Wanangu, nianze kwa kuwapa hongera ya Krismasi na kwamba mliofanikiwa kufika katika Sikukuu hii, hamna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani si wote waliopata bahati hii ambayo ninyi kwa nafasi na upendeleo wa nafsi zenu kwa Mwenyezi Mungu mmefanikiwa.

Wapo ndugu zenu na watu wengi waliopanga kufanya jambo fulani katika Sikukuu hii lakini hawajaweza, wapo waliopo hospitali na wapo waliotangulia mbele ya haki.

 

Wanangu, kwanza nawapa pole kwa masahibu yote yaliyowakumba katika kipindi hiki cha kumaliza mwaka, na mfululizo wa mahitaji ya fedha yaliyowakumba sanjari na ukame mkubwa mlionao mifukoni katika nchi ambayo ina utajiri uliokifu. Najua kuwa baadhi watapingana na mimi katika usemi huu wa utajiri uliokifu, lakini ukweli ni kwamba watakaopingana na mimi ni wachache kuliko watakaokubaliana na mimi.

 

Wiki jana wanangu nilijaribu kuwaeleza kwa akili yangu ningefanya nini kama ningekuwa waziri wa usalama barabarani. Nilitoa mawazo yangu bila kuangalia upande wa pili wa shilingi kwamba kila jambo lina ugumu na urahisi wake katika utekelezaji, baadhi ya waliochangia katika hotuba yangu ile walisema jambo hilo ni gumu, kwani wanaofanya makosa ni hao hao wenye mamlaka.

 

Hivyo basi, kama rais wangu angeniteua sasa kuwa waziri wa usalama barabarani, naamini ningerudi kwake na kumuomba wizara nyingine na chaguo langu la kwanza lingekuwa wizara ya uwekezaji na ajira. Ningefanya kazi katika wizara hii kwa sababu naamini ningekuwa mtetezi wa wanyonge wengi ambao wanadhulumiwa haki yao ya msingi, ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa katika eneo linalofaa kujengwa kiwanda au kuchimbwa madini.

 

Lakini pia ningelimuomba rais wangu, aniongezee kipengele cha ajira ambazo wawekezaji wanapewa ili kuweza kudhibiti athari zinazojitokeza katika ajira zao, na kuligeuza taifa hili kuwa zizi la wafungwa wa Ulaya kufanya kazi hapa au wasio na ajira na sifa za kutosha kutoka nje ya nchi, kuja kujiita wataalamu katika ardhi yetu tukufu yenye wasomi waliojitosheleza kwa kiwango chao.

 

Ningefanya hii kazi bila woga kwa sababu najua mambo mengi yanayoendelea kwa wananchi wangu na labda yanashindwa kukufikia wewe kutokana na protokali zilivyo, mimi ningeanza kuchukua hatua na wewe ungepata malalamiko kutoka kwa hao wanaobebwa na watu fulani na kuitwa wawekezaji, na ajira zao kiasi kwamba ungefarijika na kujionea fahari kwamba una msaidizi wa kweli katika wizara.

 

Wanangu, naandika waraka huu nikiwa najua nitafanya nini katika wizara hii nyeti kwa taifa letu. Kwanza najua wawekezaji wengi hawafuati sheria za nchi, wanajichukulia sheria mkononi baada ya kuona mkataba wenye vipengele vinavyotubana na ambavyo vimepita katika mazingira ya utatanishi, vinaanza kuota mbawa na kuonesha makucha yake, wanafanya hivyo baada ya mkataba kusainiwa.

 

Wawekezaji hawa wanajua kuwa hawajaja hapa kwa sababu kwao kuna madini, bali wamekuja kwa sababu kwao hakuna madini kwa hiyo wanapaswa kutuheshimu wananchi wenye kumiliki hayo madini ili tushirikiane nao katika utaalamu wa kuyachimba na si kutudharau kana kwamba hatuna uwezo wa kuyachimba. Ningeweka kaulimbiu katika bango la wizara ambalo lingesomeka hivi, “Tanzania tumeishi na madini lakini hatukuwahi kuomba msaada wa kuchimbiwa.”

 

Wanangu, ningeanza kuangalia umuhimu wa uwekezaji katika nchi yetu, ningejiuliza ni sehemu gani muhimu zinazohitaji uwekezaji na kwa manufaa ya nani, ningeangalia upungufu wa zahanati na hospitali, ningeangalia suala la elimu na vitendea kazi, ningeangalia kilimo kwanza na matokeo yake, ningeangalia maji salama na upatikanaji wake, ndipo nirudi katika maduka yao, madini, viwanda vinavyoua viwanda vyetu na mengine mengi.

 

Najua hapo Watanzania wengi wangeniunga mkono, lakini ningeungwa mkono zaidi na Watanzania hawa wenye shida ya ajira na kipato, pale ambapo ningeanza kuangalia nafasi za ajira kwa wageni. Wote wenye sifa ambazo Watanzania wanazo, ningewatimua haraka sana bila kujali masuala ya uhusiano na mataifa waliyotoka kwani wao ndiyo walioanza kutudhalilisha kwa kutuletea vituko.

 

Nisingekubali kuletewa mnyapara anayeshika kiuno kuangalia Watanzania wanaofanya kazi, nisingekubali ubwenyenye na umwinyi huo tuliokataa wakati wa TANU. Nisingekubali kumleta mgeni auze duka la maua kana kwamba hatuna wazawa ambao wanaweza kuhesabu fedha. Nisingekubali kumleta meneja wa baa na anayeuza vinywaji vyetu kisa mwekezaji anahitaji muuzaji kutoka nje. Huko ni kudhalilishana kwa kijinga,

 

Naamini ningegombana na wengi katika hili la watumishi feki kutoka nje, kwani watumishi wa Kitanzania wapo wengi sana na hawana ajira, na sera yetu ya chama ni kuongeza ajira si kupunguza ajira, hapo rais angejua kuwa kampata msaidizi wa kweli.

 

Wanangu, ningekuwa waziri wa uwekezaji na ajira nisingeruhusu akinamama ntilie watoke nje, nisingeruhusu manyapara, wahasibu, madereva, wapishi watoke nje ya nchi. Ningeruhusu walimu, madaktari, wahandisi na taaluma ambazo ni muhimu kwa taifa, nisingekubali kudhalilishwa kwamba hatuna madereva wala wapishi.

 

Wanangu, ningefanya kazi bila kinyongo, ningehamishia uamuzi wote sehemu moja kuondoa ujanjaujanja wa kucheza na makaratasi, na kuifanya nchi yetu kuwa jalala la watu wenye tabia za ajabu ajabu, ambao hawataki kurudi kwao baada ya kuona wamepata unyapara katika mazingira ya kutatanisha.

 

Nisingeruhusu vibali vya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania, nisingeruhusu viwanda ambavyo vinaua viwanda vya Tanzania, nisingeruhusu uwekezaji usio na tija kwa taifa, nisingeruhusu uwekezaji eti kwa sababu ni sera ya dunia, ‘no way’ kila nchi ina utaratibu wake na mipango yake, ningewafanya waelewe hivyo na siyo kutupangia.

 

Krismasi Njema wanangu na heri ya Mwaka Mpya, mimi nimebarizi upenuni nikingoja uteuzi nifanye kazi.

 

Mungu ibariki Tanzania, wabariki viumbe wake.

 

Mzee Zuzu

Kipatimo


Mzee Zuzu,

C/O Duka la Kijiji Kipatimo,

S.L.P. Private,

Maneromango.

Mtanzania Mwenzangu,

Yahoo.com/hotmail.com/excite.com/www.http,

Tanzania Yetu.