Na Dotto Mwaibale, JamhuriMedia, Singida
SHEREHE za Mahafali ya 21 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida imemalizika huku idadi kubwa ya wanawake ikizidi kuongezeka mara dufu ikilinganishwa na idadi ya wanaume.
Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo jumla ya wanawake 938 sawa na asilimia 55.2 wamehitimu katika mahafali hayo Kampasi ya Singida ikilinganishwa na idadi ya wanaume 762 sawa na asilimia 44.8.
Akizungumza kwenye mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 17, 2023 Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo amesema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1,700 katika kampasi hiyo kati yao wanawake 938 sawa na asilimia 55.2 na wanaume 762 sawa na asilimia 44.8, wamepata tunuku zao kwenye fani mbalimbali.
Amesema jumla ya Wahitimu ngazi ya Cheti cha Awali ni 567, Astashahada 452, Stashahada 491, na Shahada 190.
Profesa Pallangyo amesema idadi hiyo kubwa ya wahitimu wanawake inadhihirisha kwamba TIA inanaunga mkono jitihada za Serikali, kwa kutoa fursa ya mafunzo pasipo ubaguzi.
Amesema idadi ya wahitimu wote wa TIA kwa mwaka wa masomo 2022/2023 kwa Kampasi za Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Singida ni 13,218 ambapo wanawake ni 7,139 sawa na asilimia 54 na wanaume ni 6,079 sawa na asilimia 46.
Amesema wanaposherehekea mahafali hayo ya Ishirini na moja TIA imepiga hatua kubwa katika uendeshaji wa mafunzo, huduma ya ushauri wa kitaalam, rasilimali watu, pamoja na miundombinu ya kusomea na kufundishia katika kampasi hii ya Singida.
Amesema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa katika Kampasi ya Singida imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Mathalani, katika mwaka huu wa masomo 2023/2024, ulioanza mwezi Oktoba, 2023, jumla ya wanachuo 1,443 wamedahiliwa katika kampasi ya Singida.
Ameongeza kuwa hata hivyo, zoezi la usajili bado linaendelea na lengo ni kudahili wanachuo wapya 2,600 ukilinganisha na udahili wa wanachuo 1,556 katika mwaka wa masomo 2022/2023.
Amesema ongezeko hilo la wanafunzi kwa kiasi kikubwa linatokana na mambo makubwa matatu ambayo ni ubora wa elimu itolewayo inayotokana na mitaala inayowajengea wanachuo wa ngazi zote msingi wa umahiri hivyo kumwezesha mhitimu kuajiriwa na hata kujiajiri pindi anapohitimu masomo yake. Hatua hii huwafanya wazazi na wanafunzi kuichagua TIA.
Utaratibu mzuri wa Serikali wa kuwapangia vyuo moja kwa moja wahitimu wa kidato cha nne waliofaulu na kukidhi vigezo (kupitia TAMISEMI). Mathalan, katika mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya wanafunzi 1,170.
“Ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada hatua ambayo imewezesha watanzania wengi wenye sifa kumudu gharama za masomo. Kwa mfano, katika mwaka huu 2023/2024 Serikali imepanga kuwafadhili wanachuo 810 wa shahada katika kampasi hii ya Singida na hili ni ongezeko la asilimia 15.9 ukilinganisha na wanachuo 699 waliofadhiliwa mwaka 2022/2023,” amesema Pallangyo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo amesema amefurahishwa sana na mpango wa ukuzaji na uendelezaji wa wanafunzi kitaaluma na kitaalamu yaani (Career Development Program) wanaoufanya kwa wanafunzi wa taasisi hiyo kwa kujitengenezea fursa muhimu za kibiashara kwa kuendeleza ubunifu wao ambao ni fursa adhimu kwa wanafunzi hao.
“ Mmedhihirisha umahiri wenu, na kutupa wasaa wa kushuhudia matunda ya juhudi zenu. Hivyo, sina budi kwa niaba ya Serikali, kutoa pongezi zangu za dhati kwa Uongozi, Wahadhiri na wafanyakazi Waendeshaji, kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha mafunzo yenu.
Safari yenu ya mafunzo haikuwa nyepesi; safari yenu ilihitaji uvumilivu, ushirikiano, nidhamu, kujituma na zaidi ya yote kumtegemea Mungu. Kwa pamoja, haya ndiyo yamewawezesha kufikia hatua hii muhimu,” Mwenda alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Serikali.
Aidha, Mwenda aliwaasa wahitimu hao kwamba, hatua waliyoifikia iwe ni chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira na kujiajiri na kuwa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inahimiza sana Taasisi zote kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wanafunzi iwe elimu, ujuzi na maarifa ya kukidhi mahitaji ya soko ili itumike kuleta tija na maendeleo yanayoendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.