Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza maboresho katika maeneo ya vyuo vyake vya Ardhi vya Morogoro (ARIMO) na Tabora (ARITA)
Hayo yamebainishwa tarehe Novemba 24, 2023 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda wakati wa Sherehe za Mahafali ya 42 ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) yaliyofanyika chuoni hapo.
Amesema, wizara yake imeanza kufanya Mapitio ya Sera ya Wizara aliyoieleza kuwa ni ya siku nyingi na iliyojaa mapungufu ambapo ameweka wazi kuwa, sera pendekezwa tayari imekamilika na kuwasilishwa kwa wadau pamoja na Baraza la Mawaziri.
“Hivi sasa sera pendekezwa imekwishakamilika na kuwasilishwa kwa wadau mbalimbali, na tayari imekwishawasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri hivyo iko katika hatua nzuri ambapo ndani ya sera hiyo vyuo vimepewa nafasi kubwa katika kuleta mageuzi makubwa ndani ya wizara” alisema Mhe. Pinda
Kwa mujibu wa Mhe. Pinda, Sera hiyo imetoa msukumo mpya wa vyuo vya kati vya Morogoro na Tabora pamoja na Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Taarifa za Kijiografia kilichoanzishwa Dodoma na kuzinduliwa hivi karibuni na Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt Dotto Biteko kuwa na sheria itakayosimamia uendeshaji wa vyuo hivyo.
“Pamoja na kutambuliwa na mamlaka mbalimbali zinazosimamia mafunzo hapa nchini bado vyuo vyetu vilikuwa havina sheria, mfano Chuo cha Morogoro kilikuwa chini ya Chuo cha Ardhi Dar es Salaam ambapo sheria ya chuo hicho ilipotungwa ilikiondolea sifa chuo hiki kutumia sheria ile” alisema Mhe Pinda.
Amemshukuru Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuijali wizara ya ardhi ambapo amebainisha kuwa, mabadiliko yote yanayoendelea katika wizara hiyo ameridhia kuendelea nayo sambamba na kukubali kuidhinisha miradi mikubwa ya kimkakati yenye fedha nyingi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda amesema, chuo cha ARIMO kina changamoto kadhaa zinazoendelea kushughulikiwa na kubainisha kuwa kati ya changamoto hizo baadhi zinahitaji msukumo wa wizara.
Ametoa mfano wa changamoto zinazohitaji msukumo wa wizara kuwa, ni suala la vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi. Amesema, mafunzo ya chuo hicho yanahitaji umahiri wa kutenda na siyo kusimulia hivyo ni muhimu kwa chuo kuwa na vifaa vya kutosha vya kujifunza umahiri huo wanaoenda kuufanya wanafunzi katika soko.
Ameitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya chuo inayoendelea kushughulikiea na chuo ambapo hata hivyo amesema chuo hicho cha ARIMO tayari kinao mpango kabambe alioueleza kuwa ana imani utakuwa muaroabini wa changamoto hiyo.
“Tunashukuru kwamba mwaka huu Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kuanza kutekeleza mpango huo kwa kujenga madarasa mawili” alisema Saguda.
Maadhimisho hayo ya Mahafali ya 42 ya Chuo cha Ardhi Morogoro yalitanguliwa na Maonesho ya Taaluma pamoja na Maandamano ya Kitaaluma yaliyoongozwa na Naibu Waziri Mhe. Geofrey Pinda.
Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kinatoa kozi za upimaji Ardhi pamoja na ushauri wa kitaalamu unaohusu mambo ya ardhi ambapo kozi zinazotolewa ni Jiomatikia katika ngazi ya Cheti na Stashahada pamoja na kozi ya Mipango Miji katika ngazi hizo.