Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROAD) Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Mlima Ngaile amefariki dunia leo asubuhi wakati akishiriki mbio za Wiloles Foundation Marathon 2024 yenye lengo la kuchangia matibabu ya watoto waliozaliwa kabla ya muda wao (Njiti) katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Songea (HOMSO) Ruvuma.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wiliam Kapenjama Ndile, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa limetokea leo Januari 12, 2024 ,majira ya saa 3, asubuhi kwenye eneo la barabara karibu na baa ya Shefazi katika Kata ya Matarawe Manispaa ya Songea.
Amesema kuwa walifika asubuhi kwenye eneo la viwanja vya michezo vya Majimaji ambako walijisajili kisha wakaanza kukimbia umbali wa Km.5 ambao katika kundi lao iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile.
Amesema kuwa kabla hawajamaliza hizo Km.5 wakiwa mlimani mhandisi Ngaile aliwapita wenzake kwa kasi eneo la mlimani na haikuchukuwa muda ghafla alianguka ndipo zilifanyika jitihada za kumpatia matibabu ya huduma ya kwanza na kisha walimkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea (HOMSO) kwa matibabu zaidi.
“Ni kweli tukio limetukuta kwenye mbio za Wiloles foundation Marathon ambako tulikuwa tumeanza pamoja kukimbia lakini tulipofika maeneo ya barabara karibu na baa ya Shefazi mwenzetu alitupita kwa kasi baadae alianguka na alikimbizwa hospitali ambako ilidaiwa kuwa alipofikishwa chumba cha huduma ya dharula tayari alikuwa ameshafariki akiwa mjini.” amesema mkuu wa wilaya huyo.
Hata hivyo mkuu huyo wa Wilaya Kapenjama amesema kuwa tayari amewasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kwa ajili ya taratibu zingine ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na mwajiri wake kwa taratibu zaidi.
Mwenyekiti wa mbio za Wiloles foundation Marathon Yusuph Mwikoki amesema kuwa maandalizi ya mbio hizo yaliandaliwa vizuri kwa zaidi ya mwezi mmoja na leo majira ya saa za asubuhi ndipo mbio hizo zilianza ambazo ziliwashilikisha watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali na pamoja na wa vyama vya siasa.
Kwa upande wake kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma Marko Chilya alipohojiwa kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo amedai kuwa mhandisi Ngaile alifariki dunia wakati akiwa kwenye mbio za umbali wa Km.5 na kwamba tayari jeshi la polisi kwa kushirikiana na wataalam wengine wanendelea kufanya uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo cha kifo chake.
Juhudi za kumtafuta Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea (HOMSO) Magafu Majura, hazikuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa kwani ni miongoni mwa washiriki wa mbio hizo na ndie aliyetoa huduma ya kwanza wakati mhandisi Ngaile alipoanguka.