Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Kigoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka zaidi ya sh bil 8 katika halmashauri ya manispaa Kigoma-Ujiji ili kuboreshwa miundombinu ya elimu na afya.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo Mwantum Mgonja alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake.
Amesema katika kipindi cha miaka 2 ya Utawala wa Rais Samia wamepokea zaidi ya sh bil 3.5 kwa ajili ya kuboreshwa miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari ikiwemo kujengwa shule mpya za msingi na sekondari.
Amefafanua kuwa fedha hizo zimekarabati na kujenga madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, shule mpya na nyumba za watumishi kwa baadhi ya shule.
Mwantum amebainisha kuwa kupitia mradi wa boost walipokea kiasi cha sh bil 1.5 ambazo zimewezesha kujengwa shule mpya 2 za msingi, vyumba vya madarasa zaidi ya 20 na matundu ya vyoo zaidi ya 20.
Aidha zaidi ya sh bil 1.5 zimetumika kuboresha miundombinu ya shule za sekondari kwa kukarabati na kujenga madarasa mapya, Ofisi za walimu, matundu ya vyoo na mabweni ya wanafunzi katika shule ya sekondari Kigoma na Kasingirima.
Kwa upande wa afya Mkurugenzi amesema walipokea kiasi cha sh bil 3.4 ambazo zimetumika kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujengwa hospitali mpya ya wilaya eneo la Kagera, kujengwa kituo cha afya Gungu na zahanati ya Kamala.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuboresha miundombinu ya afya na elimu hali iliyopelekea kuboreshwa huduma za jamii kwa kiasi kikubwa sana,” amebainisha.
Mwantum ameongeza kuwa serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la halmashauri na nyumba ya Mkurugenzi ambapo zaidi ya sh bil 1 zmeletwa kwa ajili ya kazi hiyo.