Wiki iliyopita niliandika juu ya hatari ya kuanzishwa kwa sarafu moja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya kukamilisha matakwa ya msingi yenye kujenga mfumo wa kuwezesha sarafu moja kufanya kazi kwa ufanisi. Nilieleza mambo mengi yanayohitaji kufanyika kabla ya kufikia uamuzi wa kuanzisha sarafu moja au la.

Nilisema hakuna jinsi tunavyoweza kuanzisha sarafu moja kabla ya kuwa na Benki Kuu ya Afrika Mashariki. Ndiyo najua ipo Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, lakini benki hii si kazi yake kufanya kazi za Benki Kuu. Nilizungumzia suala la mfumko wa bei, ambapo kuna tofauti kubwa kati ya nchi wanachama.

 

Nilisema hatuwezi kuanzisha sarafu moja kabla ya kuwa na sera zinazofanana katika masuala kama ya deni la taifa, maduka ya fedha (bureau de change), jinsi ya kukokotoa mfumko wa bei, kiwango cha juu cha mfumko wa bei, urali wa malipo, fidia kwa uchumi utakaopoteza, gharama za uchapishaji wa fedha na viwango, mpango shirikishi wa maendeleo kwenye jumuiya, vipaumbele vya uwekezaji, gharama za uendeshaji wa serikali, sheria ya ununuzi, miundombinu na mambo mengine mengi.

 

Nilisema Kenya wanakusanya kodi wastani wa asilimia 24 ya pato la taifa. Tanzania tunajidai tumeongeza kiwango kutoka asilimia 16 katika mwaka huu wa fedha tunalenga kukusanya asilimia 18 ya pato la taifa. Uganda, Rwanda na Burundi usiniulize. Sarafu ya Kenya na Rwanda ina nguvu mara 20 ya madafu yetu. Kenya walikuwa na mfumko wa bei asilimia 29 miezi mitatu iliyopita, lakini hadi naandika makala ya wiki iliyopita mfumko wa bei kwa Kenya ulikuwa asilimia 4.2, hapa kwetu tunakisia asilimia 15.7.

 

Sipendi kuirudia makala ile, ila ingependeza msomaji ukipata fursa ukaipitia upya na kuona nini nilichozunguzia.

 

Hata hivyo, nilipata simu na ujumbe mwingi wenye kunisihi nisiishie kuandika madhara ya sarafu moja pekee, bali ikiwezekana wiki hii nigusie faida za kuwa na sarafu moja. Nakiri kuwa nilipanga kwa dhati kuwa wiki hii nitaandika juu ya faida za sarafu moja. Faida zipo na za haja, ila nasisitiza kuzifikia kwa mfumo wa uchumi kama wa kwetu tunahitaji kwanza kusafisha nyumba yetu.

 

Sitanii, kwa nchi zilizoendelea mfumo wa sarafu moja ni faida mno. Jumuiya ya Ulaya baada ya kuanza kutumia sarafu moja, uchumi wao umekua kwa kiwango kikubwa. Moja ya faida kubwa nchi zinapotumia sarafu moja kwa kila hali hurasimisha mfumo. Ujanja ujanja wa kuchapa fedha na kuingiza kwenye soko bila kuzifanyia kazi au kuuza hatifungani za serikali kisha kuendesha serikali kwa madeni hukoma.

 

Hapa kinakuwapo chombo chenye kudhibiti sera za uchumi mkuu (macroeconomics) wa kila taifa, na hivyo uendeshaji wa uchumi wa nchi wanachama hufuata viwango vya kimataifa bila utaratibu wa kupika takwimu.

 

Faida nyingine ambayo ni ya wazi ni nchi wanachama kujiongezea pato kwa kuacha matumizi ya fedha za kigeni. Hili namaanisha nini? Unapotumia dola kubadilisha kwenda faranga za Rwanda kuna kiasi cha fedha kinachopotea katika kubadili fedha (loss through exchange rate). Kwa maana hiyo, kila mwananchi katika nchi wanachama anaposafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine, hawana sababu ya kubadilisha fedha na kuwafaidisha wenye maduka ya fedha (bureau de change).

 

Kwa nchi za Tanzania, Rwanda, Kenya, Uganda na Burundi, inakisiwa kuwa zina watu wapatao milioni 120. Watu hawa wakitumia sarafu moja na kusafiri wakanunua na kuuza bidhaa na huduma ndani ya nchi tano bila vikwazo ni wazi kuwa mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa na pato la nchi hizi litaongezeka.

 

Sitanii faida nyingine ni wazi kuwa nchi hizi tano zikiamua kutumia sarafu moja kwa mgeni anayetembelea Afrika Mashariki kwake itakuwa rahisi kubadili fedha mara moja tu anapoingia katika moja ya nchi za Jumuiya hii na hivyo kuondoa usumbufu wa kuwa na sarafu tano unapotembelea Jumuiya. Hii peke yake inaweza kuwa kivutio kwa watalii.

 

Faida hii inakwenda mbali zaidi kuwa nchi zinazoizunguka Jumuiya kama Sudan Kusini, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia, Malawi na Msumbiji au hata Afrika Kusini kwa njia moja au nyingine, kwa kutaka au kwa kutotaka zitajikuta zinaanza kutumia sarafu hii. Wafanyabiashara kutoka nchi hizi watajikuta ni rahisi kununua sarafu ya Afrika Mashariki moja kwa moja badala ya kununua dola na baadae sarafu ya Afrika Mashariki.

 

Kwa kufanya hivyo, faida iliyokuwa ikiipata nchi kama Marekani kwa watu wetu kununua dola itahamia kwenye sarafu yetu ya Afrika Mashariki. Hii itapunguza gharama za kufanya biashara (Lower transaction cost) na kuleta utangamano wa fedha katika masoko kwani wananchi wa Afrika Mashariki wanatembeleana mara nyingi kuliko kwenda Ulaya na Amerika.

 

Si hayo tu kama leo tunavyonunua dola, euro, paundi na fedha nyingine za kigeni na kukaa nazo katika nchi zetu, wageni watakaokuja hapa kwetu kwa kuepusha usumbufu siku za usoni wataishia kununua fedha zetu nao kwenda nazo nyumbani kwao kisha kwa njia hii tutapata fedha za kigeni.

Sitanii, kwa mantiki hiyo ukubwa wa eneo la kiuchumi linapokuwa kubwa kwa idadi hiyo ya watu milioni 120 huzaa utangamano wa bei, biashara kati ya sarafu hii (shilingi ya Afrika Mashariki) na majirani na kuua magendo ya fedha (black market) huku ikihakikisha utangamao wa bei.

 

Faida hizi ni za msingi, hoja yangu inabaki pale pale kuwa je, nchi zetu hizi bila maandalizi ya kina zitatufikisha huko? Hatutaishia kuwa na sarafu moja jina bila mifumo? Mimi ni mmoja wa waumini wa muungano kwa maana ya kuwa na eneo pana la kiutawala na watu wakasafiri kutoka eneo moja kwenda jingine bila vikwazo.

 

Mfano hai ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Leo Mtanganyika akitoka Dar es Salaam akaenda Machomane, Pemba, wala hana sababu ya kupitia kwenye duka la fedha kubadili sarafu. Ingekuwa bado tunao utaratibu wa zamani, ni wazi ukitaka kwenda Zanzibar au kinyumbe chake basi ulisitahili kubadili fedha zako kuwa za nchi unayotaka kwenda kisha unapoteza sehemu ya fedha zako.

 

Namaanisha nini kwa kusema unapoteza sehemu ya fedha zako? Leo kama unasafiri kwenda Uganda, unapofika mpakani unabadili fedha kwa wastani wa Sh 100 ya Tanzania kwa 180 ya Uganda. Hata hivyo, unapokuwa unatoka Uganda unarejea kwa kuwa wanajua huna matumizi nazo za Uganda, ukifika mpakani badala ya Sh 100 kwa 180 wanataka ukiwapa Sh 180 ya Uganda wakupe Sh 70 za Tanzania. Hivyo unakuwa umepunjwa shilingi 30.

 

Sitanii, tukiwa na sarafu moja mchezo wa kuibiwa fedha kupitia maduka ya fedha utakoma na nchi yetu itasonga mbele kwa kasi kubwa. Hata hivyo, yatupasa kuwa makini kabla ya kufikia uamuzi huu.