· Ni Ahlam Azam Mohamed avunja rekodi kuwa daktari mdogo zaidi
· Madaktari 138 kutunukiwa Shahada Jumamosi
Na Mwandishi Wetu, Jamhurimedia
MWANAFUNZI wa udaktari, Ahlam Azam Mohamed, ameweka rekodi ya kuwa mwanafunzi mdogo kuliko wote kuwahi kutokea nchini kuhitimu Shahada ya Udaktari wa binadamu akiwa na miaka 21.
Mwanafunzi huyo atakuwa miongoni mwa wahitimu 138 wa fani ya udaktai katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) kwenye mahafali ya 21 yatakayofanyika siku ya Jumamosi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam Makamu Mkuu wa chuo cha (HKMU), Profesa Yohana Mashalla wakati akizungumzia mahafali ya 21 ya chuo hicho.
Alisema kuwa wameangalia rekodi kwenye vyuo mbalimbali nchini na hawajaona mtu aliyewahi kuhitimu fani ya udaktari binadamu kwa umri huo.
“Tumeuliza kwenye vyuo mbalimbali vya tiba kuona kama kuna mtu aliyewahi kuhitimu shahada ya udaktari katika umri wa miaka 21 tumekosa. Tumeuliza Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS) lakini wamesema hawajawahi kutokea kwa hiyo tunampongeza Ahlam kwa kuweka rekodi,” alisema
Alisema mwanafunzi aliyewahi kupata Shahada ya Udaktari kwa umri mdogo alikuwa na umri wa miaka 23 hivyi kuwa na miaka 21 Ahlam ameweka rekodi ya aina yake.
Vile vile, HKMU) kimesema kimejipanga kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu, kuongeza tafiti, machapisho na ubunifu ili kwenda na kasi ya dunia kidijitali.
Alisema maboresho hayo yamo kwenye mpango mkakati wa miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2023-2028 ambao umejiita kwenye maeneo sita ya kimkakati.
Profesa Mashalla alisema HKMU imemaliza tathmini ya utekelezaji wa mpango mkakati wa chuo wa miaka mitano wa 2018-2023 mwezi huu kilizindua mpango mkakati wa miaka mitano.
Alisema mpango huo umejikita katika uimarishaji wa utoaji wa elimu na utawala ikiwa ni pamoja na mazingira ya kufundishia na kuongeza udahili, kuboresha mtandao na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu kwa wanafunzi, wanataaluma na wafanyakazi.
Aidha, Profesa Mashalla lisema kwenye mpango mkakati huo chuo kimepanga kuongeza tafiti, machapisho, ubunifu na kuimarisha mifumo ya mipango na fedha.
Alisema katia kutekeleza mpango huo mwaka huu wa masomo chuo kimedahili wanafunzi wapya 465 katika fani mbalimbali.
“Ongezeko hili la wanafunzi katika mwaka wa kwanza litafanya chuo kuwa na jumla ya wanafunzi 1,628 kulinganisha na wanafunzi 1,452 katika mwaka wa masomo uliopita.
Alisema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu watakuwa 296 na kati yao wanawake ni 166 na wanaume ni 130 wakati kwenye Shahada ya Udaktari wa Binadamu wanawake ni 65 na wanaume ni 73.
Profesa alisema kabla ya mahafali hayo kutakuwa na kusanyiko la kitaaluma ambao pia utajadili fursa za kibiashara na mgeni rasmi atakuwa aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene.
“Tumeona badala ya kujadili masuala ya afya peke yake tuita wataalamu wabobezi kwenye masuala ya biashara na uchumi ili nao watoe mchango wao katika utoaji wa watalamu kwenye sekta ya afya,” alisema