Na Mwandishi Wtu JAMHURI MEDIA, Dar es Salaam
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt.Jakaya Kikwete amewataka wadau wa afya nchini ikiwemo serikali kuwekeza kwenye vyuo vya afya kwa kuangalia mitaala inayotumika na njia zinazotumika kufundishia kwani zinapaswa kuendana na wakati uliopo.
Dkt. Kikwete ameyasema hayo Novemba 15 jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa pili wa kisayansi kuhusu afya ya uzazi mama na mtoto wenye kauli mbiu isemayo “Boresha huduma ya afya ya uzazi mama na mtoto na lishe kutokana na matokeo ya kisayansi”
Amesema wataalam wa afya wanapaswa kupewa mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na wakati uliopo.
“Tusimamie kwa dhati mafunzo ya kazi ili kuhakikisha watoa huduma za afya wanaenda na wakati wapate ujuzi mpya wa maendeleo ya sayansi hii itasaidia hata waliosoma zamani waweze kuendana na wakati,”amesema Kikwete
Ameongeza kuwa madaktari bingwa waliopo wanapaswa kuimarishwa ili waweze kufika mpaka ngazi za chini lakini pia kuboresha mfumo wa rufaa kwa wajawazito na watoto na kuweka mfumo mmoja wa gari la wagonjwa.
Amesema pamoja na serikali kuwekeza vizuri katika sekta ya afya bado kuna changamoto ya vifo vya watoto wachanga kwani imepungua kwa kiasi kidogo sana.
“Katika eneo la afya tunapaswa tuwe na kauli mbiu ambayo itakua inawahamasisha kufanyakazi nafikili kauli mbiu hii ya “tujiongeze tuwavushe salama”hii itawapa hamasa ya kufanya kazi,” amesema.
Naye Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema nchi imepiga hatua katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai l00000 mwaka 2015 mpaka vifo 104 kwa kila vizazi hai laki moja mwaka 2022.
Amesema mafanikio waliyoyapata yamechangiwa na mambo makubwa matatu ikiwemo wanawake kuwa na imani na vituo vya huduma ya afya.
“Maudhulio manne ya kliniki ya wajawazito yameongezeka kutoka asilimia 53 hadi asilimia 64 lakini idadi ya wanawake wanaojifungulia vituo vya afya imeongezeka kutoka asilimia 63 mwaka 2015 hadi asilimia 81,”amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Nasor Ahmed Mazlui amesema serikali hizi mbili zikishirikiana zitafikia malengo ya kimataifa kabla ya kufika 2030.
“Tunapaswa wananchi na seriakali kushirikiana ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea katika kupunguza vifa vya mama na watoto madamu nia tunayo basi mafanikio yatapatikana,”amesema Mazlui