Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Chuo cha Wenye Ulemavu Songea na amepongeza uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa chuo hicho kwa ubora wa kazi inayoendelea kufanyika.
Prof. Ndalichako ametoa pongezi hizo jana wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa chuo hicho ambacho ujenzi wa madarasa, karakana, mabweni, Kituo cha maelezi ya awali changamshi kwa watoto wadogo, huduma za marekebisho, mabweni, maeneo ya michezo, bwalo, kumbi na jengo la utawala vikiendelea kujengwa .
Aidha Prof. Ndalichako amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amedhamiria kuleta ustawi kwa watanzania na kutoa vipaumbele kwenye masuala ya Elimu, Afya, miundombinu ya barabara, Maji na kuwapa Afua stahiki zinazosaidia kundi la wenye Ulemavu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa chuo hicho mkoani kwake kwani kitasaidia kuchochea maendeleo ya kielimu mkoani humo.