*Kasi ujenzi nyumba za makazi, vitegauchumi yaongezeka
*Nyumba 1,000 kwa wenye kipato kidogo kujengwa mikoa 14
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kutimiza dhima ya kuanzishwa kwake kwa kuhakikisha linatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na vitega uchumi.
Kwa sasa NHC imekamilisha baadhi ya miradi, mingine inaendelea na pia imejiwekea mpango mkakati wa kuendelea na ujenzi wa nyumba kwa mahitaji mbalimbali nchini.
Miradi iliyokamilika
Nyumba za Makazi Meru
Nyumba za Makazi Meru zipo jijini Arusha. Kumejengwa ghorofa sita za kisasa zenye nyumba 48 ambazo tayari baadhi ya wamiliki wameanza kuishi na wengine wanaendelea kuingia. Mradi huu umewalenga watu wa kipato cha kati. Kila nyumba ina ukubwa wa mita za mraba 169. Unatarajiwa kuwa na wakazi 240. Huduma zinazopatikana ni pamoja viwanja vya michezo kwa watoto, mtandao wa barabara, sehemu za waenda kwa miguu, maeneo ya kujihifadhi wakati wa dharura, na mfumo wa uteketezaji taka.
Majengo ya Biashara
Lumumba Plaza
Lumumba Plaza ni jengo la kibiashara lililojengwa mjini Kigoma. Lina ukubwa wa mita za mraba 5,550. Ni maalumu kwa matumizi ya biashara mbalimbali kama benki, maduka makubwa, maduka ya kawaida na sehemu za ofisi ambazo ni ghorofa ya pili hadi ya nne. Huduma nyingine zinazopatikana ni za maegesho ya magari, jenereta na sehemu ya kuhifadhi maji.
Miradi inayotekelezwa
Nyumba za makazi:
Kibada Village
Mradi wa ujenzi wa nyumba 216 unaendelea kwa kasi. Kila nyumba itakuwa na vyumba kati ya viwili na vitatu, kimoja kikiwa “en-suite”. Mradi umewalenga watu wa kipato cha chini. Vyumba viwili, kila kimoja kina ukubwa wa mita za mraba 56. Nyumba zenye vyumba vitatu kila moja ina ukubwa wa mita za mraba 70. Wakazi 1,080 wanatarajiwa kunufaika na mradi huu. Huduma zitakazopatikana Kibada ni pamoja na maegesho kwa kila nyumba, zahanati, shule ya awali, kiwanja cha michezo kwa watoto, uwanja wa mpira na eneo la maduka na soko.
Nyumba za Makazi Chang’ombe
Nyumba za makazi Chang’ombe zipo katika eneo la Chang’ombe, Dar es Salaam. Kunajengwa jengo moja kubwa lenye vyumba 20. Kila nyumba itakuwa na ukubwa wa mita za mraba 62. Wakazi 100 wanatarajiwa kufaidika katika mradi huu. Baadhi ya huduma muhimu zitakazokuwapo ni maeneo ya michezo kwa watoto, sehemu za kufulia nguo, hifadhi kubwa ya maji na mfumo wa uteketezaji taka.
Mradi wa Nyumba za Makazi Ubungo
Mradi huu upo eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam. Kunajengwa mafleti manne yenye nyumba za makazi 80. Mradi umewalenga watu wenye kipato cha kati, na tayari zote zimeshapata wanunuzi. Kila nyumba itakuwa na ukubwa wa mita za mraba 54. Watu 400 watanufaika kwa mradi huu. Huduma muhimu zinazopatikana ni pamoja na maeneo ya michezo kwa watoto, sehemu za kufulia na kuanika nguo, maduka, ofisi za meneja mradi, hifadhi ya maji na mfumo wa uteketezaji taka.
Mradi wa Makazi wa Levolosi
Mradi wa Levolosi upo katika Jiji la Arusha ukiwa ni wa mafleti ya kisasa matano yenye nyumba za makazi 98. Nyumba zote zimeshauzwa. Mradi huu umewalenga watu wenye kipato cha kati. Kila nyumba itakuwa na ukubwa wa mita za mraba 62. Wakazi 490 wanatarajiwa kunufaika. Mradi una huduma za viwanja vya michezo kwa watoto, sehemu za kufulia na kuanika nguo, ofisi za meneja mradi, hifadhi kubwa ya maji iliyojengwa chini ya ardhi na mfumo wa uteketezaji taka.
Mradi wa Makazi Mchikichi
Mradi wa Mchikichi upo jijini Dar es Salaam, ukiwa na mafleti matatu ya kisasa yenye nyumba 48 za makazi. Nyumba zote zimeshapata wanunuzi. Mradi utawanufaisha watu wa kipato cha kati. Kila nyumba ina ukubwa wa mita za mraba 115. Wakazi 240 watanufaika. Utakapokamilika, huduma zitakazopatikana ni pamoja na maeneo ya michezo kwa watoto, sehemu za kufulia na kuanika nguo, ofisi ya meneja wa mradi, hifadhi ya maji, na sehemu ya uteketezaji taka.
Mradi wa Makazi Medeli
Mradi wa Medeli unajengwa katika Manispaa ya Dodoma ukiwa na nyumba 150 za makazi. Awamu ya kwanza imeshakamilika. Awamu ya pili inaendelea. Walengwa ni watu wa kipato cha kati. Kila nyumba ina ukubwa wa mita za mraba 115. Wakazi 750 watanufaika. Huduma zitakazopatikana ni pamoja na maeneo ya kuchezea ya watoto, sehemu za kufulia na kuanika nguo, maduka, ofisi ya meneja mradi, hifadhi ya maji na mfumo wa uteketezaji taka.
Mradi wa Mindu
Mradi wa Mindu upo Upanga katika Mtaa wa Mindu jijini Dar es Salaam. Ni wa ghorofa moja kubwa lenye nyumba 60 za makazi. Mradi umewalenga watu wa kipato cha juu. Kila nyumba ina ukubwa mita za mraba 141. Kutakuwa na wazi 300. Huduma zitakazopatikana ni pamoja na bwawa la kuogelea, klabu ya mazoezi ya viungo, nyumba zote zitakuwa na viyoyozi, ving’amuzi vya moto, maegesho ya magari, jenereta la dharura kwa saa 24, mfumo wa ukusanyaji taka, ofisi ya meneja mradi, na huduma ya uhakika ya maji.
Mradi wa Ufukweni
Mradi huu ni wa kipekee kabisa hapa nchini na katika ukanda huu wa Afrika. Ni wa ujenzi wa huduma za biashara. Upo katika makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Ufukweni, jijini Dar es Salaam. Jengo lina ukubwa wa mita za mraba 13,810. Linafaa kwa biashara mbalimbali, lina ghorofa mbili chini ya ardhi kwa ajili ya maegesho ya magari, benki; na ghorofa ya kwanza hadi ya nane ni kwa ajili ya ofisi mbalimbali. Huduma kama za maegesho, jenereta ya uhakika na hifadhi ya maji, zinapatikana.
Miradi ijayo
Nyumba za Makazi
Mpango wa nyumba za bei nafuu. Mpango huu utatekelezwa katika mikoa 14. Wastani wa nyumba zitakazojengwa ni 1,000. Zitakuwa ni nyumba moja kwa mbili zenye vyumba vitatu kila moja. Maeneo ya mradi huu ni Tanga (Mkinga), Manyara (Babati), Arusha (Monduli na Longido), Morogoro (Mvomero), Dodoma (Kongwa), Singida (Unyankuni), Katavi (Ilembo), Lindi (Mtanda), Geita, Ruvuma (Songea-Mkuzo), Mbeya (Iwambi), Kigoma (Mlole), Mwanza (Buswelu) na Kagera (Muleba)
Mradi utawalenga watu wa kipato cha chini. Nyumba yenye vyumba viwili itakuwa na ukubwa wa mita za mraba 56. Zenye vyumba vitatu zitakuwa na ukubwa wa mita za mraba 70. Huduma zitakazopatikana kwenye mradi huo ni pamoja na maegesho kwa kila nyumba, zahanati, shule za awali, viwanja vya michezo vya watoto, viwanja vya mpira na maeneo ya maduka na soko.
Mradi wa Makazi Kurasini
Mradi huu wa Kurasini jijini Dar es Salaam utajengwa mafleti yenye nyumba 80. Mradi utawalenga watu wa kipato cha kati. Kila nyumba itakuwa na vyumba viwili vya kulala vyenye wastani wa mita za mraba 89. Makadirio ni kuwanufaisha wakazi 400. Huduma zitakazopatikana ni pamoja na maegesho ya magari, baiskeli, pikipiki na kwa watu wenye ulemavu, maduka ya kisasa, klabu, ofisi za meneja mradi, sehemu za kujilinda wakati wa dharura na viwanja vya michezo kwa ajili ya watoto.
Ngano Village
Mradi utakuwa na nyumba 120 zenye vyumba vitatu kwa kila nyumba. Jengo litakuwa na urefu wa ghorofa 14 hadi 16. Wastani wa wakazi 600 wanatarajiwa kunufaika. Ukubwa wa nyumba yenye vyumba vitatu utakuwa wastani wa mita za mraba kati ya 100 hadi 120.
Huduma nyingine ni maegesho, bwawa la kuogelea, kituo cha mazoezi, viwanja vya michezo kwa watoto, ofisi za meneja wa mradi, maeneo ya kujihifadhi wakati wa dharura, na mfumo wa uteketezaji taka.
Ushindi Place (Victoria)
Mradi huu unatarajiwa kujengwa flati yenye nyumba 180 ambako kila moja itakuwa na vyumba vitatu vya kulala. Vyumba viwili kila kimoja kitakuwa na ukubwa wa wastani wa mita za mraba 70 hadi 80. Nyumba yenye vyumba vitatu zenye ukubwa wa wastani zitakuwa na ukubwa wa mita za mraba 90 hadi 100. Wakazi 900 wanatarajiwa kunufaika. Kutakuwa na nyumba sita za ju ya paa (upenu-mbili kwa kila jengo). Kila mmoja utakuwa na ukubwa wa mita za mraba 200 hadi 250. Utakuwa na bwawa la kuogelea, jacuzzi, maktaba, ofisi, sehemu za mazoezi, vyumba vya watumishi, na kadhalika.
Golden Anniversary Towers (Ofisi za zamani za NHC Upanga)
Mradi huu wa aina yake utajengwa Upanga, Dar es Salaam mahali kulipokuwa ofisi za NHC.
Kutajengwa majengo mawili (minara) yenye ghorofa 20 hadi 25. Majengo hayo ni kwa ajili ya makazi. Wakazi 1,250 wanatarajiwa kunufaika. Kutakuwa na huduma zote muhimu zikiwamo za maktaba, ofisi, Jacuzzi, maduka, mighahawa, na kadhalika.
Majengo ya Biashara
Singidani Complex
Singidani Complex ni jengo la kibiashara mjini Singida. Jengo lina ukubwa wa mita za mraba 5,388. Litakuwa na sehemu za biashara, benki, maduka makubwa, na ofisi.
Morogoro
Jengo la kisasa la biashara litajengwa katika Manispaa ya Morogoro. Lina ukubwa wa mita za mraba 7,800. Nyumba ya chini pamoja na ghorofa ya kwanza ni kwa ajili ya benki, maduka, mighahawa; ilhali ghorofa za juu ni kwa ajili ya matumizi ya ofisi mbalimbali. Litakuwa na sehemu za maegesho ya magari, jenereta, hifadhi ya maji na huduma mbalimbali.
Mpanda Paradise
Jengo hili lipo Mpanda mkoani Katavi. Lina ukubwa wa mita za mraba 5,550. Ni kwa ajili ya biashara.
Sehemu ya jengo la chini ni kwa ajili ya matawi ya benki mbalimbali, maduka; na ghorofa za juu ni kwa ajili ya ofisi. Huduma zote muhimu-maji, jenereta, na maegesho vinapatikana.
Moshi
Moshi Complex ni jengo la biashara lililopo katika Manispaa nya Moshi. Lina ukubwa wa mita za mraba 5,763. Jengo la chini ni kwa ajili ya matawi ya benki mbalimbali, maduka; na ghorifa za juu ni kwa ajili ya ofisi. Kama yalivyo majengo mengine ya NHC, hili nalo litakuwa na huduma zote muhimu za maegesho, maji, jenereta na kadhalika.