nyara hizo yametokana na ushirikiano mzuri wa kioperesheni baina ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Maliasili na Utalii (Idara ya Wanyama Pori).”

 

Takwimu nyingine zinaonesha kuwa matukio ya kupatikana kwa dawa za kulevya za viwandani (heroin, cocaine, mandrax na morphine) yamedhibitiwa. Katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2012 matukio 482 yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio 565 yaliyoripotiwa katika kipindi cha mwaka 2011, ikiwa ni upungufu wa matukio 83.

 

“Mwaka huu tumekamata kiwango kikubwa zaidi cha dawa za kulevya kutokana na operesheni kabambe zilizofanyika, ambapo kilo 55,499 na watuhumiwa 6,933 vimekamatwa, ikilinganisha na kilo 17,776 na watuhumiwa 211 waliokamatwa mwaka 2011,” anasema DCP Mungulu.

 

Kuhusu ajali za barabarani, anasema tangu Januari hadi Novemba 2012, matukio makubwa ya ajali za barabarani yaliyoripotiwa ni 21,531, ikilinganishwa na matukio 22,208 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2011.

 

DCP Mungulu anaongeza, “Ingawa  matukio makubwa yamepungua, idadi ya ajali zilizosababisha vifo imeongezeka kutoka matukio 3,012 mwaka 2011 hadi matukio 3,144 mwaka 2012. Hili ni ongezeko la matukio 132.  Idadi ya watu waliokufa mwaka 2012 ni 3,655 na waliojeruhiwa ni 18,348, ukilinganisha na kipindi kama hicho cha mwaka 2011, ambapo waliokufa walikuwa 3,682 na waliojeruhiwa 19,238.”

 

Sambamba na kupungua kwa matukio makubwa ya ajali za barabarani, matukio madogo yamekuwa yakiongezeka.  Matukio madogo 548,600 yameripotiwa tangu Januari hadi Novemba 2012, ikilinganishwa na matukio 397,292 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2011. “Hivyo, kuna ongezeko la matukio 151,308 sawa na asilimia 27.6,” anasema DCP Mungulu.

Amezitaja sababu za ajali, hasa zinazotokana na makosa ya kibinadamu kuwa ni pamoja na ulevi, uzembe, mwendo kasi, uchakavu wa magari, ubovu na ufinyu wa barabara na ongezeko la vyombo vya usafiri.

 

Takwimu za matukio ya usalama barabarani zinaonyesha kuwa bado zinahitajika juhudi kubwa za kuendelea kuwaelimisha na kuwahimiza madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri kufuata kanuni, taratibu na sheria za usalama barabarani.

 

Kwa mujibu wa DCP Mungulu, silaha 889 na risasi 10,210 za aina mbalimbali zilikamatwa katika operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu tangu Januari hadi Novemba, 2012.

 

Anasema, “Agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Dk. Emmanuel Nchimbi) la kuwataka watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa hiari, katika kipindi cha mwezi mmoja wa Desemba linaendelea vizuri. Silaha 98 aina mbalimbali zimesalimishwa, zikiwemo za kijeshi na kiraia.”

 

Pia mwaka 2012 kumekuwapo na matukio kadhaa ya migogoro ya kisiasa, kidini na kijamii, iliyohusisha migomo na maandamano yasiyo halali yaliyosababisha uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali katika baadhi ya maeneo nchini.

 

DCP Mungulu anasema jitihada mbalimbali zilichukuliwa zikiwamo za kuwakamata wahusika wa matukio hayo na kuwafikisha mahakamani. “Vilevile elimu juu ya faida za kutii sheria za nchi bila kushurutishwa imeendelea kutolewa,” anaongeza.

 

Katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka, kila mtu kwa nafasi yake, taasisi za Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi za ulinzi, vyama vya siasa, madhehebu ya dini na wananchi kwa jumla, wanapaswa kuendelea kulipatia Jeshi la Polisi ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kukabili vitendo vya uhalifu nchini.