Yaeleza hatua ilizochukua kwa wafanyakazi na Kampuni zilizosababisha hasara
Ma Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali imeeleza hatua stahiki zilizochukuliwa kufuatia hasara iliyojitokeza kwa Serikali kupitia Kampuni ya mafuta ya TANOIL ikiwemo hatua ya kuwasimamisha kazi wafanyakazi wanne wa TANOIL.
Hatua hizo zimeelezwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa hoja zilizowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (CAG).
Ametaja hatua nyingine iliyochukuliwa ni Kampuni zilizosababisha hasara hiyo kupisha TAKUKURU kufanya kazi yake.
Amesema, Serikali inatambua umuhimu wa Sekta ya Mafuta nchini kwa uchumi wa nchi na ndio maana imechukua hatua kwa wote waliohusika kusababisha hasara ya takribani shilingi bilioni 7 kwa TANOIL.
“Nipende kuwataarifu waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeshachukua na inaendelea na hatua za ndani kufuatia TANOIL kusababisha hasara kwa Serikali,” amesema Waziri Kapinga.
Bunge linaendelea na majadiliano ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (CAG).