Ndugu Rais, wako watu walisema mbuzi wa masikini hazai. Wengine wakaongeza eti akizaa huzaa mwaka wa njaa! Ukiuliza ni akina nani hao wanaosema hivyo, utajibiwa eti ni wahenga ndiyo walisema. Sikubaliani nao hata kidogo. Busara za wahenga hazipishani na ukweli!

Baba, kabla ya kuanza shule mimi nilichunga mbuzi. Masikini mmoja alipewa mbuzi mmoja na mjomba wake akamleta tumchungie pamoja na mbuzi wetu. Mbuzi yule alizaa na uzao wake ukazaliana sana. Masikini akaja kuwa tajiri wa mbuzi. Haya ni maneno ya kizazi cha kati kilichotokea kati ya kizazi chetu na kizazi cha wahenga.

Ndugu Rais, matokeo ya kidato cha nne yametangazwa. Mbuzi wa masikini kazaa! Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia binti yangu Margarita matokeo mazuri sana. Mwanangu amepata DIVISION ONE! Kumbe kuzaa kwa mbuzi hakutegemei hali ya mwenye mbuzi. 

Jioni tukiwa tunaangalia taarifa ya habari, ikatangazwa kuwa walimu wakuu wa shule tano zilizofanya vibaya sana katika Mkoa wa Dar es Salaam wamevuliwa madaraka! Binti yangu akaniambia, “Baba, unajua hiyo siyo ‘solution’ (utatuzi wa tatizo)!” Sikumjibu! Sikutaka anichanganye na wajinga. Iweje binti mdogo kama huyu ajue kuwa kuwavua vyeo walimu wakuu siyo utatuzi wa tatizo huku watu wazima ambao labda na shuleni walipitia tu, waone ni utatuzi wa tatizo?

Baba, binti yangu alinifanya niirejee ile busara kubwa ya Waziri Mkuu wetu Kassim Majaliwa. Kiongozi wetu anayejiona ni ‘Mungu’ alisema,

“Ukiniona nimesimama hapa jua ni Mungu mwenyewe amesimama hapa” kisha akamsema kiongozi wa chini yake hadharani kuwa, “Hawa ndiyo vichaa wetu tunaohangaika nao katika mkoa wetu”.

Waziri Mkuu alimwambia yule bwana hadharani bila unafiki kuwa, “Acha kulalamika unapokuwa umeshindwa kutimiza wajibu wako…timiza wajibu wako vinginevyo nitaanza na wewe!” Mwenyezi Mungu amjalie Waziri Mkuu wetu hekima ya kuwaongoza waja wake kwa haki na bila unafiki.

Ndugu Rais, hawa wanaowavua walimu wakuu madaraka, mpaka hali inafikia hapa, wao walikuwa wapi? Walikuwa ofisini kwenye viyoyozi. Waliwahi hata mara moja kuzitembelea hizo shule kuangalia maendeleo yake? Baba na wewe anza na hawa! Bila kuwatumbua ni kuwalea viongozi wabovu na kuwazidishia machungu walio chini yao.

Tangu kuondokewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nchi yetu imekuwa sawa na mbuzi wa masikini. Hata inapotokea kuwa imezaa, dhahabu na madini mengine, gesi na wanyamapori, inakuwa kama ni mbuzi amezaa mwaka wa njaa. Manyang’au na matumbo yao yasiyoshiba wamekuwa wakikomba kila kitu kuanzia vilivyopo juu ya ardhi, majini hadi vilivyopo chini ya ardhi! Wamekomba hata vile vilivyoko katika anga inayotuhusu.

Matumaini yalitokeza ulipoingia Ikulu. Ukawaambia watu wa Mungu kuwa uliikuta nchi ni majipu matupu. Kama itatokea mpaka kuondoka kwetu nchi itakuwa bado ni majipu matupu, tutakuwa tumewatukuza sana waliosema kinachofanyika sasa ni kupuyanga tu! Umesema hutaki kufukua makaburi, sawa. Lakini ukijenga nyumba juu ya kaburi elewa kuwa iko siku utalazimika kuikimbia hiyo nyumba!

Ndugu Rais, kumbe mdomo siyo karakana inayotengeneza maneno yamtokayo mtu. Mdomo unatumika kama chumba cha maonyesho ‘showroom’ kinavyotumika kuoneshea bidhaa zinazotengenezwa. Maneno yamtokayo mtu kiwanda chake kiko katika akili yake. Ndiyo maana wanaposema huyu ni punguani wanamaanisha huyu amepungukiwa kichwani, siyo mdomoni. Lazima tuwe waangalifu sana kwa matamshi yetu.

Ndugu Rais, neno njaa lilikuwa bado kidogo tu liwafanye watu wakabane mashati. Hawa wanasema kuna njaa huku wengine wakisema hakuna njaa.

Wenzetu wengine wako uhamishoni kwa sababu tu walisema kuna watu wanaweza kufa kwa njaa.

Charles Tizeba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ametangaza bungeni kuwa halmashauri 55 zenye watu 1,186,028 nchini zinakabiliwa na upungufu wa chakula kiasi cha tani 35,400. Kati yao watu hao, wameathirika zaidi na wanahitaji tani 3,549 za chakula cha bei nafuu haraka.

Sikusikia akitamka neno njaa hivyo sijui kwake kama nchi ina njaa au la!

Ndugu Rais, nchi ina utajiri mkubwa wa gesi. Utajiri ambao ungeiwezesha nchi kufanya yote iyatakayo kwa ajili ya ustawi wa watu wake. Lakini jambo hili linaonekana halina wa kulisimamia. Tumeendekeza mizozo ya kijingajinga. Kwa uhakika wa utajiri huu wengi wanadhani hata kama siyo yote, mipango mingi ingeachwa tulimalize hili. Badala yake hadithi za mikopo zimekuwa nyingi. Leo tumepewa mkopo wa kiasi kadhaa kutoka nchi fulani au taasisi fulani na kesho tumepewa mikopo mingine.

Viongozi wetu ni nini wanachokiweka kama dhamana kwa mikopo yote hii? Chochote kinachowekwa kama dhamana ni mali ya wananchi. Viongozi hawana haki ya kuweka rehani mali ya wananchi bila ridhaa ya wananchi wenyewe!

Ndugu Rais, ukurasa wa 16 wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu umeandikwa, “Baadhi ya mawaziri wamechoka kiakili na hivyo hupata taabu ya kufikiri kile wanachotaka kukisema hadharani. Waziri anasema, sasa tunachagua tukakope wapi. Kwa baadhi ya viongozi kukopa ni ufahari. Umbali mrefu anaoweza kufikiri ni wapi akakope mkopo mpya ili aweze kulipia mkopo wa zamani kidogo”.

Kwa mawazo ya viongozi kama hawa mbuzi wa masikini hawezi kuzaa; na ikitokea akazaa utakuwa ni mwaka wa njaa! Ukimya wa Serikali kuhusu gesi una kishindo kikubwa. Viongozi wetu lazima wafahamu kuwa huku mitaani kuna vi-manenomaneno visivyokuwa na ukweli vingi. Mara oh! Gesi imekwishauzwa yote si mnaona mikataba ilivyo mingi tena yote inafanywa kwa siri! Mara oh! Ziko meli zinazochukua gesi juu kwa juu kutoka kule kule kisimani. Maneno kama haya ndiyo huwafanya wananchi ambao hawaambiwi ukweli kudhani kuwa ni ya kweli na hivyo kujenga hisia mbaya juu ya Serikali yao. Ni muhimu kwa Serikali kusimama hadharani na kusema ni nini hasa kinachoendelea kuhusu gesi.

Baba waambie ukweli watu wako, ni kipi kinafanya hata wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wazuiwe hata kuiona tu hiyo mikataba wanaoingia viongozi wetu na wageni? Baba badilika! Watanzania wanataka mabadiliko ili mbuzi wao azae!