Kwa akili za kawaida kabisa, mtu unajiuliza kwani huo uislamu au ukabila umejikita katika mkoa wa mjini magharibi tu? Kwani Zanzibar na Pemba ni mkoa huo huo mmoja tu? Mbona kiserikali tunajua iko mikoa mitano Visiwani? Mjini Magharibi, Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa Kaskazini Unguja kuna Chakechake kule Pemba na Mkoani kule Kusini Pemba ?
Kwa nini vituko vyote vya Uamsho kama kuchoma makanisa 25, kuchoma baa 12 vitokee Stone Town na Viunga vyake tu? Hili ni jambo lile lile la Waarabu kulilia utawala wao wa Sultani kabla ya Mapinduzi! Ndiyo maana mimi naoanisha madai ya Kiongozi wa Uamsho Mwarabu Sheikh Farid ya kudai Serikali yao ya zamani ile ya kabla ya Mapinduzi kuwa halina tofauti na maandishi ya mwarabu mwingine Sheikh Issa Bin Nasser Al – Ismaily katika ukurasa wa mwanzo kabisa wa kitabu chake anachokiita ZANZIBAR : Kinyang’anyiro na Utumwa, pale anapodai namnukuu. “…
Kwa kutokana na maumbile hayo, tusistaajabu kuona kwamba taarikhi baina ya Oman na Zanzibar inajirejelea wenyewe mara kwa mara.” Halafu anahitimisha kwa kudai hivi, “Kabla ya hayo ‘Mapinduzi’ ya 1964 Zanzibar ilikuwa nchi huru yenye kujitawala wenyewe kikamilifu”. Maneno namna hii yanaonyesha wazi usongo walionao waarabu huko Zanzibar .
Wangependa Muungano usiwepo ili warejee kwenye unyonyaji wao ule ule wa enzi za usultani. Kumbe dini ya Kiislamu inaukataza udini na maadui wa Waislamu wametajwa katika Qur’an na wala siyo Wakristo ambao makanisa yao yamevunjwa na kuchomwa moto.
Waislamu kwa kadri ya maongozi ya Qur’an Tukufu sura ile ya V – MAIDAH, ibara ya 82 tunayakuta maneno haya, “Hakika utawakuta walio maadui zaidi kwa waislamu ni Mayahudi na mushirikina (polytheist). Na utawakuta waliokaribu kwa urafiki na waislamu ni wale wanaosema sisi ni Wakristu. Allah anasema marafiki wazuri kwa Waislamu ni Wakristo kwa sababu wanamcha Mungu, tena hawajivuni basi ni vema kuwafanya marafiki ili muige uvumilivu wao”.
Mwongozo huu wa Mtume Muhammad (S.A.W) kama ungefuatwa na kila Mwislamu kusingetokea uchomaji makanisa ambayo ni nyumba za ibada. Uamsho hao wanakwenda kinyume kabisa cha dini yao ama hawaijui Qur’an sura ile ya V ibara ile ya 82 au wana sababu zao za binafsi kuleta vurugu na mvunjiko wa amani Visiwani na Tanzania kwa jumla.
Mvunjiko wowote wa amani hutokana na kuvunja sheria za nchi. Kwa uelewa wangu neno ISLAM lina maanisha AMANI, basi Waislamu tungetarajia wawe watu wa amani kama neno la dini yao linavyomaanisha, wala si vinginevyo!
Mimi namshangaa sana huyu Mwarabu Sheikh Issa Bin Nasser Al – Ismaily anavyotamba kubeza Waafrika na Serikali yao ya Mapinduzi. Huyu kazaliwa mwaka 1927 Utaani, Pemba lakini anadiriki kumwona Kamishina wa Polisi Edington Kisasi kama mtu mdogo sana , amemwandika hivi; “Ni Mchaga, mkristo, Inspekta wa Polisi ni mgeni Zanzibar aliyeletwa Zanzibar na rafiki yake Mwingereza aliyekuwa Superintendent wa Polisi Zanzibar akiitwa Thorn katika miaka ya 1940 (Kitabu ZANZIBAR: Kinyang’anyiro na Utumwa uk . 127).
Huu ni upuuzi na uongo. Kisasi, mimi nimekuwa naye Zanzibar kama rika wangu. Tulikuwa na Hayati Mzee Mwita Marwa kama Brigedi Kamanda wa Nyuki, mimi kama Kamanda wa JKU na rafiki yetu mkubwa ndiye huyo hayati MBM Edington Kisasi. Sote tumezaliwa mwaka 1930 sasa haiwezekani kabisa mtoto wa miaka 10 mwaka huo 1940 (anavyodai alikuwa Inspekta wa Polisi na yeye Sheikh Ismaily akiwa mtoto wa miaka 13) akayaona haya aliyoandika. Huu ni uongo wa mchana kweupe (Waingereza wanaita naked lie).
Nimechombeza kipande hiki wasomaji muone hao wanaolilia Zanzibar walivyo hatari. Wako tayari kusema au kuandika uongo ili mradi Muungano uonekane hautakiwi na wananchi asilia wa Visiwani kumbe ni kulilia uhondo wa Stone Town tu. Mbona mikoa mingine hakuna vitimbi vya namna ya Sheikh Farid au Sheikh Issa Bin Nasser Al-Ismaily wanavyovitoa? Wana Uamsho wasisingizie dini ya Kiislamu huku ajenda yao kubwa ni kurudisha utawala wao ule wa miaka ya 1963 kabla ya Mapinduzi.
Inabidi wananchi wa Visiwani wawe wazalendo na wasipumbazike na matakwa ya wageni aliowaita Mzee Karume “Wamanga wangu hawa”. Mwasia yeyote hawezi kuwa na uchungu na Afrika yetu hii. Hilo tulijue. Mwarabu anatoka Bara Asia ndogo (Asia Minor), hivyo bara ni lile lile la Asia tu. Kamwe hawezi kujiita mwenye asili ya Visiwani kuliko Edington Kisasi ambaye ni Mwafrika halisi.
Hilo sote tuliweke maanani. Wazanzibari wamejijengea utamaduni sasa wa UMOJA, UAMINIANO na USHIRIKIANO na wamesahau CHUKI na UHASAMA wote wa zamani enzi za ukoloni walipobaguliwa kimatabaka ya mbari zao.
Mtazamo wangu mimi ni kwamba huko nyuma enzi za wazee waasisi wa Muungano wetu walisukumwa na historia ya vyama vya siasa enzi za ukoloni. Kila watu walianzisha chama kama njia ya kujikwamua kutoka kwenye adha ya ukoloni ili kujipatia Uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe kimisingi ya ubinadamu na utu wao.
Basi kila chama kilichoundwa kililenga kumkomboa mwananchi huyu wa Unguja na Pemba . Hapa ningependa sana niwaonjeshe vijana wa siku hizi vyama vile vya siasa kule Unguja na Pemba vilianzishwaje na vilifanikiwaje hata leo hii sisi tunakula matunda ya Uhuru na tunaweza kutamba kuwa tu Taifa la Tanzania .
Vyama vikubwa Visiwani vilikuwa ARAB ASSOCIATION, INDIAN ASSOCIATION na AFRICAN ASSOCIATION. Na kutokana na vyama namna hiyo vikajazaliwa vyama kama SHIRAZI ASSOCIATION na UMMA – PARTY.
ITAENDELEA
Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).