Mauji ya raia wasiokuwa na hatia yanaendelea mkoani Mara. Kwa miaka mingi Wilaya ya Tarime ndiyo iliyosifika kwa vitendo hivyo.
Lakini kwa miaka na miezi ya karibuni, Wilaya za Musoma na Butiama, zinaonekana kuipiku Tarime na hata Serengeti. Umeibuka uharamia wa watu kuchinjwa kama kuku. Zamani walikuwa wakiondoka na viungo vya siri, ulimi au hata ngozi (kwa albino), lakini sasa wameibuka na mahitaji mengine-wanaondoka na vichwa.
Miezi kadhaa iliyopita mauaji haya yaliripotiwa katika vyombo vya habari. Ikaelezwa kwamba ndani ya mwezi mmoja, watu zaidi ya 10 walikuwa wameuawa kwa kuchinjwa katika Wilaya ya Musoma na Wilaya mpya ya Butiama.
Kama ilivyo ada, wakajitokeza viongozi wetu. Wakatumia misuli yao yote kukanusha habari hizo walizoziita kuwa ni za uzushi. Wanahabari hawakuchoka, wakaendelea kuripoti mauaji hayo kadri walivyoweza.
Wiki iliyopita watu wengine waliuawa. Miongoni mwao ni mkazi wa Kijiji cha Kwikuba, Tabu Makanya (68). Aliuawa mbele ya mtoto wake. Wataalamu wa saikolojia wanatusaidia kujua hatima ya maisha ya mtoto huyo baada ya kushuhudia mauaji hayo.
Mauaji hayo yakawa yameibua hasira za wananchi, wakiongozwa na vijana waendesha pikipiki ambao waliamua kuandamana hadi Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara wakimtaka aeleze ni hatua gani zinafanywa na jeshi hilo katika kukomesha mauaji.
Kilio chao kikawa, “Mwema (IGP) Kikwete (Rais Kikwete) mko wapi kukomesha mauaji haya? Hatutaki, tumechoka, hatutaki, tumechoka,” walipaaza sauti.
Hasira za vijana hao zilikolezwa na kumbukumbu ya mauaji ya mwenzao wiki iliyopita. Tena basi, wakawa bado na kumbukumbu ya mauji mengine katika Kijiji cha Kabegi, Kata ya Nyakatende wilayani Butiama, ambako Sabina Mkireri, aliuawa. Wauaji waliondoaka na kichwa.
Mauaji haya wakati yakiendelea kufanywa kwa kasi, kumbukumbu za wakazi wengi wa Musoma na Butiama wanakumbuka jinsi raia kadhaa karibu 20 walivyouawa kwa kuchinjwa kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kulipiza kisasi.
Kwanini mauaji haya yanaendelea kutokea mkoani Mara, hususani Musoma na Butiama? Majibu yapo. Suala la mauaji ya aina hii si kwa Mkoa wa Mara pekee. Karibu mikoa yote ya Kanda ya Ziwa inakabiliwa na changamoto hii. Katika Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na hata Mwanza, vikongwe wanamalizwa kana kwamba nchi hii ipo kwa ajili ya vijana tu. Wenye macho mekundu wanauawa, kana kwamba aina hiyo ya macho ni laana.
Mauaji ya kishirikina yameshika kasi mno kutokana na sababu kadha wa kadha. Kuibuka kwa uchimbaji dhahabu na upungufu wa samaki katika Ziwa Victoria , vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa mauaji haya.
Mkoa wa Mara, kama ilivyo mikoa mingi ya Tanzania , ina watu wanaoamini sana katika ushirikina. Bado watu wengi wanaishi katika wingu hilo . Hapa zinahitajika juhudi za kila mmoja wetu-wanasiasa, walimu, viongozi wa dini, wafanyabiashara, wazazi, walezi, na kila mmoja katika jamii yetu, kushiriki katikia vita hii.
Viongozi wa vyombo vya dola wanapopelekwa kufanya kazi katika Mkoa wa Mara, akili mwao hujiaminisha kuwa wanakwenda kufanya kazi na watu wakorofi, wababe na wasio na simile. Hali hiyo imewafanya baadhi ya watendaji, wakiwamo polisi, mara nyingi kuyaona mauaji yanayotokea kama sehemu ya maisha ya kawaida ya wananchi wa mkoa huo. Hii ni dhana potofu
Ukweli wa hili unadhihirishwa na kasi ndogo inayofanywa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara katika kukabiliana na vitendo vya mauaji. Tena, basi watumishi wa Mahakama na Polisi wanaoutambua Mkoa wa Mara wanasema ni sehemu nzuri sana ya kufanya kazi kutokana na uwazi wa watu wake.
Nilipata kuzungumza na Jaji mstaafu Maina. Akanieleza kwamba wakati wa utendaji kazi wake, alipokwenda kusikiliza kesi za mauaji zilizowahusu wakazi wengi wa Mkoa wa Mara, hakupata shida. Hakupata shida kwa sababu mtuhumiwa aliposomewa mashtaka, hakuzungusha maneno, au kwa maneno mengine hakutaka kuisumbua Mahakama. Kama aliua, alikiri bila kusita. Hii inaonyesha kuwa wanachohitaji zaidi hawa ndugu zetu ni elimu tu ya kuwawezesha kutambua na kuthamini haki ya kuishi ya watu wengine.
Nimesema viongozi wa kisiasa na vyombo vya ulinzi na usalama wanastahili lawama kwa utowekaji amani mkoani Mara kwa sababu hawaonyeshi kama wana nia ya kweli ya kumaliza mauaji haya. Hapa ndipo inapojengeka dhana ya kwamba kwao, mauaji wanaona ni sehemu ya maisha ya wakazi wa mkoa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome, mara zote amekuwa mstari wa mbele kukanusha habari zinazotangazwa na kuandikwa kuhusu mauaji wilayani humo. Msome akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika wilaya hiyo, haonekani kuguswa moja kwa moja kwa mauaji hayo. Hilo linathibitishwa na ukame wa vikao na mikutano yenye maudhui ya kukabiliana na wimbi la mauaji. Msome ambaye ni mjumbe wa NEC wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekuwa mwepesi sana wa kufanya mikutano na viongozi wa CCM, lakini imekuwa kinyume linapokuja suala la mauaji.
Hali hii inawafanya wananchi wengi waamini kuwa kwake yeye, mkakati wa kuimarisha chama, na ikiwezekana “kulikomboa” Jimbo la Musoma Mjini, ni wa maana na muhimu zaidi kuliko kuhangaika kutafuta mbinu ya kukomesha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Polisi tunaweza kuwashutumu kwa kushindwa kung’amua mapema njama za mauaji, lakini wakati mwingine tunapaswa kuangalia mazingira ya kazi zao. Hapa lawama zinapaswa kumwendea Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara.
Ni ukweli ulio wazi kwamba polisi mkoani Mara wanafanya kazi katika mazingira magumu sana . Wana magari mapya ya kisasa yasiyokuwa na taili na mafuta. Fungu la mafuta linatolewa kila mwaka. Fungu la ununuzi wa matairi lipo. Lakini kama hivyo ndivyo, inakuwaje magari yasiwe na tairi zinazofaa? Kwanini magari yakose mafuta ilhali shangingi lake lisilohusika kwenye mapambano dhidi ya wahalifu likiwa na mafuta muda wote?
Mauaji mkoani Mara, si tu kwamba yanaleta simanzi na vilio kwa ndugu wa marehemu, bali yanawaathiri hata wale ambao hawana uhusiano wa moja kwa moja na marehemu hao.
Kwa mfano, sifa ya mkoa wa Mara ambayo sasa ni ya mauaji, haiwavutii watumishi wengi wa umma kutaka kwenda kufanya kazi huko. Madaktari hawataki. Walimu hawana shauku tena. Wataalamu wa kada mbalimbali wanauona mkoa wa Mara kama njia ya mkato ya kuwafanya wafike ahera mapema. Mauji yanatokea kila leo, lakini viongozi, hasa DC anasimama kukanusha. Hili haliwezi kukubalika.
Viongozi wa serikali, vyama vya siasa, madhehebu na wananchi wote mkoani Mara wanapaswa kushirikiana katika kukomesha mauaji haya. Badala ya kuhangaika kupanga namna ya kulikomboa Jimbo la Musoma Mjini, wahangaike kulinda maisha ya wananchi mkoani Mara ambao sasa hawana amani kabisa kutokana na mauaji yanayoendelea.
….tamati…