Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Desemba 07,2023 amepokea taarifa ya tathimini ya maafa katika Mkoa huo ambayo inatokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha iliyowasilishwa na Wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wanaohusika na maafa kwa kushirikiana na Wataalam kutoka ofisi yake.
RC Chalamila baada ya kupokea taarifa hiyo ameelekeza kila Wilaya kuangalia maeneo ambayo wataalam wa maafa wameainisha kupitia wasilisho lililowasilishwa na kuja na majibu ya nini kifanyike katika maeneo hiyo.
Vilevile RC Chalamila amewataka viongozi wa Wilaya kuhakikisha hakuna Shule itakayofungwa au vituo vya Afya kwa sababu ya athari za mvua, kuendelea kuzibua maeneo ambayo yamezibwa ambayo ni mkondo wa maji hata kama watu wamejenga kuta zibomolewe, kuendelea kutoa elimu kwa umma namna ya kukabiliana na majanga, usafi wa mazingira, pia kuendelea kuweka mipango ya muda mrefu katika kuboresha miundombinu mfano vivuko na madaraja,
Mwisho RC Chalamila amewataka viongozi na wananchi kuelekeza nguvu katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko kwa kuwa mvua zinaponyesha ni rahisi magonjwa ya milipuko kuibuka ikiwemo kipindupindu, vilevile kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake ili Kuimarisha ulinzi na usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam
Aidha kikao hicho cha kuwasilisha taarifa ya tathimini ya maafa katika Mkoa kimehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa Bi Rehema Madenge kamati ya usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Mameya, Sekretarieti ya Mkoa, wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wanaoshughulika na maafa, DAWASA, TANROAD na TANESCO.