Takribani watu 37 wamefariki katika mkanyagano wakati wa harakati za kuwasajili wanajeshi katika uwanja wa michezo nchini Congo, serikali imesema.
Baadhi ya watu walijaribu kupita kwa nguvu kupitia lango la uwanja wa michezo katika mji mkuu, Brazzaville, na kusababisha mkanyagano.
Wiki iliyopita, jeshi lilitangaza mipango ya kuajiri takribani watu 1,500 kati ya umri wa miaka 18 na 25.
Watu wengi walijeruhiwa katika tukio hilo, taarifa ya serikali ilieleza.
Kulingana na taarifa ya Associated Press, watu 700 kwa siku wamekuwa wakijiandikisha wiki iliyopita katika vituo vya kuajiri.
Ukosefu wa ajira kwa vijana uko karibu asilimia 42 nchini Congo, na vijana wengi wanaona jeshi moja ya maeneo machache ambapo wanaweza kupata kazi.