Na Mwandishi Wetu, JamburiMedia
Wataalamu wa sekta afya wanahitaji msaada wa ujuzi na maarifa kuliko aina nyingine ya misaada kwa kuwa itasaidia kusambaza maarifa hayo kwa vizazi na vizazi na hatimaye kusaidia kuokoa maisha.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mafunzo maalumu ya siku tano ya wataalamu wa upasuaji kwa watoto (Paediatric Surgery) yanayohusisha washiriki kutoka hospitali zilizo mikoa ya pembezoni mwa Tanzania, ambayo yanatolewa na wakufunzi kutoka Oxford University kwa ufadhili wa shirika la Kids-OR
“Kabla ya mtaalamu kutoka hospitali za pembezoni kumpa rufaa mtoto kwenda kwenye hospitali ya juu inabidi ahakikishe kuwa amempa huduma nzuri za awali ili kuokoa maisha na kumsaidia afike salama hii inawezekana tu ikiwa mtaalamu husika atakuwa na maarifa ya kutosha” amesema.
Prof. Janabi amewaasa washiriki kutumia vizuri muda wa siku tano wa mafunzo hayo ili waweze kunufaika na maarifa ambayo yatasaidia kuokoa maisha ya watoto
Kwa Upande wake Mkufunzi Mkuu wa Mafunzo hayo Prof.Kokila Lakhoo amesema kuwa yalifanyika mafunzo ya majaribio nchini India katika mji wa Valoo, mji ambao changamoto zake zinafanana na mazingira ya Afrika
Prof. Lakhoo amesema baada ya mafunzo majaribio waliwaalika wataalamu wa upasuaji kutoka nchi sita za Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Ghana na Malawi ambao walijifunza na kuhitimu hivyo wao ndio wakufunzi wenza katika mafunzo haya yanayoendelea.
Amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuwa mwenyeji wa mafunzo na mafunzo yajayo yatafanyika Ethiopia na kwamba wataalamu watakaotokana na mafunzo haya ndio watakuwa wakufunzi haitahotajika tena wataalamu kutoka India.