Gazeti Jamhuri linaungana na wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu (soka) barani Afrika kama si duniani kuwapongeza wachezaji viunga mahiri, Yaya Toure, Didier Drogba na Alex Song kwa kutwaa ushindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora barani Afrika.
Tuna kila sababu ya kuwapongeza vijana hao tukiamini kuwa walijituma kufanya kazi pevu iliyowawezesha kuibuka na ushindi huo miongoni mwa mamia ya wachezaji waliokuwa wanaiwabnia tuzo hiyo.
Jamhuri tunaamini kuwa ushindi huo wa wachezaji hao ni changamoto kubwa kwa wachezaji wengine kuongeza juhudi za kujituma ili nao siku moja waweze kutwaa tuzo hiyo.
Mcheza mahiri wa soka wa Manchester City, Yaya Toure, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora barani Afrika mwaka huu, huo ukiwa ni ushindi wake kwa mwaka wa pili mfululizo.
Toure amewapiku nahodha wa Ivory Coast na mshambulizi wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba aliyetwaa nafasi ya pili na aliyekuwa mlinda lango wa Arsenal, Alex Song, aliyeshika nafasi ya tatu katika tuzo hiyo.
Uteuzi umefanywa wiki iliyopita na makocha na maafisa wa kiufundi wa timu za soka barani Afrika ambazo ni wanachama wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Aliyekuwa mshambulizi wa Barcelona Samuel Eto’o ndiye anayeshikilia rekodi ya kushinda Tuzo ya Mchezaji Boara wa Afrika mara nyingi. Eto’o ameshashinda tuzo hiyo mara nne.
Mabingwa wa soka barani Afrika, Zambia, wametuzwa kuwa timu bora barani mwaka huu na kocha wao, Herve Renard, ameteuliwa kuwa kocha bora wa mwaka huu.
Song kwa sasa anaichezea klabu ya Barcelona naye Drogba anaicheza klabu ya Shanghai Shenhua ya China tangu Mei, Mwaka huu.
Toure, ambaye alishinda tuzo hiyo mwaka jana, ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa ya Ivory Coast, wanaoelekea nchini Afrika Kusini katika michuano ya Kombe la Mataifa Bingwa barani Afrika, itakayoanza Januari mwakani.
Matumaini ya wengi ni kwamba ushindi huo wa Toure, Drogba na Song ni utakuwa mwanzo wa wao kujituma zaidi, lakini pia utachochea ushindani kwa wachezaji wengine wenye vipaji mahiri vya soka barani Afrika katika kipindi cha mwaka ujao.