Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Oktoba 31,2023 ameongoza kikao maalum cha tathimini ya ukusanyaji mapato katika Mkoa huo kwa kipindi cha robo mwaka wa fedha 2023/2024 ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Arnatoglo Mnazimmoja na kuhudhuriwa na wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, TRA na Sekretarieti ya Mkoa ikiongozwa na Katibu Tawala Mkoa Bi Rehema Madenge.
RC Chalamila katika kikao hicho alipata wasaa wa kusikiliza wasilisho la hali halisi ya mapato katika Halmashauri na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwataka kuongeza Kasi ya ukusanyaji mapato, kuthibiti matumizi, kuwa na ubunifu wa kubuni vyanzo vipya vya mapato pia kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
“Kila Halmashauri ijipange kukusanya zaidi ya makisio yao waliyojiwekea kwa mwaka, mfano jiji makisio yake yalikuwa ni Bilioni 89 lakini uko uwezekano mkubwa wa kukusanya zaidi ya Bilioni 120 kutokana na mikakati yake” amesema Chalamila.
Aidha RC Chalamila amesema vikao vya tathimini ya mapato kuanzia sasa vitakua vinafanyika mara kwa mara na ratiba maalum ya vikao hivyo itatolewa na katibu Tawala wa Mkoa.
Vilevile Mkuu wa Mkoa amesema makusanyo ya mapato yaendane na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ni aibu kwa Mkoa huu ambao kila kitu kipo unashindwa kukamilisha miradi ya maendeleo.
Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa Rehema Madenge amepongeza Halmashauri kwa asilimia kubwa zimefikia lengo la robo ambapo amewataka kuendelea kusimamia vema mapato na matumizi, kuziba mianya ya upotevu wa mapato katika mifumo, kutenga asilimia 10 vilevile mkoa huo unatakiwa kuwa na miradi ya mfano, mizuri na yenye tija kwa masilahi mapana kwa umma.