Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeutaka umma kuchukua tahadhari juu ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema wananchi wanapaswa kuzingatia hatua zote za kiafya ili kuepukana na maambuzi kwa kuwa ripoti za hivi karibuni zinaonesha kuwa ugonjwa wa malaria na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa yanaongoza.
Kwa mujibu wa wa taarifa ya waziri huyo, Hospitali za Unguja na Pemba zimepokea watu 15,310 kwa ajili ya vipimo. Miongoni mwao, 198 wamekutwa na maambukizi ya magonjwa ya upumuaji, kati yao 29 walikutwa na virusi vya UVIKO-19.
Amesema isivyo bahati, tangu Januari, 2023 hadi leo ndani ya Visiwa vya Zanzibar, jumla ya watu 37 wamekufa kutokana na UVIKO-19.
Waziri huyo ametahadharisha kuwa idadi ya watu wanaoripotiwa kukubwa na changamoto ya upumuaji inaongezeka, hivyo amewataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Ameonya vitendo vya kukumbatiana, kubusu, salamu za kushikana mikono, pia ameshauri kukimbiliana haraka kupata chanjo.
Mazrui amehitimisha kwa kusema kuwa, ingawa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limetangaza kudhibiti UVIKO-19 lakini bado umma unapaswa kuchukua tahadhari, kwa kuwa ugonjwa huo unateketeza uhai wa watu.