Na Mwamvua Mwinyi, JAMHURI MEDIA, Pwani.
Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri imetatua kero ya kutembea masafa, umbali wa km 4 kufuata elimu ya Sekondari kutoka Kijiji cha Kilimahewa kwenda Kiimbwanindi , wilayani Mkuranga Mkoani Pwani ,ambapo sasa imebaki historia.
Kutokana na kero hiyo iliyodumu kipindi kirefu , Serikali ilianza ujenzi wa shule ya Sekondari Kilimahewa Day ili kuondoa kadhia hiyo.
Hayo yamebainika Mkuranga, katika muendelezo wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge , kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo Mkoani humo.
Anasema ,ameambiwa ujenzi huo kwasasa umefikia asilimia 92 ,unatarajia kukamilika wakati wowote mwezi huu na kugharimu kiasi cha sh.milioni 528.9 .
“Mmemtendea haki Rais, mmetuheshimisha kukamilisha ujenzi huu,ni shule bora miongoni mwa shule bora, tuna mpango fulani na shule hii,sio kama tunabagua”alieleza Kunenge.
Aidha Kunenge amewaasa watoto wa kike kupenda kusoma na kuchukua masomo ya sayansi.
“Watoto wa kike msome ,baadhi ya watu Pwani wanafikiri ukisoma madrasa umemaliza, Rais wetu ni mwanamke pia ametokea ukanda wa Pwani na amesoma uchumi ,mambo mengi na anaiongoza nchi, Mkuu wa Wilaya ni mwanamke amesoma ,someni mfikie malengo yenu,”
Vilevile Kunenge ,aliwaambia wanafunzi hao kuwa Serikali mkoa inatarajia matokeo mazuri ya kitaaluma,na hatarajii kuona mdondoko.
Awali mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir alieleza, kukamilika kwa mradi kutawezesha zoezi la ufundishaji na ufunzaji kukamilika kiufasaha kutokana na miundombinu hiyo.
“Tunashukuru Serikali, kutuletea fedha nyingi Mkuranga, awali watoto walikuwa wakitembea masafa ili kufika Mkamba Sekondari,” Tunashukuru inaenda kukamilika kwani tumefikia asilimia 80,”
Hadija ameahidi wiki mbili kusimamia kukamilishwa kwa ujenzi huo .
Akitoa taarifa ya mradi wa shule hiyo, Kaimu Mkuu wa shule ya Sekondari Kilimahewa Day, Rabii Athumani amefafanua kuwa, shule ilianza machi 2023 baada ya kupata usajili.
Amesema, milioni 528.9 ilipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nane, maabara tatu,jengo la utawala,maktaba,chumba cha Tehama, matundu ya vyoo nane na chumba maalum cha wasichana.
Rabii amesema, kufikia Octoba 2023 majengo bado yapo hatua ya umaliziaji ,mradi umetumia milioni 441.2 na umefikia asilimia 92.
Wakati huo huo, Kunenge amekagua ujenzi wa shule ya Sekondari dkt Samia Suluhu Hassan iliyopo Shungubweni, ambapo utagharimu milioni 595.
Eneo hilo lilikuwa halina shule ya Sekondari tangu Uhuru na kwasasa imekuwa ni shule ya Sekondari ya 37 ikiwa ni ongezeko la shule hizo Mkuranga.
Kunenge alieleza, eneo la Shungubweni ni kipaombele chake , na amebeba dhamana kulifungua eneo hilo.