Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es salaam.
Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Mark Mwandosya, ameishauri serikali kutunga sera ya kudhibiti matumizi ya akili bandia ili kuzuia watu kuitumia vibaya teknolojia hiyo.
Prof Mwandosya ametoa ushauri huo jana wakati wa mjadala ulioandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), jijini Dar es Salaam.
Profesa Mwandosya alisema bila kuwepo udhibiti wa teknolojia hiyo wanaweza kuibuka watu wakaitumia vibaya na kusababisha taharuki kwenye jamii kwa kufanya mambo ambayo hayapendezi.
Amesema teknolojia duniani inaendelea kukua kwa kasi tofauti na matarajio ya watu wengi na baadhi ya nchi wanatumia teknolojia hiyo kutengeneza vifaa kama kompyuta na magari.
“Ukiangalia kwenye viwanda vingi kwenye nchi zilizoendelea kwa sasa mashine ndizo zinafanyakazi ambazo awali zilikuwa zinafanywa na binadamu na zinafanyakazi hizo kwa haraka na kwa ubora zaidi bila matatizo,” alisema Profesa Mwandosya
“Tusipoangalia watu ambao hawawatakii mema binadamu wengine wanaweza kuitumia hiyo tekbolojia vibaya kwa hiyo naona umefika wakati wa kuwa na sera ya kudhibiti kwa sababu uzoefu unaonyesha kwamba biashara inapenda sana kushamiri ambako hakuna sera wala udhibiti, “ alisema
Profesa Mwandosya ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), alisema sasa hivi dunia inaondokana na magari yanayotumia mafuta ambayo yamekuwa yakizalisha hewa ya ukaa unaosababisha joto duniani.
Amesema wazalishaji wa magari wanaondokana na teknolojia ya magari ya sasa yanayotumia petrol na dizeli na kwenda kwenye matumizi ya betri za umeme na wameshaanza kuyatengeneza.
“Bila shaka nasisi Tanzania tutakuwa tumeliona hilo kwa hiyo kwa upande wetu tunapaswa kuanza kutengeneza sera ya matumizi ya magari ya umeme, nimesisitiza hilo kwa sababu Tanzania tumegundua madini ambayo yatatengeneza betri zinazotumika kwenye magari ya umeme,” alisema
Amesema kuna nchi duniani zimegundua teknolojia ambapo mtu anaweza kuchaji betri kwa dakika kumi na kusafiri na gari lake kutoka jijini Dar es Salaam hadi mkoani Mbeya bila kulazimika kuchaji tena.
“Lazima tufanye kitu tusingoje teknolojia itukute wakati hatujajitayarisha tunaweza kuwa kwenye matatizo kwa hiyo lazima wataalamu tuishauri serikali kuja na sera itakayolisaidia taifa tusije kujikuta tunaishi kwenye karne iliyopita,” amesema
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Dk. Nkundwe Mwasaga, alisema teknolojia inatakiwa kuongeza ubunifu na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Sisi tume tunasimamia masuala ya mapinduzi ya kidijitali na kwenye mapinduzi hayo tunaangalia nguzo tano, moja ya nguzo hizo ni kuongeza ujuzi wa watanzania, kuhakikisha mifumo inakuwa salama na inawezakuaminina, kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana maeneo yote bila ubaguzi wowote, kutengeneza uchumi wa kidijitali unaojumuisha watanzania wote na kuhakikisha masuala ya utafii ubunifu na ujasiriamali wa kidijitali unatumiwa vizuri ili tuwe na kampuni nyingi za kisasa,” alisema
Mkuu wa chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga, alisema chuo hicho kimekuwa kikiandaa midahalo kama hiyo mara kwa mara ambayo inatoa suluhisho kwa changamoto kwa kutoa mawazo mbadala.
“Tumeamua tuwe na midahalo kama hii kwasababu sisi wajibu wetu ni kutoa taaluma, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu sasa kama tutafanya tafiti na kuzifungia tu kwenya makabati hatutkuwa tunasaidia taifa letu kwa hiyo tukaona midahalo hii ya mtandaoni kama sehemu ya kutoa taarifa,” alisema Profesa Lwoga