Shirika lisilo la Serikali la Kuwezesha Wanawake Kibiashara (EfG) Tanzania, limekuwa mstari wa mbele kusaidia wafanyabiashara wasio katika sekta rasmi, ikiwa ni juhudi za kuinua nafasi zao katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi.
Shughuli za shirika hilo zinawalenga zaidi wanawake walioajiriwa au kujiajiri katika sekta zisizo rasmi, kwa kuwajengea uwezo wa kutambua fursa za masuala yanayohusu maisha yao, utawala na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kutokana na hali hiyo, shirika hilo lilianzisha rasmi mradi wa Sauti ya Wanawake Sokoni Oktoba, 2011, katika masoko 18 yaliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, kuwezesha wanawake kuboresha mazingira ya kuendesha biashara zao. Mradi huo ni zao la utafiti uliofanywa na EfG mwaka 2009.
Mradi huo unalenga kuhamasisha sauti na umoja wa wanawake masokoni kwa kuwajengea uwezo wa kusimamia biashara, kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wanawake na hivyo kuwa washiriki muhimu wa kuendeleza masoko yao kwa kushirikiana na uongozi wa halmashauri za manispaa husika nchini.
Kwa kuwa dira ya shirika ni kuona hakuna vikwazo vya kijinsia na unyonyaji vinavyoathiri wanawake wafanyabiashara, liliona umuhimu wa kuwaandalia waandishi wahabari warsha maalumu iliyofanyika hivi karibuni kutambulisha shughuli zake na kuwawezesha umuhimu wa kuripoti masuala yote yanayohusu sekta zisizo rasmi ikiwamo ya upigaji vita ukatili wa kijinsia kwa wanawake.
Warsha hiyo iliyofadhiliwa na British High Comission kupitia EfG, imewezesha wanahabari kutambua umuhimu wa kampeni ya Ukatili wa Kijinsia (GBV). EfG limeweza kufanya kampeni ya siku 16 (Novemba 25 – Desemba 10, mwaka huu) ya kupinga ukatili wa kijinsia katika masoko ya Ferry, Kigogo Sambusa, Ilala, Buguruni na Kibasira.
Kampeni hiyo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya kilele cha siku ya haki za binadamu duniani.
Mkurugenzi wa EfG, Jane Magigita, amesema kampeni hiyo imekuja baada ya kufanya utafiti katika masoko 10 yaliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala; ambayo ni Buguruni, Kisutu, Ferry, Mchikichini, Ilala, Kibasila, Kigogo Sambusa, Kiwalani, Vingunguti na Tabata Muslim.
Kampeni hiyo iliwezesha kujua idadi ya wafanyabiashara, hali halisi ya wanawake na mazingira ya masoko hayo kwa jumla.
“Utafiti umeonesha kuwa asilimia 31.6 ya wanawake wanaofanya biashara sokoni walishawahi kudhalilishwa na asilimia 92.7 walishawahi kukumbwa na kebehi, kejeli na matusi. Imebainika kwamba udhalilishaji huo unachukuliwa kama jambo la kawaida.
“Asilimia 97.9 ya wanawake hawakuwahi kuripoti polisi matukio yoyote yanayohusu kudhalilishwa, asilimia 78 hawakuwahi kuripoti kwa mtu yoyote kama viongozi wa masoko, asilimia 39.7 wanawake wanashambuliwa mara kwa mara, asilimia nne wanafanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 24.3 wanadhalilishwa kingono. Hii inamaanisha kuwa wanawake wenyewe wanachangia kuendeleza matumizi ya lugha chafu masokoni,” amesema.
Mkufunzi wa masuala ya jinsia na ujasiriamali, Jane Lyatuu, amesema bado wanawake wana fursa ndogo katika kupata mikopo, elimu na kumiliki rasilimali kama vile ardhi, ikilinganishwa na fursa kubwa walizonazo wanaume katika masuala hayo.
Hali hiyo inatoa changamoto kwa wanahabari na wadau wengine kutumia nafasi zao kuwezesha wanawake kufaidika na fursa zilizopo na kuleta maendeleo yanayozingatia usawa wa kijinsia.
Amesema baadhi ya wanawake wanadharau na kukata tamaa katika jamii kutokana na kunyimwa haki za kupata elimu ya biashara na kumiliki rasilimali zenye thamani kubwa.
“Ufumbuzi utawezekana ikiwa kutakuwa na taarifa tenganifu za kijinsia zinazoainisha mwingiliano wa jinsia na kulingana na dhana na taratibu zinazozingatia wajibu, kanuni, uhalali na hali halisi ya mazingira yanayoizunguka jamii kama vile ardhi, miundombinu, elimu, ajira, nakadhalika,’’ ameongeza.
Amesema Serikali kupitia TAMISEMI, ina jukumu la kuendeleza wanawake waliyopo katika sekta zisizo rasmi kuwezesha uelewa kuhusu umuhimu wa kushirikisha makundi maalumu kama vile wanawake, watu wenye ulemavu na wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika shughuli za kiuchumi.
Naye Wakili na Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC), Magdalena Mlolele, amesema utafiti uliofanywa mwaka 2000-2003 ulilenga usaili wa watu 1820 Dar es Salaam na 1450 Mbeya ulionesha ukubwa wa tatizo la ukatili kwa wanawake umekuwa ukijitokeza katika sura tofauti ukiwemo ukatili wa kimwili, kisaikolojia, kiuchumi na kingono.
Ametaja sababu za vitendo vya ukatili katika jamii kuwa vinatokana na mila na desturi zilizopo, sheria kandamizi, sera na matumizi yake, ufanisi mdogo wa vyombo vya kusimamia na kuhudumia waathirika wa ukatili, kutokuwepo usawa baina ya wanawake na wanaume, kadhalika.
Amesema kuwa kuna umuhimu wa wadau kuendelea kujengewa uelewa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na kuhusu utekelezaji wa sheria za kusimamia haki zao kuondokana na tatizo hilo.
Baadaye waandishi walipata fursa ya kuchangia namna watakavyoweza kushiriki vyema kusaidia shirika la EfG katika kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wafanyabiashara wanawake katika masoko mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, mwanahabari Lucas Lukumbo, amesema waandishi wana nafasi kubwa ya kutumia kalamu za kuandika habari na makala mbalimbali za kutetea masuala yote yanayowahusu wafanyabiashara wanawake.
Bila shaka kasi hii iliyoanzaishwa na EfG itasaidia kuwainua wanawake wafanyabishara katika sekta zisizo rasmi Tanzania, kuwa na uwezo wa kutambua haki na fursa zao juu ya masuala yanayohusu maisha yao kiuchumi, kiutawala na kimaendeleo kwa manufaa ya jamii nzima.
0765821621